Tafuta

Papa Francisko: Siku ya Chakula Duniani 2021: Maboresho ya mifumo ya chakula duniani: Baharini, Mezani, Upotevu na Utupaji wa Chakula. Papa Francisko: Siku ya Chakula Duniani 2021: Maboresho ya mifumo ya chakula duniani: Baharini, Mezani, Upotevu na Utupaji wa Chakula. 

Ujumbe wa Papa Francisko Maadhimisho Siku ya Chakula Duniani 2021: Kashfa ya Njaa!

Papa Francisko: Kuna haja ya kufanya mabadiliko katika mifumo yote ya chakula duniani. Maeneo ya maboresho: Baharini, Mezani, Upotevu na Utupaji wa Chakula. Mtindo wa maisha na ulaji una athari kubwa katika mazingira. Watu waongozwe na kanuni maadili , kwa kuchagua chakula na kuwawezesha vijana kuona kwamba, wanaweza kuchangia katika mapambano ya baa la njaa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya 41 ya Chakula Duniani, tarehe 15 Oktoba 2021 yananogeshwa na kauli mbiu: “Zingatia Uzalishaji na Mazingira Endelevu kwa Lishe na Maisha Bora.” Athari za mabadiliko ya tabianchi yaani: ukame wa kutisha, mafuriko, majanga asilia, vita, ghasia, kinzani na machafuko mbalimbali, ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kusababisha ongezeko kubwa la baa la njaa, ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula na umaskini duniani. Hii ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa, ili kuweza kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Ili kufanikisha malengo haya, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha pekee kwa uzalishaji katika sekta ya kilimo, kwa kuwawezesha pia wakulima wadogo wadogo wanaochangia uhakika wa usalama wa chakula kwa familia zao pamoja na kujipatia kipato cha kuweza kuboresha hali ya maisha ya watu wengi duniani. Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO linabainisha kwamba, hata kabla ya kuzuka na hatimaye kupamba moto kwa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 kumesababisha ongezeko la watu wanaosiginwa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha.

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu milioni 700 wanaoshambuliwa na baa la njaa duniani. Changamoto mamboleo ni uhakika na usalama wa chakula duniani, hali ambayo inapaswa kwenda sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na maboresho ya maisha ya watu duniani. FAO inapenda kuwekeza zaidi katika teknolojia rafiki, utunzaji bora wa takwimu, utawala bora pamoja na maboresho ya taasisi mbalimbali zitakazosaidia katika mchakato wa mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo wa kutisha duniani. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Dr. QU Dongyu, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, anasema, maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yanaikutanisha Jumuiya ya Kimataifa mubashara na changamoto ya baa la njaa duniani. Baba Mtakatifu anasema kwamba, Mwezi Septemba 2021 huko New York, nchini Marekani, Umoja wa Mataifa umefanya mkutano kuhusu: Mifumo Endelevu ya Chakula mintarafu Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030.

Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yameendelea kusababisha uharibifu kwa mazingira na ukame kwa maisha ya kiroho. Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuzalisha chakula kingi na cha kutosha mahitaji ya watu, lakini kwa bahati mbaya bado kuna umati mkubwa wa watu wanaopekenywa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha, ukosefu wa maji safi na salama pamoja na tiba muafaka kwa magonjwa yanayowasumbua binadamu. Hii ni kashfa inayokwenda kinyume cha haki msingi za binadamu. Maadhimisho ya Siku ya 41 ya Chakula Duniani, tarehe 15 Oktoba 2021 yananogeshwa na kauli mbiu: “Zingatia Uzalishaji na Mazingira Endelevu kwa Lishe na Maisha Bora.” Haya ni mambo msingi yanayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa ili walau kila mtu aweze kupata lishe bora na ya kutosha kwa gharama nafuu. Baba Mtakatifu anasema Jumuiya ya Kimataifa inahitaji mshikamano mpya unaowahusisha watu wote. Watu wote wanaweza kushirikiana kama vyombo vya Mwenyezi Mungu kwa ajili kutunza mazingira kila mmoja kadiri ya utamaduni, mang’amuzi, shughuli na vipaji vyake. Rej. Laudato si 14.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu bilioni 3 ambao hawapati lishe bora na watu bilioni 2 wana uzito wa kupindukia kutokana na lishe duni sanjari na ukosefu wa mazoezi ya viungo. Ili kuweza kukabiliana na changamoto zote hizi, Baba Mtakatifu Francisko anasema kuna haja ya kufanya mabadiliko katika mifumo yote ya chakula duniani. Maeneo makuu manne yanahitaji kufanyiwa maboresho; Baharini, Mezani, Upotevu na Utupaji wa Chakula. Mtindo wa maisha na ulaji una athari kubwa katika mazingira, mambo yanayohitaji kuongozwa na kanuni maadili na utu wema, kwa kuchagua chakula pamoja na kuwawezesha vijana wa kizazi kipya kuona kwamba, wana mchango wanaoweza kuutoa katika mapambano ya baa la njaa duniani. Kila mtu anaweza kuchangia katika maboresho haya kwa kuwa na maisha ya kawaida; kwa kufahamu na kutunza vyema mazingira nyumba ya wote. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 imekuwa ni fursa ya kubadili mwelekeo na kuwekeza zaidi kwenye usalama na uhakika wa chakula duniani. Mchango wa wakulima wadogo wadogo upewe kipaumbele cha pekee, kwa kuwawezesha kupata pembejeo mpya na za kisasa zitakazowawezesja kupambana na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote.

Kuwepo na ongezeko la uzalishaji wa chakula pamoja na kuunga mkono mnyororo wa ongezeko la thamani katika uzalishaji wa mazao ya chakula. Mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo wa kutisha yanahitaji kuvuka mantiki ya soko linalojikita zaidi katika kupata faida kubwa. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa kwa Dr. QU Dongyu, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, Chakula kisiwe ni bidhaa na badala yake, Jumuiya ya Kimataifa ijielekeze zaidi katika ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kanisa Katoliki na Vatican katika ujumla wake, itaendelea kuunga mkono jitihada za FAO pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaotaka kuhakikisha kwamba, baa la njaa linatoweka katika uso wa dunia. Wale wote wanaoendelea kupandikiza mbegu ya matumaini watambue kwamba, wanaungwa mkono na Baba Mtakatifu Francisko.

Mbinu Mkakati na Ushauri wa FAO: Kupunguza upotevu na utupaji wa chakula ni muhimu katika dunia ambayo mamilioni ya watu wanalala njaa kila siku, limesema Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO.  Shirika hilo limesisitiza “Tunapopunguza utupaji chakula, tunaheshimu kuwa chakula hakipatikani kirahisi kwa mamilioni ya watu ambao wanalala njaa kila uchao. Ni juu yetu kubadili tabia zetu ili kufanya upotevu wa chakula kutokuwa ndio mfumo wa maisha maisha.” FAO imeainisha hatua rahisi ambazo kila mmoja anaweza kuchukua ili kukithamini na kukienzi chakula: Tumia lishe bora na endelevu Maisha yanaenda kwa kasi na kuandaa chakula chenye lishe inaweza kuwa changamoto, lakini milo yenye afya si lazima itumie muda mrefu kuandaliwa. Mtandao umejaa mapishi ya haraka yenye afya ambayo unaweza kushiriki na familia yako na marafiki zako.

