Tafuta

Gazeti la L' Osservatore Romano kwa lugha ya Kijerumani tarehe 8 Oktoba 2021 limeadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Gazeti la L' Osservatore Romano kwa lugha ya Kijerumani tarehe 8 Oktoba 2021 limeadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.  

Jubilei ya Miaka 50 ya Gazeti la L'Osservatore Romano Kijerumani

Katika kipindi cha Miaka 50 Gazeti la L’Osservatore Romano kwa lugha ya Kijerumani limejikita katika mchakato wa kuwajuza wasomaji wake kwa mtazamo wa maisha na utume wa Kanisa kutoka mjini Vatican na ulimwengu katika ujumla wake. Yote haya yanapania kuwawezesha wasomaji wa Gazeti la L’Osservatore Romano kulifahamu zaidi Kanisa la kiulimwengu na Vatican!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Gazeti la L’Osservatore Romano linalomilikiwa na Vatican mwaka 2021 linasherehekea Miaka 160 tangu kuanzishwa kwake na Miaka 50 tangu Gazeti hili lianze kuchapishwa kwa lugha ya Kijerumani hapo tarehe 8 Oktoba 1971. Katika kipindi cha miaka yote mambo makuu mawili yamepewa kipaumbele cha kwanza: Uaminifu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na Ubunifu katika kutangaza na kushuhudia maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Vatican. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza waandishi wa habari wa Gazeti la L’Osservatore Romano linalochapishwa mara moja kwa juma katika lugha ya Kijerumani. Anapenda kuwasindikiza wadau wote kwa sala na sadaka yake. Katika kipindi cha Miaka 50 Gazeti la L’Osservatore Romano kwa lugha ya Kijerumani limejikita katika mchakato wa kuwajuza wasomaji wake kwa mtazamo wa maisha na utume wa Kanisa kutoka mjini Vatican na ulimwengu katika ujumla wake. Ni Gazeti linalohabarisha matukio makuu na nyaraka mbalimbali zinazotolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro sanjari na kutoa mchango mkubwa unaosheheni utajiri wa kitamaduni. Yote haya yanapania kuwawezesha wasomaji wa Gazeti la L’Osservatore Romano kulifahamu zaidi Kanisa la Kiulimwengu. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko ametoa baraka zake za kitume kwa wale wote wanaochangia kwa hali na mali katika kufanikisha utume huu pamoja na wasomaji wake wote.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Nikola Eterović, Balozi wa Vatican nchini Ujerumani anasema, Gazeti hili lilianzishwa wakati ambapo utawala wa Kifashisti pamoja na machafuko makubwa ya kisiasa kwa ajili ya kudai demokrasia yalikuwa yamepamba moto. Ni Gazeti ambalo limeshuhudia maisha na utume wa Papa Paulo VI, Papa Yohane Paulo I aliyeliongoza Kanisa kwa muda wa siku thelathini na tatu tu; Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na sasa Baba Mtakatifu Francisko ndiye aliyeshikilia usukani. Ni Gazeti ambalo limewasindikiza viongozi wa Kanisa katika maisha na utume wao kwa Kanisa la Kiulimwengu na Vatican katika ujumla wake. Nyaraka zote hizi zimekuwa zikichapishwa na kwa hakika wasomaji wengi wa Gazeti hili watakubaliana kimsingi kwamba, nyaraka hizi ni amana na utajiri mkubwa kutoka kwa Kanisa bila kusahau mchango wa wa wataalam katika fani mbalimbali za maisha. Askofu mkuu Nikola Eterović, anaendelea kuelezea kwa kusema, Gazeti la L’Osservatore Romano kwa lugha ya Kijerumani, limekuwa ni msaada mkubwa kwa wasomaji, kwa kuwashirikisha hija za kitume zinazofanywa na Baba Mtakatifu sehemu mbalimbali za dunia.

Habari hizi zimesheheni pia amana na utajiri wa tafakari, hotuba na sala mbalimbali zinazotolewa na wakuu wa Kanisa kutoka katika Madhabahu ya Bikira Maria. Maadhimisho ya Siku za Vijana Kimataifa na matukio mbalimbali ya maisha na utume wa Kanisa yamekuwa yakizipamba nyaraka zinazochapishwa na Gazeti hili. Kwa kupitia Ubalozi wa Vatican nchini Ujerumani, Gazeti la L’Osservatore Romano linaweza kuwafikia wanadiplomasia kwa lugha mbalimbali. Ni Gazeti linalosomwa na waamini wa dini mbalimbali kama sehemu ya mchakato wa kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene ili kujenga mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Katika kipindi cha Miaka 50 iliyopita, kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika tasnia ya mawasiliano ya jamii. Katika muktadha huu, hata Gazeti la L’Osservatore Romano limeguswa kutokana na mabadiliko ya tabia na wasomaji wake. Leo hii mwelekeo uliopo ni wasomaji kutaka kupata habari motomoto hata kama hazijafanyiwa utafiti wa kutosha kwa kuzingatia sheria, kanuni, weledi na taaluma ya uandishi wa habari. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, habari inaweka mahali pake, ikiwa imefanyiwa upembuzi yakinifu na wenye kina!

Jubilei ni kipindi cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Askofu mkuu Nikola Eterović, Balozi wa Vatican nchini Ujerumani anapenda kuchukua fursa hii, kuwashukuru na kuwapongeza wale wote waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwenye Gazeti la L’Osservatore Romano. Mwenyezi Mungu awajalie maisha na uzima wa milele wale wote waliotangulia mbele ya haki! Kwa Mhariri mkuu na waandishi wote wa habari wanaochakarika kwa wakati, huu, shukrani za dhati kabisa ziwaendee wote. Anawaombea neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ufanisi wa Gazeti la L’Osservatore Romano! Hakuna sababu ya kuwa na wasi wasi kwani hakuna mambo yanayoweza kuwashinda! Inasomeka vizuri zaidi kwa lugha la Kilatini: “Unicuique suum, Non praevalebunt.”

Jubilei Miaka 50
09 October 2021, 16:44