Papa Francisko asikitishwa na mauaji ya kigaidi nchini Afghanistan. Atoa mwaliko kwa watu wa Mungu kusali, kufunga, kutubu na kumwongokea Mungu sanjari na ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Papa Francisko asikitishwa na mauaji ya kigaidi nchini Afghanistan. Atoa mwaliko kwa watu wa Mungu kusali, kufunga, kutubu na kumwongokea Mungu sanjari na ujenzi wa udugu wa kibinadamu. 

Papa Francisko Kwa Afghanistan: Sala, Kufunga, Toba na Umoja!

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wote kujikita zaidi katika kufunga, kusali na kufanya toba, ili kukimbilia upendo wa huruma ya Mungu na msamaha kwa watu wanaoteseka nchini Afghanistan. Itakumbukwa kwamba, bomu la kujitosa mhanga, Alhamisi tarehe 26 Agosti 2021 lilipelekea zaidi ya watu 170 kupoteza maisha na wengine zaidi 200 kujeruhiwa vibaya. Hali ni tete!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 29 Agosti 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican aliyaelekeza mawazo yake nchini Afghanistan, ambayo kwa sasa imegeuka kuwa ni uwanja wa fujo. Baba Mtakatifu anasema, anaendelea kufuatilia kwa karibu zaidi machafuko ya kisiasa nchini Afghanistan. Anashiriki uchungu wa wale wanaolia na kuwaombolezea ndugu, jamaa na rafiki zao waliouwawa hivi karibuni kutokana na bomu la kujitosa mhanga pamoja na wale wote wanaotafuta msaada na ulinzi kwa maisha yao. Wote hawa, Baba Mtakatifu anapenda kuwaweka chini ya huruma ya Mwenyezi Mungu wale wote waliofariki dunia na anaendelea kuwashukuru na kuwapongeza wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Afghanistan wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha, na kwa namna ya pekee kabisa, wanawake na watoto. Baba Mtakatifu anawaalika watu wote kuendelea kuwasaidia wananchi wa Afghanistan sanjari na kusali ili majadiliano katika ukweli na uwazi pamoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu uwe ni chemchemi ya matumaini kwa ajili ya maisha bora zaidi kwa watu wa Mungu nchini Afghanistan.

Kwa namna ya pekee kabisa katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anawaalika watu wote kujikita zaidi katika kufunga, kusali na kufanya toba, ili kukimbilia upendo wa huruma ya Mungu na msamaha kwa watu wanaoteseka nchini Afghanistan. Itakumbukwa kwamba, bomu la kujitosa mhanga, Alhamisi tarehe 26 Agosti 2021 lilipelekea zaidi ya watu 170 kupoteza maisha na wengine zaidi 200 kujeruhiwa vibaya. Jeshi la Marekani liliwapoteza wanajeshi vijana 13 waliokuwa na umri kati ya miaka 20-31. Miili yao tayari imerejeshwa nchini Marekani kwa maziko ya kitaifa! Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea karibu na uwanja wa ndege wa Kabul nchini Afghanistan. Kwa sasa hali bado ni tete nchini Afghanstan na kwamba, Umoja wa Mataifa utaendelea kujizatiti zaidi kutoa msaada na kwamba, kuna haja ya kulinda usalama wa maisha ya wananchi wa Afghanistan pamoja na miundombinu. ISIS-K imejigamba kuhusika na shambulio hili la kigaidi na kwamba, bado kuna wasi wasi kwamba, mashambulio mengine yakajitokeza nchini Afghanistan.

Papa Afghanistan

 

 

30 August 2021, 14:53