Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni. Kauli mbiu "Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia" Mdo 4:20. Shukrani kwa Wamisionari kwa ushuhuda na huduma. Maadhimisho ya Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni. Kauli mbiu "Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia" Mdo 4:20. Shukrani kwa Wamisionari kwa ushuhuda na huduma. 

Siku ya Kimisionari Ulimwenguni 2021: Ushuhuda: Imani na Huduma!

Papa amewakumbuka na kuwaombea wamisionari wanaotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Hawa ni mashuhuda wa Injili wanaotumia nguvu zao kwa ajili huduma kwa Mama Kanisa. Wakati mwingine, huduma hii imewagharimu maisha yao. Wamisionari hawa wanaendelea kujisadaka kwa ajili ya mchakato wa uinjilishaji na wala si wongofu wa shuruti! Ushuhuda!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Maadhimisho ya Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni, Dominika tarehe 24 Oktoba 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewakumbuka na kuwaombea wamisionari waliotawanyika sehemu mbalimbali za dunia kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Hawa ni mashuhuda wa Injili wanaotumia nguvu zao kwa ajili huduma kwa Mama Kanisa. Wakati mwingine, huduma hii imewagharimu maisha yao. Wamisionari hawa wanaendelea kujisadaka kwa ajili ya mchakato wa uinjilishaji na wala si wongofu wa shuruti. Wanataka Kristo Yesu, Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, aweze kufahamika, kupendwa na kutumikiwa na wengi. Maadhimisho ya Mwaka huu yananogeshwa na kauli mbiu: “Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.” Mdo 4:20. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wanashiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu! Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza, kushuhudia na kurithisha imani yao kwa watu wanaotembea katika giza na uvuli wa mauti; watu wenye hofu na mashaka, ili waweze kumtambua Kristo Yesu, Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, Nyakati zote ni zake!

Ili kuweza kutekeleza vyema dhamana na wajibu huu, kuna haja kwa Wakristo kujiaminisha kwa Kristo Yesu na kuendelea kujikita katika Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu. Licha ya Wakristo sehemu mbalimbali za dunia, kuendelea kukumbana na dhuluma, nyanyaso na mateso lakini hawana budi kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kama ilivyokuwa hata kwa Wakristo wa Kanisa la Mwanzo. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuishi: wito na utume wao wa kimisionari unaowafanya kustawisha hisia alizo nazo Kristo Yesu; Kuamini pamoja Naye kwamba, jirani zao ni ndugu zao pia. Upendo wa Kristo uamshe tena nyoyo za waamini, ili wote waweze kuwa ni Mitume Wamisionari! Maadhimisho ya Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni, Jumapili tarehe 24 Oktoba 2021 yananogeshwa na kauli mbiu: “Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.” Mdo 4:20. Baba Mtakatifu anagusia kuhusu uzoefu wa Mitume wa Yesu walioguswa na upendo wa Yesu kiasi cha kuacha yote na kuamua kumfuasa Kristo Yesu katika maisha na utume wakeb. Hawa ndio wale wanaosimulia kile ambacho wameona, wamesikia na sasa wanatoa shukrani zao kama wanavyoeleza kwenye Kitabu cha Matendo ya Mitume.

Licha ya patashika nguo kuchanika, lakini Mitume waliweza kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu. Mchakato wa uinjilishaji bado unakabiliwa na changamoto pevu, lakini waamini wanaitwa ili waweze kuwa ni wamisionari wa matumaini, kwa kutambua kwamba, hakuna mtu anayeweza kujiokoa mwenyewe! Kila mwamini anaweza kuchangia katika mchakato wa uinjilishaji kadiri ya hali na mazingira yake. Hiki ni kipindi cha kushirikisha wema na kuendelea kuwa ni watu wa shukrani, ili kuendeleza wito na utume wa kimisionari, kama vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa nyakati hizi! Kwa upande wake Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, katika maadhimisho haya anasema, wamisionari ni watu walioguswa na kuvutwa na huruma na upendo wa Mungu, wakaamua kutoka katika ubinafsi wao tayari kujifunga kibwebwe na kwenda nje ya mipaka ya kijiografia, ili kuambata mambo msingi katika maisha ya mwanadamu. Wito wa kimisionari ni zawadi ya imani kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayopaswa kushirikishwa kwa wengine.

Waamini wanahamasishwa kusali, ili zawadi hii kutoka kwa Roho Mtakatifu, iweze kumwilishwa katika msingi wa huruma na matumaini. Mitume wa Yesu walisikiliza kwa makini mafundisho yake ambayo yamewekwa kwa muhtasari katika Heri za Mlimani na Sala ya Baba Yetu. Walishuhudia jinsi ambavyo Kristo Yesu alijitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini, wagonjwa na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Akawasamehe dhambi, akawaganga na kuwaponya magonjwa yao; akawalisha na kuwanywesha kutoka katika chemchemi ya huruma na upendo wake wa daima. Kwa hakika, umisionari ni kielelezo cha ushuhuda wa furaha na moyo wa shukrani. Hata katika ulimwengu mamboleo, bado kuna changamoto zinazoendelea kuwaandama waamini hasa kutokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, bado kuna nyanyaso, dhuluma na mateso dhidi ya Wakristo sehemu mbalimbali za dunia. Njia za mawasiliano na mitandao ya kijamii imeliwezesha Kanisa kuwafikia watu wengi zaidi, kwa kukutana katika uhalisia wa maisha, ili kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha ya waja wake. Waamini wahamasike kusali kwa ajili shughuli mbalimbali za kimisionari zinazotekelezwa na Mama Kanisa na wawe tayari pia kuchangia rasilimali fedha kama alama ya shukrani. Mchakato wa uinjilishaji unatekelezwa kwa namna ya pekee kabisa katika upendo wa Kiinjili!

Wamisionari Duniani

 

24 October 2021, 15:20