Tafuta

Katekesi Kuhusu Waraka wa Mtume Paulo Kwa Wagalatia: Pasaka Kiini Cha Wokovu na Imani

Mt. Paulo Mtume alitangaza Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko kwa wafu. Kiini cha wokovu na imani ni mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Anatoa ufafanuzi huu kwa kuwawekea mbele yao Kristo Mfufuka akisema “Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa? Gal 3:1.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia ni katekesi ya jinsi ambavyo Wakristo wanavyopaswa kuishi kikamilifu imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Utume wa Kanisa ni kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu yaani “Kerygma.” Baba Mtakatifu Francisko katika Mzunguko wa Katekesi ya Waraka wa Mtume Paulo Kwa Wagalatia amekwisha kugusia kuhusu: Ushuhuda wa Mtume Paulo, Fumbo la Maisha ya Kristo Yesu, Wito wa Mtume Paulo kutoka kwa Mungu, jinsi alivyolitesa Kanisa na jinsi ambavyo neema ya Mungu ilivyomwezesha kuwa ni Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Maadui wa Mtume Paulo walijikita zaidi katika mapokeo na Torati na kusahau upya ulioletwa na Injili ya Kristo Yesu! Hakuna Injili mpya isipokuwa ile iliyotangazwa na kushuhudiwa na Mitume wa Yesu! Mtume Paulo anapozungumzia kuhusu Sheria anakazia: Sheria ya Musa pamoja na Amri Kumi za Mungu, msingi wa Agano kati ya Mwenyezi Mungu na Waisraeli. Baba Mtakatifu Francisko amekwisha kutafakari pia kuhusu hatari zinazoweza kuibuka kutokana na utekelezaji wa Torati katika misingi ya uhuru kamili, hali inayoweza kupelekea baadhi ya waamini kuwa wanafiki kwa kuogopa kukutana na ukweli!

Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo kwa kushirikiana na Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani, limechapisha Tamko la Pamoja Kuhusu Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki. Hii ni hatua muhimu sana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Tarehe 3 Januari 2021, Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri kwa pamoja yamefanya kumbukumbu ya miaka 500 tangu Martin Luther alipotengwa rasmi na Kanisa Katoliki. Kwa pamoja, Makanisa haya yanapenda kutangaza nia ya kufanya hija ya upendo na mshikamano kutoka kwenye kinzani kuelekea kwenye umoja kamili wa Wakristo. Tamko la Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki la tarehe 31 Oktoba 1999 lilikuwa na: Utangulizi, Ujumbe wa Biblia juu ya Kuhesabiwa Haki, Mafundisho ya Kuhesabiwa haki kama suala la kiekumene; Ufahamu na maelezo ya pamoja juu ya kuhesabiwa haki. Tamko lilifafanua kuhusu udhaifu wa binadamu, msamaha wa dhambi na kufanyika wenye haki; kuhesabiwa haki kwa njia ya imani na neema. Lilimwangalia aliyehesabiwa haki kama mtu mkosefu; Sheria na Injili; Uhakikisho wa wokovu; Matendo mema ya mtu aliye hesabiwa haki sanjari na umuhimu na lengo la maafikiano yaliyofikiwa. Baba Mtakatifu katika Katekesi yake, mwishoni, ametafakari kuhusu uhuru wa kweli ambao Kristo Yesu amewakirimia waja wake kama zawadi inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, binadamu amekombolewa kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti, mwaliko wa kutambua na kutembea katika ukweli na imani!

Ikumbukwe kwamba, uhuru wa Kikristo ni chachu ya ukombozi ulimwenguni na unapata chimbuko lake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Baba Takatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 27 Oktoba 2021 amejikita kutafakari kuhusu Tunda la Roho kama anavyofafanua Mtume Paulo katika Waraka wake kwa Wagalatia 5: 22-24. “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.” Mtakatifu Paulo Mtume alitangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka ya Kristo yaani: mateso, kifo na ufufuko kwa wafu. Kiini cha wokovu na imani ni mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Anatoa ufafanuzi huu kwa kuwawekea mbele yao Kristo Mfufuka akisema “Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa? Gal 3:1.

