Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko asikitishwa sana na mateso, nyanyaso na dhuluma wanazofanyiwa watu wa Mungu nchini Libya. Baba Mtakatifu Francisko asikitishwa sana na mateso, nyanyaso na dhuluma wanazofanyiwa watu wa Mungu nchini Libya. 

Papa Francisko Asikitishwa na Dhuluma na Mateso Ya Walibya!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hajawasahau, anaendelea kusikiliza kwa makini kilio chao na anawakumbuka katika sala na sadaka yake. Anatambua fika mateso, dhuluma na nyanyaso wanazofanyiwa wanawake na watoto. Papa anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza dhamana, wajibu na ahadi zake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Libya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa kwa mara ya kwanza baada ya miaka 10 kupita imeshuhudia mkutano wa Kimataifa kuhusu utulivu nchini Libya, ukifanyika mjini Tripoli tarehe 21 Oktoba 2021 chini ya uongozi wa Serikali ya mpito nchini Libya. Mkutano umehudhuriwa na wawakilishi kutoka katika nchi 27, sanjari na wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Umoja wa Jumuiya ya Ulaya. Zote hizi ni jitihada za Jumuiya ya Kimataifa kusaidia mchakato wa amani na utulivu katika kipindi hiki cha mpito na hatimaye, uchaguzi mkuu wa Rais ambao umepangwa kufanyika hapo tarehe 24 Desemba 2021. Serikali ya Umoja wa Kitaifa; amani na utulivu; majadiliano ya kisiasa katika ukweli na uwazi ni muhimu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Libya. Uwepo wa majeshi na wapiganaji wa kulipwa nchini Libya ni kikwazo kikuu cha amani na utulivu! Miaka 10 imegota tangu Kanali Muammar Gaddafi (1942-10 Oktoba 211) aliyekuwa Rais wa Libya kupinduliwa madarakani na hatimaye, kuuwawa kikatili. Marekani, Ufaransa na Uingereza zilitoa msaada wa kijeshi katika mapinduzi hayo ambayo yameitumbukiza Libya katika machafuko ya kisiasa kwa kipindi cha miaka kumi.

Libya imekuwa ikikabiliana na changamoto ya machafuko na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, hali ambayo imepelekea wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Kaskazini mwa Afrika, kutafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi Barani Ulaya. Lakini kwa bahati mbaya, wengi wao wamekuwa wakifariki dunia hata kabla ya kuwasili Ulaya kwa kuzama baharini au kupoteza maisha katika mazingira magumu na hatarishi kwenye Jangwa la Sahara. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika, tarehe 24 Oktoba 2021 amependa kuonesha uwepo na ukaribu wake kwa watu wa Mungu nchini Libya. Lakini kwa namna ya pekee kabisa na wakimbizi, wahamiaji, wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa bila kuwasahau wale wote wenye mahitaji msingi. Baba Mtakatifu anasema, kamwe hajawasahau, anaendelea kusikiliza kwa makini kilio chao na anawakumbuka katika sala na sadaka yake. Anatambua fika mateso, dhuluma na nyanyaso wanazofanyiwa wanawake na watoto.

Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inatekeleza dhamana, wajibu na ahadi zake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Libya. Ni wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuratibu wimbi kubwa la wakimbizi kwenye Bahari ya Mediterrania, ambako kuna watu wengi wanaoendelea kupoteza maisha na wengine kurudishwa kwa nguvu nchini Libya. Kuna haja ya kusitisha mchakato wa kuwarejesha wakimbizi na wahamiaji katika nchi ambazo hazina usalama! Kipaumbele cha kwanza kiwe ni kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu, kwa kuhakikisha kwamba, usalama, utu na heshima yao vinalindwa na kuendelezwa. Kuna haja ya kuangalia uwezekano wa kuwapatia wakimbizi na wahamiaji wanaohifadhiwa kwenye Vituo maalum njia mbadala za kuishi, kwa kuboresha mchakato wa watu hawa kupata vibali maalum, vitakavyowawezesha kupata haki zao kama wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu anawataka watu wote kuwajibika kikamilifu, kwa sababu kwa muda wa miaka mingi, wananchi hawa wamekuwa ni wahanga wa mateso, nyanyaso na dhuluma!

Papa Mateso ya Libya

 

25 October 2021, 16:08