Baba Mtakatifu Francisko anasema maskini ni amana na utajiri wa Kanisa, wanapaswa kuheshimiwa, kuthaminiwa na kusaidiwa kwa hali na mali. Baba Mtakatifu Francisko anasema maskini ni amana na utajiri wa Kanisa, wanapaswa kuheshimiwa, kuthaminiwa na kusaidiwa kwa hali na mali. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Slovakia: Maskini na Kanisa!

Papa ameonesha furaha yake kubwa ya kukaribishwa na kuwa kati yao. Amewashukuru watawa wanaoendelea kujisadaka kwa ajili kuwakaribisha, kuwasindikiza na kuwahudumia wale wote wanaopata huduma kutoka katika Kituo hiki cha Bethlehemu. Amewahakikishia uwepo wa Kristo Yesu kati pamoja nao na anaendelea kufurahi pamoja nao na hata katika shida na magumu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, anawaalika Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza kutoka kwenye shule ya maskini. Kati ya maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum, humu humu kuna watakatifu na watu ambao wanaweza kuwafundisha wengine tunu msingi za maisha ya kijamii, kiutu na kiroho. Maskini si mzigo bali ni shule makini kwa watu wa Mungu. Kumbe, kuna umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Maskini ni kielelezo cha Kristo Yesu kati ya watu wake. Katika shule ya upendo, watu wanatafuta faraja, mahusiano na mafungamano; utu na heshima ya binadamu na kwa njia hii, waamini wanaweza kujifunza kutoka kwa maskini kwa kuwakaribisha, kuwasikiliza, kuwakirimia na kuwahudumia kwa upendo na nidhamu ya hali ya juu. Kanisa linawategemea sana maskini katika maisha na utume wake, kwani maskini ni amana na utajiri wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kimsingi, maskini ndio walengwa wakuu wa Injili. Dhana ya umaskini inajikita katika umaskini wa hali na mali; maadili na utu wema; kwani wote hawa, Kristo Yesu amejisadaka kwa ajili ya kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu. Wakristo wanapaswa kuwajali, kuwathamini na kuwapenda maskini na watu wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama afanyavyo mama mzazi kwa watoto wake. Kanisa linatoa huduma ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa maskini, kwa kujali na kuthamini utu, heshima na haki zao msingi, kwani hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa hija yake ya kitume nchini Slovakia kuanzia tarehe 12 hadi 15 Septemba 2021, Jumatatu tarehe 13 Septemba, ametembelea Kituo cha Maskini Bethlehemu, mjini Bratislava, kinachosimamiwa na kuendeshwa na Shirika la Wamisionari wa Upendo, maarufu kama Watawa wa Mama Theresa wa Calcutta.

Baba Mtakatifu ameonesha furaha yake kubwa ya kukaribishwa na kuwa kati yao. Amewashukuru na kuwapongeza watawa wanaoendelea kujisadaka kwa ajili kuwakaribisha, kuwasindikiza na kuwahudumia wale wote wanaopata huduma kutoka katika Kituo hiki cha Bethlehemu. Baba Mtakatifu amewahakikishia uwepo wa Kristo Yesu kati pamoja nao na anaendelea kufurahi pamoja nao na hata wanapokabiliwa na matatizo pamoja na changamoto za maisha. Daima Kristo Yesu yuko kati pamoja nao, hata kama haonekani kwa macho makavu ya kibinadamu! Kristo Yesu yuko kati pamoja nao hasa wakati wa magumu na majaribu ya maisha! Baba Mtakatifu katika ujumbe aliouandika kwenye Kitabu cha wageni anawashukuru watawa hawa kwa ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Anawashukuru na kuwapongeza pia wale wote wanaoshirikiana nao katika kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo. Bikira Maria awalinde na Mwenyezi Mungu awabariki!

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 4 Septemba 2016 alimtangaza Mama Theresa wa Calcutta kuwa Mtakatifu, kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Huruma ya Mungu kwa wafanyakazi wa huruma na wale wa kujitolea. Katika mahubiri yake, alikazia umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo wa Mungu. Waamini wawe ni mashuhuda wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Huruma iwe ni kielelezo cha sala na imani tendaji inayomwilishwa katika huduma na unyenyekevu. Waamini wanapaswa kuwa na ujasiri na kuthubutu kumwona na kumtambua Kristo Yesu kati ya watu wadogo, wanyonge na maskini. Wote hawa waoneshwe Injili ya matumaini, huruma na upendo. Mama Theresa wa Calcutta alisimama kidete kutangaza na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Aliinama na kuwaganga maskini kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini. Akasimama kidete kulinda: utu, heshima na haki zao msingi. Alikuwa ni sauti ya maskini na wanyonge duniani, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Mungu kati ya maskini.

Papa Maskini
14 September 2021, 10:10