Patriaki Bartholomeo wa kwanza katika tafakari yake kwenye kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa amekazia kuhusu umuhimu wa Ekaristi katika huduma na utunzaji bora wa kazi ya uumbaji. Patriaki Bartholomeo wa kwanza katika tafakari yake kwenye kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa amekazia kuhusu umuhimu wa Ekaristi katika huduma na utunzaji bora wa kazi ya uumbaji. 

Kongamano la 52 La Ekaristi Kimataifa: Majadiliano ya Kiekumene

Patriaki Bartolomeo wa kwanza wakati wa maadhimisho ya kongamano hili amekazia zaidi kuhusu umuhimu wa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu kama kielelezo cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu, ili kulinda kazi ya uumbaji kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Huduma makini kwa watu wa Mungu ni zawadi inayopata chapa yake katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC) kuanzia tarehe 5-12 Septemba 2021, huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria yameongozwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Kongamano hili pamoja na mambo mengine lilipania kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene, kidini na kitamaduni ili kunogesha na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu nchini Hungaria. Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol ameshiriki kikamilifu kwa kutoa mada na Ibada ya kufunga Kongamano hili, iliyoadhimishwa na Baba Mtakatifu Francisko. Wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Mashahidi wa Hungaria, Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol.

Kwa upande wake, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol wakati wa maadhimisho ya kongamano hili amekazia zaidi kuhusu umuhimu wa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu “εὐχαριστία” kama kielelezo cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu, ili kulinda na kudumisha kazi ya uumbaji kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Huduma makini kwa watu wa Mungu ni zawadi inayopata chapa yake katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Hili pia ni fumbo la umoja “κοινωνία, koinonía” kwa ajili ya maisha ya binadamu na viumbe wengine wote. Uzoefu na mang’amuzi ya Kiekaristi yasaidie kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari, tayari kuinjilisha kwa kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, kama ushuhuda wa imani tendaji. Wakristo wanahimizwa kuwa ni chumvi na nuru na Kristo Yesu anakaza kusema, “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.” Mt 5:14-16.

Sakramenti za Kanisa na Sanaa Takatifu ni sehemu ya Kazi ya Uumbaji. Lakini katika maadhimisho la Liturujia Takatifu ya Kanisa, waamini bila kujali asili, tofauti, nyadhifa na uwezo wao wa kiuchumi wanakutana ili kuadhimisha Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, tukio la Kikanisa, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya wokovu unaobubujika kutoka katika Kanisa. Fumbo la Ekaristi Takatifu liwapatie waamini nguvu na ujasiri wa kusimama kidete kulinda, kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Liwe ni chemchemi ya ujenzi wa umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Waamini wawe ni mashuhuda wa ikolojia na mshikamano unaowawajibisha kikamilifu kutumia vyema utajiri na rasilimali za dunia hii kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi! Kristo Yesu anasema, “Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.” Ufu 22:13. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa ni mashuhuda amini wa Kristo Yesu na Kanisa lake. Huu ni mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano wa Kanisa la Kristo ambalo limejeruhiwa kutokana na madonda ya utengano na kinzani. Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol anasali na kumwomba Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kuwakirimia Wakristo wote nguvu ya kuendelea kujikita katika majadiliano ya kiekumene, ili siku moja umoja wa Wakristo uweze kuonekana na huo utakuwa ni mwanzo wa Makanisa yote kuadhimisha kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu.  

Papa Uekumene
12 September 2021, 17:15