Hata leo hii anasema Baba Mtakatifu kuna watu wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani ambao wanatafuta kwa udi na uvumba usalama wa maisha katika dini, kabla ya kumtafuta Mwenyezi Mungu aliye hai na wa kweli. Wanazama zaidi katika kutekeleza ibada, badala ya kumkumbatia na kumwambata Mungu ambaye ni upendo. Ndiyo maana Mtume Paulo anawataka Wagalatia kurejea katika mambo msingi, yaani warejee kwa Mwenyezi Mungu anayewakirimia maisha kupitia kwa Kristo Yesu Msulubiwa. Anashuhudia kwa kusema “Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu.” Gal 6:14. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika mahangaiko ya maisha ya kiroho, matatizo, changamoto pamoja na kuandamwa na mawazo kibao, wajiaminishe chini ya Msalaba wa Kristo Yesu, ili waweze kuanza upya kutoka katika Fumbo la Msalaba. Waamini wajitahidi kukumbatia Msalaba wa Kristo Yesu. Wakati mwingine, waende kumwabudu Kristo Yesu katika Sakramenti kuu ya Ekaristi Takatifu.

Katika Ekaristi, Kristo Yesu amejisadaka na kujimega kwa ajili ya waja wake, Kristo Yesu Mfufuka ni nguvu ya Mungu anayemimina upendo wake nyoyoni mwa waamini. Mtakatifu Paulo awasaidie waamini kukutana na Kristo Yesu wanapojiaminisha chini ya Msalaba, anapowashirikisha maisha yake kwa njia ya Roho Mtakatifu anayebadili nyoyo za waamini ili kutubu na kumwongokea Mungu. Roho Mtakatifu ndiye anayeliongoza Kanisa na waamini wanatakiwa kumtii anapotekeleza kazi yake kadiri anavyotaka! Roho Mtakatifu aliwashukia kwanza Mitume na baadaye kwa watu wengine wote kwa sababu Injili inapaswa kutangazwa na kuenezwa duniani kote na wala hakuna mtu anayepaswa kutengwa! Maisha na utume wa waamini unapyaishwa kwa njia ya Roho Mtakatifu na hivyo kuwasaidia waamini kuendelea kupambana, ili hatimaye kuboresha maisha yao ya Kikristo! Baba Mtakatifu anakaza kusema, mapambano ya maisha ya kiroho ni kati mafundisho makuu yanayotolewa na Mtakatifu Paulo Mtume katika Waraka wake kwa Wagalatia. Anazungumzia mapambano kati ya mwili na roho kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili. Matendo ya mwili yanaonesha maisha ya hapa duniani, yakiwa na upeo mfinyu kwa kufuata mambo ya kidunia na hatimaye, kumfungia malango Roho Mtakatifu, anayewafungulia malango na kuwaonesha yale yaliyo juu, ili wapate kumwelekea Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao.

Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.” Gal 5:19-21. Mtume Paulo anasema, “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho. Tusijisifu bure, tukichokozana na kuhusudiana.” Gal 5: 22-26. Wakristo watambue kwamba, wale wote waliobatizwa katika Kristo wamemvaa Kristo Yesu na wanatakiwa kuenenda katika upya wa maisha. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusoma na kutafakari orodha inayotolewa na Mtakatifu Paulo Mtume, ili kupima mwenendo wao, ili kuona ikiwa kama unakwenda mintarafu Roho Mtakatifu na kwamba, maisha haya yanazaa tunda la Roho, yaani upendo, amani na furaha. Huu ni utambulisho kwamba, Roho Mtakatifu anaishi katika mtu huyu. Mafundisho ya Mtakatifu Paulo ni changamoto hata katika Jumuiya za Kikristo.

Waamini wajifunze kupokea uzuri wa imani kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kwa kujikita katika upendo unaorutubishwa kwa njia ya sala, amani na ushuhuda wa furaha. Kwa wale wanaokazia utekelezaji wa Amri za Mungu na mwelekeo wa kimaadili zaidi, wanaweza kukosa kutambua uzuri wa imani kwa Kristo Yesu na waja wake. Ikumbukwe kwamba, maisha katika Roho Mtakatifu yanamwilishwa katika Sakramenti za Kanisa, chanzo cha toba na wongofu wa ndani. Kwa bahati mbaya anasema Baba Mtakatifu wakleri wamekuwa wakigumisha maisha ya waamini kwa kujikita katika ukiritimba, hali ambayo inawakatisha baadhi ya waamini tamaa na kujikuta wakiacha kupokea Sakramenti za Kanisa. Ikumbukwe kwamba, nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu inajenga na kupyaisha maisha ya waamini! Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha Katekesi yake kuhusu tunda la Roho kwa kuwaambia waamini kwamba, wanao wajibu mkubwa wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyefufuka kwa wafu ndiye anayewavuvia Roho wa upendo. Kimsingi, upendo una nguvu inayoweza kuwasaidia watu kubadili nyoyo zao!

Fumbo la Wokovu

 

27 October 2021, 14:44

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >