2021.08.13 Zawadi ya Papa Franciskoya vifaa za kuzuia maambukizi kwa Hospitali ya Mchungaji Mwema, Eswatini 2021.08.13 Zawadi ya Papa Franciskoya vifaa za kuzuia maambukizi kwa Hospitali ya Mchungaji Mwema, Eswatini 

Vifaa vya kuzuia maambukizi vya Uviko:zawadi ya Papa kwa Eswatini

Vifaa vya kiafya vimepelekwa katika Hospitali Katoliki ya Mchungaji Mwema ya Siteki katika serikali ya Eswatini,Afrika Kusini ili waweze kuzuia kwa namna bora maambukizi ya janga la uviko-19.Katika maneno ya Askofu José Luis Ponce de León wa jimbo la Manzini anamshukuru Papa Francisko kwa jukumu hai na uongozi wake katika kipindi hiki kigumu cha maisha ya binadamu.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Mashine mbili za kupitishia hewa ya mapafu, masanduku kumi ya mabarakoa za kikliniki aina ya N95 na vifaa vingine vya kupima mapigo, ndiyo msaada uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Hospitali Katoliki “Mchungaji Mwema huko Siteki, Eswatini, ili iweze kupambana vyema na janga la Uviko -19. Habari hiyo ilitangazwa tarehe 11 Agosti 2021 na askofu, José Luis Ponce de León wa Manzini ambaye, katika blogi yake binafsi, aliandika kuwa: “Tangu mwanzo wa janga hili linaloathiri ulimwengu wote, Baba Mtakatifu Francisko amechukua jukumu hai na kuongoza, iwe kusimamisha katekesi zake na hata kutoa mwaliko kwa ulimwengu wote kusali. Askofu de León amekumbuka hasa saa ya maombi “Statio Orbis” iliyoongozwa na Papa, peke yake, katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mnamo tarehe 27 Machi 2020, na kwamba ilikuwa ni picha ya ulimwengu uliokuwa unaishi umetengwa, lakini katika wakati huo huo ikionesha picha ya mchungaji ambaye alibaki karibu na zizi lake”, amebainisha Askofu wa Manzini”.

Maombi, chanjo na mshikamano

Hata hivyo kiongozi huyo ameongeza: "Baadaye, chanjo ilipopatikana Papa alipata chanjo na kuhimiza ulimwengu wote kufanya vivyo hivyo, akielezea kuwa chanjo sio kuokoa maisha tu, bali pia chaguo la kimaadili”. Kwa kuongezea, Askofu de León: "Papa alikumbusha mara kwa mara juu ya hitaji la upatikanaji wa chanjo kwa wote, akihimiza kusimamishwa kwa muda kwa hati ya haki miliki. Maombi, chanjo na mshikamano vilikuwa, kwa maana hiyo, vyombo vilivyotumiwa na Baba Mtakatifu dhidi ya janga hili”, huku Askofu akisisitiza kwamba "ni sababu ambazo tunamshukuru sana na vile vile nyenzo tulizopewa”. Kwa kuhitimisha Askofu wa Manzini amesema: “Wakati huu  maneno ya Yesu yananikumbusha mwishoni mwa mfano wa Msamaria Mwema, ambayo ni, “Nenda ukafanye hivyo wewe mwenyewe”. "Mfano wa Baba Mtakatifu Francisko, kiukweli, sio tu kwa viongozi wa kidini, bali kwa sisi sote: kama Wasamaria wema wa leo, tunaitwa kusali, kuheshimu itifaki za kuzuia uviko, kujipatia chanjo, kuhimiza wengine kufanya vivyo hivyo na kusaidia wale wanaohitaji sana”. Ushauri ambao unatoka kwa kiongozi huyo ni baraka kwa wahudumu wote wa afya na madaktari wa hospitali Katoliki ya Siteki.

Zawadi zilizotumwa kwa Eswatini
Zawadi zilizotumwa kwa Eswatini

Maambukizi ya Uviko Eswatini na kampeni ya chanjo

Ikumbukwe kwamba, hadi leo hii, huko Eswatini, kuna visa zaidi ya elfu 34 za Uviko-19, na zaidi ya vifo 900. Mnamo Januari, na mlipuko wa ulioitwa “wimbi la Afrika Kusini la virusi, hatua za kuzuia magonjwa ya kuambukiza zilianza kutumika kwa wiki mbili, na kusababisha kusimamishwa kwa Misa na ushiriki wa watu wa Mungu. Wakati huo huo, kampeni ya chanjo inaendelea polepole: hadi sasa, ni zaidi ya asilimia 7 tu ya idadi ya watu wamepewa kipimo hicho kwa mara ya pili.

13 August 2021, 15:24