Watawa wawili wa Shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu nchini Sudan ya Kusini wamepigwa risasi na kuuwawa wengine 5 walikimbilia msituni, huku wakisindikizwa na mvua ya risasi. Watawa wawili wa Shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu nchini Sudan ya Kusini wamepigwa risasi na kuuwawa wengine 5 walikimbilia msituni, huku wakisindikizwa na mvua ya risasi. 

Watawa Wawili Wauwa Kwa Risasi, Wengine 5 Waponea Chupuchupu!

Ni matumaini ya Papa Francisko kwamba, mauaji haya yatakuwa ni kichocheo kikuu cha amani, upatanisho na usalama katika Ukanda huu. Marehemu wapumzike kwa amani na wale wote wanaowaombolezea, wafarijike kwa sadaka yake! Baba Mtakatifu anapenda kutoa baraka zake za kitume, wote wafarijike kwa nguvu na ushindi wa Kristo Yesu Mfufuka dhidi ya dhambi na mauti!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika salam za rambirambi zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, anapenda kuonesha masikitiko yake makubwa kwa mauaji ya kinyama dhidi ya watawa wawili wa Shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu, waliokuwa wanatekeleza utume wao, Jimbo kuu la Juba, nchini Sudan ya Kusini. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anamkumbuka na kumwombea Marehemu Sr. Mary Daniel Abut aliyekuwa Mama mkuu wa Shirika kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2018. Hadi mauti yanamfika, alikuwa ni Mwalimu mkuu wa Shule ya Usra Tuna, Jimbo kuu la Juba. Baba Mtakatifu anamwombea pia Marehemu Sr. Regina Roba aliyeuwawa pia katika shambulizi la kushtukiza hapo tarehe 16 Agosti 2021.

Baba Mtakatifu anapenda kutuma salam za rambirambi kwa wazazi, ndugu, jamaa pamoja na Shirika la Masista wa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, mauaji haya yatakuwa ni kichocheo kikuu cha amani, upatanisho na usalama katika Ukanda huu. Marehemu wapumzike kwa amani na wale wote wanaowaombolezea, wafarijike kwa sala na sadaka yake! Baba Mtakatifu anapenda kutoa baraka zake za kitume kwa wale wote watakaoshiriki katika Ibada ya mazishi kwa Masista hawa Marehemu, wafarijike kwa nguvu na ushindi wa Kristo Yesu Mfufuka dhidi ya dhambi na mauti! Habari zaidi zinabainisha kwamba, ndani ya gari kulikuwemo Masista saba waliokuwa wanatoka kuadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya Parokia ya Loa, Jimbo Katoliki la Torit ambalo ni sehemu ya Jimbo kuu la Juba, Sudan ya Kusini.

Masista wengine watano, waliweza kukimbia na kutokomea msituni, huku wakiwa wanaandamwa na “mvua za risasi” kiasi cha kupatwa na majeraha. Taarifa zaidi zinasema, Jeshi la Polisi nchini Sudan ya Kusini, tayari limewatia pingu waliohusika na mauaji ya watawa hao wawili na muda wowote ule wanatarajiwa kufikishwa mbele ya Mahakama kujibu shutuma zinazowasibu. Haki, amani na utulivu ni kati ya changamoto kubwa zinazoendelea kujitokeza nchini Sudan ya Kusini, ambayo tangu kujipatia uhuru wake, imegeuka kuwa ni uwanja wa mapambano ya silaha; uchu wa mali na madaraka. Matokeo yake ni hali nguvu ya uchumi, rushwa na ufisadi kuendelea kushamiri pamoja na mapambano ya silaha!

Mauaji ya Watawa
18 August 2021, 14:28