Sala ya Papa wanamichezo huko Tokyo na waathiriwa wa tetemeko la ardhi Italia
Na Sr. Angea Rwezaula – Vatican.
Mara baada ya katekesi yake Jumatano tarehe 25 Agosti 2021 katika ukumbi wa Paulo VI, jijini Vatcan, Papa Francisko akiwasalimia watu kwa lugha ya kiitaliano amewakumbuka kundi la pili la wanamichezo wa Olimpiki huko Tokyo ambao wameanza michuano yao itakayomalizika tarehe 5 Septemba 2021. Kwa maana hiyo ametoa salamu na shukrani zake kwa wanariadha hao kwa ushuhuda wa matumaini na ujasiri ambao wanatoa kwa kila mtu. Baba Mtakatifu amesema kuwa, “kiukweli, wanaonesha jinsi gani ya kujitolea kwa michezo kunasaidia kushinda shida zinazoonekana kuwa ni ngumu”.
Tetemeko la ardhi la 24 Agosti 2016
Baba Mtakatifu Francisko pia amekumbuka wahanga wa tetemeko la ardhi lililotokea karibu na mji wa Montegallo, katikati mwa Italia, miaka mitano iliyopita, mnamo tarehe 24 Agosti 2016. Tetemeko la ardhi la kutisha lenye kipeo cha 6.2 lilisababisha vifo zaidi ya watu 250 na kuwaacha maelfu ya majeruhi wakati huo huo na kusababisha uharibifu mkubwa wa majengo na mali nyingine ambapo hadi sasa bado hayajajengwa na wala kukarabatiwa.
Papa amesema “kaka na dada wapendwa, uwepo wenu unanipa nafasi ya kugeuza mawazo yangu kwa waathiriwa na kwa jamii zote katikati mwa Italia, pamoja na Accumoli na Amatrice, ambao walipata matokeo mabaya ya tukio hilo la tetemeko.” Baba Mtakatifu ameendelea kusisitiza umuhimu wa kuonesha kuzaliwa upya kutoka katika janga bila kuruhusu vipingamizi vya kutoamini na kwa msaada halisi wa taasisi mahalia. Papa amewaalika kuwa na ujasiri na kuendelea mbele kwa matumaini.