Nunua chakula kile tu unachohitaji. Panga bajeti ya chakula chako. Fanya orodha ya ununuzi na uizingatie, na epuka ununuzi wa kukurupuka. Sio tu utapoteza chakula kidogo, bali pia utaokoa pesa yako kwa ajili ya matumizi mengine. Chagua matunda na mboga zenye mwonekano mbaya. Kammwe usihukumu chakula kwa mwonekano kwake wa nje. Matunda na mboga zenye umbo la kushangaza au zilizopondwa mara nyingi hutupiliwa mbali kwa sababu hazifikii viwango vya kupendezesha macho. Usijali kwani ladha ni ileile. Tumia matunda yaliyokomaa kwa kutengeneza urojo, juisi na kuyala jinsi yalivyo. Hifadhi chakula kwa busara. Sogeza bidhaa za zamani mbele ya kabati yako au jokofu na mpya weka nyuma. Tumia vyombo visivyoingiza hewa kuweka chakula wazi kwenye jokofu na hakikisha vikasha vimefungwa ili kuzuia wadudu kuingia. Kuelewa uwekaji wa chakula hadi lini. Kuna tofauti kubwa kati ya tarehe "bora kabla ya " na "matumizi ifikapo ". Wakati mwingine chakula bado ni salama kula baada ya tarehe isemayo "bora kabla ya", lakini ni tarehe isemayo "matumizi ifikapo" ambayo inakuambia wakati gaani ni mwisho wa kutumia au sio salama tena kula. Angalia maandishi yanayoelezea kuhusu chakula hivyo kwa ajili ya chakula vitu au viungo visivyofaa kwa afya kama vile mafuta na vihifadhi na epuka vyakula vilivyoengezwa sukari au chumvi.

Anza kidogo. Chukua sehemu ndogo nyumbani au shiriki sehemu kubwa kwenye mikahawa. Penda mabaki yako.  Endapo hutoweza kula kila kitu, kihifadhi kilichosalia kwenye jokofu kwa ajili ya baadaye au tumia mabaki hayo kuandaa mlo mwingine. Geuza mabaki ya chakula kuwa mbolea. Badala ya kutupa mabaki ya chakula chako, yatumie kama mbolea. Kwa njia hii unarudisha virutubishi kwenye mchanga na kupunguza kiwango cha uzalishaji wako wa hewa ukaa. Heshimu chakula. Chakula kinatuunganisha wote. Ungana tena na chakula kwa kujua mchakato wa kukiandaa. Soma juu ya uzalishaji wa chakula na uwajue wakulima wako. Saidia wakulima wa eneo lako kwa kununua mazao ya ndani, unasaidia wakulima wa familia na wafanyabiashara ndogo ndogo katika jamii yako. Unasaidia pia kupambana na uchafuzi wa mazingira kwa kupunguza umbali wa kusafirisha chakula kwa malori na magari mengine.

Kula samaki kwa wingi. Kula zaidi aina mbalimbali za Samaki kama vile mackerel au sill, badala ya zile zilizo katika hatari ya kuvuliwa kupita kiasi, kama papa au jodari. Nunua samaki waliovuliwa au kufugwa kwa njia endelevu, kama samaki waliowekwa alama ya kujali mazingira au waliothibitishwa. Tumia maji kidogo. Hatuwezi kuzalisha chakula bila maji. Ingawa ni muhimu kwamba wakulima watumie maji kidogo kukuza chakula, kupunguza taka ya chakula pia kunaokoa rasilimali zote za maji zilizoingia katika kuzalisha chakula.  Punguza matumizi yako ya maji kwa njia zingine pia kama kukarabati mabomba yanayovuja au kufunga mabomba ya maji wakati unasafisha meno yako! Tunza udongo na maji. Taka zingine za nyumbani zina hatari na hazipaswi kutupwa kwenye pipa la taka za kawaida. Vitu kama betri, rangi, simu za rununu, dawa, kemikali, mbolea, matairi, makasha ya wino, n.k zinaweza kuingia kwenye mchanga na mfumo wa usambazaji wa maji, na kuharibu rasilimali za asili zinazozalisha chakula chetu.  Kula zaidi jamii ya kunde na mboga. Mara moja kwa wiki, jaribu kula chakula cha jamii ya kunde au nafaka za kale kama vile quinoa. Gawia wenzako chakula. Changia na wengine chakula ambacho kingepotea bure. Kwa mfano, apu zinaweza kuwaunganisha majirani wao kwa wao na wafanyabiashara wa ndani ili chakula cha ziada kiweze kugawanywa, na sio kutupwa.

Siku ya Chakula Duniani
15 October 2021, 15:32