Papa Francisko katika hija yake ya kitume nchini Slovakia, 13 Septemba 2021 amekutana na kuzungumza na viongozi wa serikali, wanasiasa, wanadiplomasia na wawakilishi nchini Slovakia. Papa Francisko katika hija yake ya kitume nchini Slovakia, 13 Septemba 2021 amekutana na kuzungumza na viongozi wa serikali, wanasiasa, wanadiplomasia na wawakilishi nchini Slovakia. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Slovakia: Viongozi wa Serikali

Baba Mtakatifu amegusia kuhusu amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu; uinjilishaji wa imani unaosimikwa katika umoja wa Wakristo, chumvi na mkate kama alama za ukarimu wa watu wa Mungu kutoka Slovakia na changamoto ya UVIKO-19. Baba Mtakatifu amesema, historia ya nchi hii inaonesha kuwa ni chemchemi ya amani na udugu wa kibinadamu Barani Ulaya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 13 Septemba 2021, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Slovakia. Amekaribishwa na Rais Zuzana Čaputová na hatimaye, kukaguwa gwaride la heshima, lililoandaliwa kwa ajili yake. Amefanya mazungumzo ya faragha na Rais wa Slovakia na baadaye akakutana na kuwahutubia viongozi wa Serikali, Vyama vya kijamii, Mabalozi na Wawakilishi mbalimbali walioko nchini Slovakia. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amegusia kuhusu amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu; uinjilishaji wa imani unaosimikwa katika umoja wa Wakristo, chumvi na mkate kama alama za ukarimu wa watu wa Mungu kutoka Slovakia na changamoto ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru watu wa Mungu nchini Slovakia kwa ukarimu wao na kwamba, historia ya nchi hii inaonesha kuwa ni chemchemi ya amani na udugu wa kibinadamu Barani Ulaya. Mpango Mkakati wa Ufufuaji wa Uchumi Barani Ulaya “European Union Economic Recovery Plan”, huu usaidie mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu na hivyo kuondokana na hali ya kutovumiliana, uchu wa mali na kutaka kupata faida kubwa, hali inayoweza kuleta mpasuko mkubwa, badala ya kuwaunganisha watu.

Mpango Mkakati wa Kufufua Uchumi Barani Ulaya hauna budi kusimikwa katika msingi wa amani na utulivu ili kuchochea maendeleo fungamani ya binadamu. Imani katika asili yake, isaidie kukoleza udugu wa kibinadamu, kwa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa kati ya wananchi wa Slovakia kama ilivyokuwa kwa Watakatifu Cyril na Method katika utume wao wa uinjilishaji, kwa kutambua yale mambo msingi yanayowaunganisha wote kwa pamoja. Imani iwasaidie watu wa Mungu kujikita katika ukweli na uwazi na kwamba, viongozi mbalimbali wanaweza kuwa ni alama ya umoja! Watu wa Mungu nchini Slovakia ni wakarimu sana kwa wageni na kadiri ya mila na desturi zao njema, mgeni anapowasili anapewa mkate na chumvi. Mkate ni muhimu kwa ajili ya kulinda maisha, lakini pia ni kielelezo cha ushirikiano. Utajiri wa kweli unafumbatwa katika ule uwezo wa kugawana kile kilichopo na wala si muujiza wa kuongeza mikate. Mkate uliomegwa ni kielelezo cha udhaifu wa binadamu, hali inayo wadai watu wa Mungu kushirikiana, kushikamana na kuhudumiana. Na wala kusiwepo kitendo cha watu kubaguliwa, wala kuonekana kuwa ni mzigo mzito wa kutua.

Kila mtu apewe heshima yake, asaidiwe na kulindwa. Mkate uliomegwa unaonesha umuhimu wa kutoa haki, ili kila mtu aweze kutekeleza ndoto yake katika maisha. Hii ni changamoto ya kukuza na kudumisha umoja na mshimamano wa Kitaifa. Ni mwaliko wa kupambana kufa na kupona na kashfa ya rushwa na ubadhilifu wa mali ya umma sanjari na kuhakikisha kwamba, utawala wa sheria unadumishwa. Watu wapewe fursa za ajira, ili kusiwepo na ulazima wa watu kuikimbia familia na nchi yao kwa kutafuta, usalama, hifadhi na maisha bora ughaibuni. Chumvi ni alama ambayo Kristo Yesu aliitumia kuwafundishia wafuasi wake, changamoto na mwaliko wa kunogesha ladha kwenye mshikamano na udugu wa kibinadamu. Isaidie kukoleza moyo wa kujitoa sadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani. Vijana wahamasishwe zaidi, ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuiunda na kuijenga jamii yao kwa ndoto na kipaji chao cha ubunifu. Vijana wahusishwe kikamilifu katika ujenzi wa nchi yao, vinginevyo, watageuzwa kuwa “mateja” na walaji wa kupindukia.Baba Mtakatifu anakaza kusema, Barani Ulaya, kuna watu wameelemewa pamoja na kuchanganyikiwa na maisha, kiasi cha kupoteza matumaini. Shida kubwa ni watu kushindwa kuwahudumia jirani zao. Upendo kwa jirani unaongeza ladha ya maisha.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, utajiri wa mila na desturi njema za watu wa Mungu nchini Slovakia, hazitaharibiwa na ulaji wa kupindukia sanjari na ukoloni wa kitikadi; utakaovuruga uhuru na kuukosesha maana. Leo hii dhana ya maendeleo imegeuzwa kuwa ni mchakato wa kutafuta faida kubwa na haki kwa wachache. Imani haijasaidia kupambana na utamaduni wa vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kwa kujikita katika Injili ya huduma ya upendo. Tunu msingi za Injili zisaidie kuchochea ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, mwaliko unaobubukila kutoka kwa watakatifu wanaoheshimiwa nchini Slovakia. Hawa ni watu walioipamba jamii kwa kuwa na mwono wa Heri za Mlimani, kwa kuendelea kuwa wazi katika mchakato wa upyaisho wa maisha. Watakatifu hawa walipambana na changamoto nyingi za maisha; wakateswa, wakanyanyaswa na kudhulumiwa, lakini ndani mwao waliendelea kubaki huru, wakiwa na ujasiri kiasi cha kupambana na ukosefu wa haki. Chumvi ya Msamaha ni muhimu sana katika ulimwengu mamboleo! Baba Mtakatifu Francisko anasema, janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ni mtihani mkubwa katika ulimwengu mamboleo unaohitaji umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Huu ni muda wa kufanya tafakari makini kuhusu mitindo ya maisha, kwa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni changamoto pia ya kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote!

Viongozi wa Kisiasa

 

13 September 2021, 15:27