Tafuta

Katika maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu, Papa Francisko anakazia umuhimu wa sala ya Kanisa ili kuomba ulinzi, tunza na maongozi ya Roho Mtakatifu. Katika maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu, Papa Francisko anakazia umuhimu wa sala ya Kanisa ili kuomba ulinzi, tunza na maongozi ya Roho Mtakatifu. 

Sinodi ya Maaskofu 2021-2023: Umuhimu wa Sala ya Kanisa

Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa utatumika pia kwa ajili ya kuombea Sinodi ya XVI ya Maaskofu iliyozinduliwa tarehe 10 Oktoba 2021 kwa kukazia: Umuhimu wa Kanisa kukutana na Kristo Mfufuka katika Neno, Sakramenti na Huduma makini kwa watu wa Mungu. Huu ni wakati wa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini, ili hatimaye, waweze kufanya mang’amuzi ya pamoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya kijamii, changamoto ambayo imevaliwa njuga na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, unaoendelea kusoma alama za nyakati, ili ujumbe na nia za Baba Mtakatifu kila mwezi ziweze kuwafikia watu wengi zaidi mahali walipo! Utume wa Sala Kimataifa kwa sasa unaendelea kuchanja mbuga kwa kutumia mitandao ya kijamii, ili kuweza kuwashirikisha waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema katika sala, huku wakiwa wameungana na Baba Mtakatifu Francisko. Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii yanaliwezesha hata Kanisa kuweza kuvuka mipaka ya kijiografia na kuwa karibu zaidi na watu kwa njia ya mitandao ya kijamii. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, ili kuliwezesha Kanisa kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha na utume wake, daima likisoma alama za nyakati na kujibu kilio cha Mama Dunia na kile cha watu wa Mungu mintarafu mwanga na kweli za Kiinjili. Baba Mtakatifu tarehe 27 Machi 2018 aliidhinisha Katiba Mpya ya Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa kama sehemu ya utume wa Kipapa na makao yake makuu yakahamishiwa mjini Vatican.

Kwa miaka mingi, Utume wa Sala umekuwa ukiratibiwa na Wayesuit, kwa kuandaa na kusambaza Nia za Baba Mtakatifu kwa kila mwezi. Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa Padre Frédéric Fornos kuwa Mkurugenzi wa Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa. Utume wa Sala umeenea katika nchi 98 duniani na unashirikiana kwa karibu sana na Chama cha Kitume cha Vijana wa Ekaristi. Baba Mtakatifu Francisko Jumanne tarehe 19 Oktoba 2021 katika uzinduzi wa mtandao wa sala kwa ajili ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume” anasema, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, katika mikutano yao, daima walianza kwa Sala kwa ajili ya Roho Mtakatifu: Uje Roho Mtakatifu “Adsumus, Sancte Spiritus”. Ni katika muktadha huu, Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa utatumika pia kwa ajili ya kuombea Sinodi ya XVI ya Maaskofu iliyozinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 10 Oktoba 2021 kwa kukazia umuhimu wa Kanisa kukutana na Kristo Mfufuka katika Neno, Sakramenti na Huduma makini kwa watu wa Mungu.

Huu ni wakati wa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini, ili hatimaye, waweze kufanya mang’amuzi ya pamoja! haya yanawezekana kutokana na maendeleo makubwa ya utamaduni wa kidigitali, unaoweza kuwafikisha watu wa Mungu kung’amua mambo msingi katika maisha. Vyombo vya mawasiliano ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha ushirika au umoja wa watu wa Mungu, dhana inayopewa kipaumbele cha pekee katika maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, utume wa sala unapyaisha mchakato wa uinjilishaji unaokita mizizi yake katika sakafu ya nyoyo za watu, kwa kujenga mtandao wa mshikamano wa upendo na sala kati ya wakleri, watawa na waamini walei; katika furaha na magumu ya maisha. Utume wa sala ni muhimu katika kukoleza moyo wa Injili ya matumaini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mitandao ya kijamii, iwe ni majukwaa ya kutangaza na kushuhudia: wema, huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mitandao, ilete mvuto wa watu kumwendea Mwenyezi Mungu ili aweze kuwa ni dira na mwongozo wa maisha yao! Sala ni mhimili wa maisha na utume wa Kanisa anasema Baba Mtakatifu, pasi na sala, Kanisa litanyauka na kutoweka kama moto wa mabua!

Umuhimu wa Sala
20 October 2021, 15:11