Tafuta

Padre Juan Eliàs Medina na wafiadini wenzake 126 wametangazwa kuwa Mwenyeheri kwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa ujasiri kiasi hata cha kumwaga damu yao! Padre Juan Eliàs Medina na wafiadini wenzake 126 wametangazwa kuwa Mwenyeheri kwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa ujasiri kiasi hata cha kumwaga damu yao! 

Padre Juan Elìas Medina na Wenzake 126 Watangazwa Kuwa Wenyeheri!

Mwenyeheri Padre Juan Elías Medina na wenzake 126 waliuwawa kikatili kutokana na chuki dhidi ya imani nchini Hispania wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe. Uaminifu wao uwe ni kielelezo cha nguvu kwa Wakristo wote wanaonyanyaswa na kudhulumiwa sehemu mbalimbali za dunia, ili waweze kupata nguvu ya kutangaza na kushuhudia kwa ujasiri Injili ya Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na watakatifu kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 16 Oktoba 2021 amemtangaza Mtumishi wa Mungu Padre Juan Elías Medina na wenzake 126 waliouwawa kikatili kutokana na chuki dhidi ya imani (In Odium Fidei) huko Cordoba, nchini Hispania wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Hispania kuwa ni Wenyeheri Hili ni kundi kubwa la Mapadre, Watawa, Waseminari na Waamini walei waliouwawa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, wakati wa Vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Hispania kati ya mwaka 1936 – 1939. Hawa ni mashuhuda wa imani, huruma na upendo wa Mungu wanaong’ara sehemu mbalimbali za dunia kwa ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hawa ndio wale waliothubutu kumfuasa Kristo Yesu, kiasi cha kuzama ndani kabisa ya Ubatizo wa Kristo Yesu na hatimaye, kukinywea kikombe chake cha mateso, baraka, neema na shukrani. Hatima ya maisha ya Mkristo ni kuungana na Fumbo la Utatu Mtakatifu na kwamba, kifo dini ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha kuungana na Kristo Yesu katika Fumbo la Msalaba na maisha ya uzima wa milele!

Mababa wa Kanisa wanasema, damu ya mashuhuda wa imani ni mbegu ya Ukristo sehemu mbalimbali za dunia! Mchakato wa kuwatangaza watumishi wa Mungu 127 ulianza kunako tarehe 16 Januari 2010 hadi 15 Septemba 2012 katika ngazi ya kijimbo na tarehe 23 Novemba 2020 nyaraka na ushuhuda zikawasilishwa mjini Vatican. Kanisa likatambua ushuhuda wa imani na kwamba, waliuwawa kikatili kwa ajili ya chuki dhidi ya dini, chuki na uhasama dhidi ya Kristo Yesu na Kanisa lake: (In Odimu Fidei). Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 17 Oktoba 2021 amemkumbuka Mwenyeheri Padre Juan Elías Medina na wenzake 126 waliouwawa kikatili kutokana na chuki dhidi ya imani (In Odium Fidei) huko Cordoba, nchini Hispania wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Hispania. Uaminifu wao uwe ni kielelezo cha nguvu kwa waamini wote na hususan kwa Wakristo wote wanaonyanyaswa na kudhulumiwa sehemu mbalimbali za dunia, ili waweze kupata nguvu ya kutangaza na kushuhudia kwa ujasiri Injili ya Kristo Yesu!

Kwa upande wake, Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na watakatifu wakati wa mahubiri amejielekeza zaidi katika ushuhuda wa imani ya wafiadini hawa, ambao ni chemchemi ya uinjilishaji mpya katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Kwa nguvu ya imani, Mashuhuda hawa wa imani waliweza kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Huu ni mwaliko pia kwa waamini kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika Sakramenti ya Upatanisho, ili Kristo Yesu aweze kuwaokoa kuwandolea na kuwasamehe dhambi zao, ili waweze kuwa na ujasiri wa kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Ni kwa njia hii, tu, Wakristo wataweza kuyashinda malimwengu na hivyo kuwa tayari kutangaza na kushuhudia: mwanga wa Kristo Mfufuka; Imani, Ukweli, Upendo na Msamaha wa kweli dhidi ya chuki na uhasama na kishawishi cha kutaka kulipiza kisasi.

Wafiadini hawa, walipokuwa kufani, walimtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Wakristo watambue kwamba, hata kabla ya kuwachukia, kuwatesa na kuwadhulumu, tayari walimtenda Kristo Yesu, ufunuo wa Uso wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Hata leo hii, kuna maelfu ya Wakristo wanaoendelea kuteswa, kunyanyaswa na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Chuki na uhasama dhidi ya Wakristo ni changamoto endelevu ambayo inapaswa kupokelewa kwa imani, matumaini, ujasiri na uaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake!

Wafia dini wa Cordoba

 

 

18 October 2021, 14:12