Tafuta

Kongamano la 52 La Ekaristi Kimataifa: Msalaba Nguzo ya Wokovu!

Papa Francisko anatumaini kuwa Msalaba utakuwa ni chemchemi ya matumaini mapya kwa sasa na kwa siku za usoni. Msalaba uwe ni chachu ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Msalaba uwe ni nguvu ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayobubujika upendo wa Kristo usiokuwa na mipaka kwa waja wake! Msalaba Nguzo thabiti ya imani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Misa Takatifu kufunga Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC), yaliyonogeshwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7, huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria amesali Sala ya Malaika wa Bwana. Neno Ekaristi linapata asili yake kutoka kwenye lugha ya Kigiriki “εὐχαριστία” maana yake “Kushukuru”. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwashukuru wote waliowezesha kufanikisha maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa sanjari na Hija yake ya Kitume nchini Hungaria; tukio ambalo pia limebeba uzito wa pekee katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini kwa uwepo na ushiriki wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol. Msalaba wa Kristo Yesu Ni Nguzo ya Wokovu wa Binadamu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Msalaba wa Kristo Yesu utakuwa ni chemchemi ya matumaini mapya kwa watu wa Mungu ndani nje ya Hungaria kwa sasa na kwa siku za usoni. Msalaba wa Kristo uwe ni chachu ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Msalaba wa Utume ndicho kilichokuwa kielelezo cha Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa.

Msalaba wa Kristo uwe ni nguvu ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayobubujika upendo wa Kristo usiokuwa na mipaka kwa watu wote. Upendo huu ukate na kuzima kiu ya watu wote wasiopendwa duniani. Baba Mtakatifu amewataja Wenyeheri wapya Kardinali Stefan Wyszyński na Sr. Elizabeth Czacka, Waasisi wa Shirika la Watawa Watumishi wa Msalaba waliotangazwa kwenye Ibada ya Misa takatifu iliyoongozwa na Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Wenyeheri na Watakatifu, Jimbo kuu la Varsavia, nchini Poland, Jumapili tarehe 12 Septemba 2021. Kardinali Stefan Wyszyński alikuwa ni mkuu wa Kanisa Katoliki nchini Poland. Alikamatwa na kutupwa gerezani. Daima katika maisha na utume wake alishuhudia ujasiri wa kuwa ni Mchungaji mwema kadiri ya Moyo Mtakatifu wa Yesu; akasimama kidete kutangaza na kulinda uhuru, utu na heshima ya binadamu. Kwa upande wake, Sr. Elizabeth Czacka, ambaye katika ujana wake aliugua na hatimaye akawa kipofu, alisadaka maisha yake yote kwa ajili ya huduma kwa vipofu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwa maombezi ya wenyeheri hawa wapya, waamini wataweza kugeuza giza kwa mwanga wa upendo! Mwishoni ametoa baraka zake kwa watu wote wa Mungu na hatimaye kusali pamoja Sala ya Malaika wa Bwana.

Kabla ya Ibada ya Misa Takatifu Kardinali Péter Erdő, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kunogesha Maadhimisho haya ambayo yamechukua mkondo wa kiekumene na majadiliano ya kidini, kuzunguka meza ya Bwana! “Statio Orbis” ni kielelezo cha umoja na mshikamano wa Kanisa. Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Kristo Yesu ni chemchemi ya maisha, furaha na nguvu ya wale wote wanaotaka kumtangaza na kumshuhudia kwa njia ya Injili ya upendo na faraja kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Budapest ni kiini cha Hungaria na daraja linalounganisha Bara la Ulaya na nchi jirani. Miaka 15 iliyopita Hungaria imetia saini makubaliano ya upatanisho na urafiki kati ya Baraza la Maaskofu Katoliki Hungaria na Slovakia, ili kujenga na kudumisha uzoefu na mang’amuzi ya pamoja ya ujenzi wa umoja, ushirikiano na udugu wa kibinadamu.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Piero Marini, Rais wa Tume ya Kipapa ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa amesema, miaka 140 imegota tangu kuanzishwa kwa Maadhimisho ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa, ili kuchota na kupyaisha imani, umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Maadhimisho haya ni sehemu ya mbinu mkakati wa uinjilishaji unaoliwezesha Kanisa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, ili watu wote waweze kuona mwanga angavu wa Injili. Rej. EG 20. Ekaristi Takatifu inawawezesha waamini kueneza Ufalme wa Mungu kati ya watu wa Mataifa, changamoto na mwaliko kwa waamini kumtolea ushuhuda wenye mvuto Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni mwaliko wa kufanya toba na wongofu wa ndani, ili kuanza kujikita katika Injili ya huruma na mapendo. Waamini wajenge utamaduni wa kushiriki adhimisho la Dominika, yaani Siku ya Bwana, ili kuchota utajiri wa Neno la Mungu na Kushiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu, nguvu ya ushuhuda wa imani, ili kuganga na kuponya majeraha mbalimbali duniani!

Papa Malaika wa Bwana
12 September 2021, 14:57

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >