Papa Francisko: Msalaba Mtakatifu ni Kitabu cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu kilichoandikwa kwa maisha ya Kristo Yesu Papa Francisko: Msalaba Mtakatifu ni Kitabu cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu kilichoandikwa kwa maisha ya Kristo Yesu 

Msalaba Ni Kitabu cha Maisha, Ufunuo na Huruma ya Mungu!

Papa ametafakari maana ya: Kuona na kishawishi cha kutokubali Fumbo la Msalaba; Kushuhudia upendo wa Mungu kwa unyenyekevu na kujitahidi kusoma Kitabu cha Msalaba kama alivyofanya Bikira Maria. Mwinjili Yohane aliona na kushuhudia Kristo Yesu akiteswa na kufa Msalabani akiwa kati kati ya majambazi wawili. Hata leo hii bado damu ya watu wasiokuwa na hatia inamwagika!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Slovakia kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 15 Septemba 2021 inanogeshwa na kauli mbiu “Pamoja na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu Njia ya Kwenda kwa Yesu.” Baba Mtakatifu Jumatatu asubuhi tarehe 14 Septemba 2021 Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba amesafiri kutoka Bratislava hadi Jimbo kuu la Prešov, ili kuadhimisha Liturujia Takatifu katika Madhehebu ya Kibizantina. Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba: Kashfa na chemchemi ya uhai; ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kama alivyoshuhudia Mwinjili Yohane akisema: “Naye aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua ya kuwa anasema kweli ili ninyi nanyi mpate kusadiki.” Yn 19:35. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake ametafakari kwa kina maana ya: Kuona na kishawishi cha kutokubali Fumbo la Msalaba; Kushuhudia upendo wa Mungu kwa unyenyekevu na kujitahidi kusoma Kitabu cha Msalaba kama alivyofanya Bikira Maria. Mwinjili Yohane aliona na kushuhudia Kristo Yesu akiteswa na kufa Msalabani akiwa kati kati ya majambazi wawili.

Hata leo hii bado damu ya watu wasiokuwa na hatia inaendelea kumwagika sehemu mbalimbali za dunia. Msalaba machoni pa walimwengu ni kielelezo cha kushindwa. Hata waamini wakati mwingine wanaweza kushindwa kuupokea Ujumbe wa Fumbo la Msalaba, chombo cha wokovu wa binadamu kilichotumiwa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Waamini wangependa kuona Ukristo wenye nguvu unaotangaza ushindi. Na kwa hakika anasema Baba Mtakatifu hiki ni kishawishi kikubwa! Ukristo pasi na Msalaba ni kielelezo cha kumezwa na malimwengu na huo ni mwelekeo hasi katika maisha ya kiroho! Mwinjili Yohane katika Fumbo la Msalaba aliiona kazi na utukufu na wokovu wa Mungu. Kwa haraka haraka waamini wanaweza kushindwa kuona ile nguvu na ujumbe wa Fumbo la Msalaba na kuanza kutamani kumwona Mungu mwenye “kujimwambafai.” Na hiki ni kishawishi kikubwa cha kutaka kuona Ukristo unaosimikwa katika utukufu, lakini ikumbukwe kwamba, Ukristo pasi na Msalaba ni kielelezo cha kumezwa na malimwengu na utasa wa maisha ya kiroho! Katika hali ya giza nene, upweke wa kutisha, hapo ndipo Mwenyezi Mungu anapoonesha uwepo wake angavu, nguvu na utukufu wake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Fumbo la Msalaba ni Kitabu cha Maisha, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu unaookoa. Mwandishi wa Kitabu hiki ni Kristo Yesu, kumbe, Msalaba unapaswa kuacha chapa ya kudumu katika maisha ya waamini. Vinginevyo, watu wataendelea kuvaa Msalaba kama mapambo shingoni, alama ya ibada na hata wakati mwingine kinzani na misigano ya kijamii au kielelezo cha dini na hali ya mtu. Tafakari ya Fumbo la Msalaba iwawezeshe waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kama walivyofanya: mashuhuda na waungamana imani. Hata nchini Slovakia kuna waamini ambao wameyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake! Hawa ni mashuhuda wa Fumbo la Msalaba unaojenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu, bila unafiki, ili kushuhudia unyenyekevu wa upendo unaopyaisha maisha kutoka katika undani wake na hatimaye kuzaa matunda ya kudumu kwa wakati wake.

Huu ni mwaliko kwa waamini kuendelea kupyaisha ushuhuda wao kwa Fumbo la Msalaba, changamoto ya kutangaza na kushuhudia imani katika uhalisia wa maisha kama walivyofanya mashujaa wa Slovakia. Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko amesema kwamba, Bikira Maria akiwa chini ya Msalaba alisoma Kitabu cha Fumbo la Msalaba na kukishuhudia kwa upendo na unyenyekevu mkuu. Kwa tunza na maombezi yake, waamini wawe na ujasiri wa kuyaelekeza mawazo na nyoyo zao kwa Kristo Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani. Katika hali na mazingira kama haya, imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake itaweza kustawi katika utimilifu wake na hatimaye kuzaa matunda kwa wakati wake. Kwa upande wake, Askofu mkuu Jàn Babjak wa Jimbo kuu la Prešov, amesema, tafakari ya Fumbo la Msalaba lipyaishe upendo na uaminifu kwa Kristo Yesu, Bikira Maria na Kanisa. Amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa jitihada zake za kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo! Amekuwa ni kielelezo makini cha Injili ya huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Fumbo la Msalaba ni mahali pa kutangaza na kushuhudia Ufunuo wa Uso wa huruma ya Mungu.

Liturujia Takatifu
14 September 2021, 16:48