Papa Francisko awataka wakristo kupyaisha maisha yao kwa kufuata hatua kuu tatu: kumtangaza, kufanya mang'amuzi na Yesu na kufuata nyayo zake! Papa Francisko awataka wakristo kupyaisha maisha yao kwa kufuata hatua kuu tatu: kumtangaza, kufanya mang'amuzi na Yesu na kufuata nyayo zake! 

Kongamano la 52 La Ekaristi Kimataifa: Hatua 3 Za Kupyaisha Ukristo!

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa wafuasi wa Kristo Yesu kupyaisha maisha yao kwa kufuata hatua kuu tatu: Kumtangaza Kristo Yesu; Kufanya mang’amuzi ya kina pamoja na kutembea nyuma yake kwa kumtambua Kristo wa kweli, ili hatimaye waweze kukiri kwa imani thabiti kwamba, “Wewe ndiwe Kristo”, yaani Imani kwa Mungu kweli na Mtu kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya Kitume nchini Hungaria, Jumapili tarehe 12 Septemba 2021 baada ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, Baraza la Maaskofu Katoliki Hungaria, viongozi wa Baraza la Makanisa pamoja na viongozi wa Jumuiya za Kiyahudi nchini Hungaria, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ili kufunga rasmi Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC), Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria.  Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa wafuasi wa Kristo Yesu kupyaisha maisha yao kwa kufuata hatua kuu tatu: Kumtangaza Kristo Yesu; Kufanya mang’amuzi ya kina pamoja naye na kutembea nyuma yake kwa kumtambua Kristo wa kweli, ili hatimaye waweze kukiri kwa imani thabiti kwamba, “Wewe ndiwe Kristo”. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wote waliojisadaka usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba, maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa yanafanikiwa.

Kwa namna ya pekee kabisa wafuasi wa Kristo Yesu wanapaswa kupyaisha maisha na utume wao wanapokiri imani yao kwa Kristo Yesu, ikiwa imekamilika barabara yaani kwa kutambua Ubinadamu na Umungu wake unaofumbatwa katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko kwa wafu. Huu ni utambulisho pia unaojionesha kwenye Fumbo la Ekaristi Takatifu na kwamba, utume wa Kristo Yesu unakamilika kwa Fumbo la Pasaka. Na hii ndiyo katekesi iliyofuata baada ya kiri ya imani ya Mtakatifu Petro, Mtume! “Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka.” Mk 8:31. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, ni kawaida hata leo hii, wafuasi wa Kristo Yesu wangependa kumwona Masiha mwenye nguvu, lakini Mwenyezi Mungu amewapatia Kristo Yesu, Mtumishi mwaminifu wa Mungu aliyeteseka na anaendelea kukaa pamoja na waja wake katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Hii ni Sakramenti inayomwonesha Mwenyezi Mungu kuwa ni Mkate wa uzima unaomegwa; Upendo wa Mungu ulioteseka. Kimsingi, Ekaristi Takatifu ni mkate uliomegwa, watu wakagawiwa na kuula. Ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, Kristo Yesu alijinyenyekesha na kuwa ni mtumishi mwaminifu, akayamimina maisha yake kwa kukubali kifo cha Msalaba! Huu ni ukweli ambao waamini wanapaswa kuutafakari daima!

Wakristo wanapaswa kufanya mang’amuzi wakiwa wameambatana na Kristo Yesu, vinginevyo watajikuta “wakimkemea Yesu” kama alivyofanya Mtume Petro na kwamba, hakuna binadamu anayeweza kukubali Fumbo la Msalaba kwa urahisi katika maisha yake. Msalaba unapotokea, mateso na magumu yanayopomsonga mwanadamu, hapo anacharuka na kugeuka kuwa “Mbogo”. Mtume Petro baada ya kumkiri Yesu kuwa ni Kristo, anakwaza na maneno ya Yesu kwamba, inampasa kuteswa, kufa na hatimaye, siku ya tatu kufufuka kwa wafu! Hata kama Msalaba bado kwa watu wengi hauna mvuto wala mashiko, lakini ndiyo dawa inayomganga na kumponya mwamini kutoka katika undani wa maisha yake, ikiwa kama atathubutu kufikiri kadiri ya mapenzi ya Mungu na wala si kwa vionjo vya kibinadamu. Mwenyezi Mungu anafikiri na kutenda katika unyenyekevu wa upendo; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kiasi hata cha kuyamimina maisha yake! Lakini mwanadamu fikira zake zimegubikwa na ubinafsi, anatafuta heshima, mafanikio ya chapuchapu na kutaka kujimwambafai mbele ya watu wengine!

Ni katika muktadha huu, Kristo Yesu alimwambia Petro arejee nyuma yake na kuanza kujifunza tena, ili aweze kumtambua Mungu wa kweli aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Huyu si Mungu anayetaka kuonesha nguvu zake, bali anatoa mwanya kwa wafuasi wake kutakasa mawazo na dini yao mbele ya Fumbo la Msalaba. Kwa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, waamini wanapata nafasi ya kuutafakari unyenyekevu wa Mungu katika maumbo ya Mkate na Divai. Huu ni Mkate unaoganga na kuponya; ni sadaka ya kweli inayomwokoa mwanadamu kutoka katika ugumu wa moyo sanjari na tabia ya kutaka kujilinda daima. Hii ni changamoto ya kumfuasa Kristo Yesu na kutembea kufuata nyayo zake! Lakini Kristo Yesu “Akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro, akasema, Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.” Mk 8:33. Yesu anatambua upendo mkuu alio nao kwa waja wake, lakini anataka kuwafundisha kujikita katika Injili ya upendo unaomwilishwa katika huduma, huku Kristo Yesu akipewa kipaumbele cha kwanza. Mtume Petro alipata taabu sana kumweka Kristo Yesu kuwa kipaumbele cha maisha yake, mara kadhaa akateleza na kuanguka, lakini kwa neema ya Mungu akasimama na kupiga moyo konde na hivyo kusonga mbele. Huu ni mchakato wa kutoka katika kusamehe na kuanza kusamehewa, ili kutambua kwa hakika Uso wa huruma ya Mungu; tayari pia kuwashirikisha wengine upendo huu unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu.

Kurejea nyuma ya Kristo Yesu ni kutambua upendo wake wa dhati na hivyo kuanza mchakato wa kufuata nyayo zake. Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha umoja wa Kanisa. Waamini wanapokutana na Kristo Yesu katika Ekaristi Takatifu wampatie nafasi ya kuwaletea mageuzi makubwa katika maisha yao kama ilivyokuwa kwa watakatifu kama Stefano wa Hungaria na Elizabeth wa Hungaria. Hawa ni watakatifu waliogundua upya wa Fumbo la Msalaba katika maisha ya Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kristo Yesu ni mkate unaomegwa kwa ajili ya uhai wa walimwengu. Kwa jinsi hii anasema Baba Mtakatifu, Wakristo wataweza kuwa ni chemchemi ya furaha kwa jirani zao! Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha mahubiri yake kwa kusema, kwamba, Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa yanahitimisha sehemu ya kwanza ya safari ya maisha ya kiroho, lakini huo ni mwanzo wa mchakato wa kukaribisha neema ya kutembea na kuambatana na Kristo Yesu “Kairos of grace” sanjari na kuendelea kuchangamotishwa na Kristo Yesu anayetaka kufahamu, wewe una mfahamu Kristo Yesu kuwa ni nani?

Papa Budapest
12 September 2021, 15:36