Tafuta

Katekesi Waraka wa Mtume Paulo Kwa Wagalatia: Kuhesabiwa Haki

Kuhesabiwa haki ni kupokea haki ya Mungu kwa imani katika Yesu, yaani kupokea wema wa mapendo ya Mungu. Pamoja na kuhesabiwa haki, imani, matumaini na mapendo humiminwa nyoyoni mwa waamini na hivyo kujaliwa kuwa mtii kwa Mungu. Kuanzisha ushirikiano kati ya neema ya Mungu na uhuru wa mtu binafsi. Hii ni kazi ya Utatu Mtakatifu na utakaso wa mtu mzima.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Mzunguko wa Katekesi ya Waraka wa Mtume Paulo Kwa Wagalatia amekwisha kukazia kuhusu: Ushuhuda wa Mtume Paulo, Fumbo la Maisha ya Kristo Yesu, Wito wa Mtume Paulo kutoka kwa Mungu, jinsi alivyolitesa Kanisa na jinsi ambavyo neema ya Mungu ilivyomwezesha kuwa ni Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia ni katekesi ya jinsi ambavyo Wakristo wanavyopaswa kuishi kikamilifu imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Utume wa Kanisa ni kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu yaani “Kerygma”. Maadui wa Mtume Paulo walijikita zaidi katika mapokeo na Torati na kusahau upya ulioletwa na Injili ya Kristo Yesu! Hakuna Injili mpya isipokuwa ile iliyotangazwa na kushuhudiwa na Mitume wa Yesu! Mtume Paulo anapozungumzia kuhusu Sheria anagusia: Sheria ya Musa pamoja na Amri Kumi za Mungu, msingi wa Agano kati ya Mwenyezi Mungu na Waisraeli. Baba Mtakatifu Francisko amechambua pia kuhusu hatari zinazoweza kuibuka kutokana na utekelezaji wa Torati katika misingi ya uhuru kamili, hali inayoweza kupelekea baadhi ya waamini kuwa wanafiki kwa kuogopa ukweli.

Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo kwa kushirikiana na Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani, limechapisha Tamko la Pamoja Kuhusu Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki. Hii ni hatua muhimu sana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Tarehe 3 Januari 2021, Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri kwa pamoja yamefanya kumbukumbu ya miaka 500 tangu Martin Luther alipotengwa rasmi na Kanisa Katoliki. Kwa pamoja, Makanisa haya yanapenda kutangaza nia ya kufanya hija ya upendo na mshikamano kutoka kwenye kinzani kuelekea kwenye umoja kamili wa Wakristo. Tamko la Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki la tarehe 31 Oktoba 1999 lilikuwa na: Utangulizi, Ujumbe wa Biblia juu ya Kuhesabiwa Haki, Mafundisho ya Kuhesabiwa haki kama suala la kiekumene; Ufahamu na maelezo ya pamoja juu ya kuhesabiwa haki. Tamko lilifafanua kuhusu udhaifu wa binadamu, msamaha wa dhambi na kufanyika wenye haki; kuhesabiwa haki kwa njia ya imani na neema. Lilimwangalia aliyehesabiwa haki kama mtu mkosefu; Sheria na Injili; Uhakikisho wa wokovu; Matendo mema ya mtu aliye hesabiwa haki sanjari na umuhimu na lengo la maafikiano yaliyofikiwa.

Radio Vatican inakuwekea yote haya ili uweze kufahamu vyema Mafundisho ya Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 29 Septemba 2021 ametafakari kuhusu: Maisha ya Imani:  Kuhesabiwa haki kunakopata chimbuko lake kutoka katika imani. Kuna haja ya kuwa makini zaidi katika kutafsiri Nyaraka za Mtakatifu Paulo. Katekesi hii imenogeshwa na Neno la Mungu kutoka katika Waraka Mtume Paulo kwa Wagalatia 2: 19-20 akisema “Nimesulubiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu. Siibatili neema ya Mungu; maana, ikiwa haki hupatikana kwa njia ya sheria, basi Kristo alikufa bure.”. Baba Mtakatifu kwa unyenyekevu mkubwa anakiri kuhusu ugumu wa tafsiri ya “Kuhesabiwa Haki” lakini anasema, hii ni tema muhimu sana!

Kwa ufupi kabisa maana ya kuhesabiwa haki ni kupokea haki ya Mungu kwa imani katika Kristo Yesu, yaani kupokea wema wa mapendo ya Mungu. Pamoja na kuhesabiwa haki, imani, matumaini na mapendo humiminwa nyoyoni mwa waamini na hivyo kujaliwa kuwa na utii kwa Mwenyezi Mungu. Kuhesabiwa haki huanzisha ushirikiano kati ya neema ya Mungu na uhuru wa mtu binafsi. Hii ni kazi ya Mungu iliyo bora sana inayodhihirishwa katika Kristo Yesu na kutolewa na Roho Mtakatifu. Kuhesabiwa haki ni pamoja na utakaso wa mtu mzima. Rej. KKK 1987-1995. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko, Kristo Yesu ameshinda dhambi na mauti na kumkirimia mwanadamu msamaha wa dhambi, upatanisho na Mungu pamoja na wokovu. Mtakatifu Paulo anasema, kuhesabiwa haki ni matunda ya neema. Mtume Paulo anawasimulia jinsi alivyotubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu baada ya kukutana mubashara na Kristo Yesu Mfufuka alipokuwa njiani kuelekea Dameski. Mtume Paulo alikuwa ni mtu wa kujiamini na mwenye kiburi, mchamungu na mwenye ari katika dini yake na alifikiri kwamba, utekelezaji wa Torati ilikuwa ni sehemu ya kuhesabiwa haki. Lakini baada ya kukutana na Kristo Yesu Mfufuka, akatambua kwamba, ni kwa njia ya imani kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka, maisha yake yamepata mwelekeo mpya kwa kugundua ukweli uliokuwa umefichika, kwani ni kwa njia ya neema kutoka kwa Kristo Yesu, watu wanaweza kuhesabiwa haki. Yale mambo yote yaliyokuwa faida kwake, aliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo Yesu. Rej. Flp. 3:7.

Mwanadamu amekombolewa kwa neema ya Mungu na wala si kwa nguvu na juhudi zake binafsi. Maisha ya mwamini tangu anapozaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu katika Sakramenti ya Ubatizo hadi mauti yanapomfika, yanafumbatwa katika Fumbo la Pasaka ya Kristo Yesu anayewakirimia neema na wokovu, wale wote wanaomwamini! Torati ya Musa ni zawadi kubwa ya Mungu kwa Waisraeli, na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuchuchumilia na kuambata Amri za Mungu ambazo ni dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu. Torati ni muhtasari wa upendo kwa Mungu na jirani. Mtu anahesabiwa haki kwa njia ya neema inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na hivyo kumwilishwa katika matendo, kama kielelezo cha imani tendaji. Mwenyezi Mungu anaendelea kuwa karibu na mwanadamu kwa njia ya: Ukaribu wake, huruma na upendo, kielelezo makini cha mtu kuhesabiwa haki. Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ni chemchemi ya ukombozi wa mwanadamu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwachia nafasi Kristo Yesu katika maisha yao, ili neema yake iweze kutenda kazi ndani mwao. Jicho la imani linawawezesha waamini kuona huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka, changamoto ni kwa waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Watu wanahesabiwa haki kutoka kwa neema ya Kristo Yesu.

Kuhesabiwa Haki Ok

 

29 September 2021, 16:06

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >