Papa Francisko: Katika majanga, mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu, Mama Kanisa anawaalika watoto wake kujikita katika sala, toba na kufunga ili kulilia huruma na upendo wa Mungu. Papa Francisko: Katika majanga, mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu, Mama Kanisa anawaalika watoto wake kujikita katika sala, toba na kufunga ili kulilia huruma na upendo wa Mungu. 

Papa: Nguvu ya Sala, Kufunga na Toba Kuomba Huruma ya Mungu!

Baba Mtakatifu anawaalika watu wote kuendelea kuwasaidia wananchi wa Afghanistan sanjari na kusali ili majadiliano katika ukweli na uwazi pamoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu uwe ni chemchemi ya matumaini kwa ajili ya maisha bora zaidi nchini Afghanistan. Anawataka watu: kufunga, kusali na kufanya toba, ili kukimbilia upendo wa huruma ya Mungu na msamaha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 29 Agosti 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican aliyaelekeza mawazo yake nchini Afghanistan, ambayo kwa sasa imetumbukia katika maafa makubwa. Baba Mtakatifu anapenda kuwaweka chini ya huruma ya Mwenyezi Mungu wale wote waliofariki dunia na anaendelea kuwashukuru na kuwapongeza wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Afghanistan wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha, na kwa namna ya pekee kabisa, wanawake na watoto. Baba Mtakatifu anawaalika watu wote kuendelea kuwasaidia wananchi wa Afghanistan sanjari na kusali ili majadiliano katika ukweli na uwazi pamoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu uwe ni chemchemi ya matumaini kwa ajili ya maisha bora zaidi kwa watu wa Mungu nchini Afghanistan. Kwa namna ya pekee kabisa katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anawaalika watu wote kujikita zaidi katika kufunga, kusali na kufanya toba, ili kukimbilia upendo wa huruma ya Mungu na msamaha kwa watu wanaoteseka nchini Afghanistan.

Hii ni si mara ya kwanza kwa Baba Mtakatifu Francisko kuwaalika waamini kusali, kufunga na kufanya toba kwa ajili ya kuombea: haki, amani na usalama katika maeneo ya vita. Alifanya hivi tarehe 7 Septemba 2013 kwa ajili ya kuombea amani nchini Siria. Mwaka 2017, waamini na watu wote wenye mapenzi mema walikusanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kuombea amani nchini Sudan ya Kusini na DRC. Baba Mtakatifu Francisko alitoa wito kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema Ijumaa tarehe 4 Septemba 2020 kufunga, kutubu na kusali kwa ajili ya kuombea amani, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu nchini Lebanon, kama alivyofanya Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1989, zaidi ya miaka thelathini iliyopita. Kutokana na matatizo na changamoto zinazofahamika na wananchi wa Lebanon, Kanisa linatambua hatari kubwa inayoinyemelea Lebanon kwa wakati huu. Yaani athari za Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 pamoja na janga la mlipuko wa mji wa Beirut. Ni katika muktadha huu, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, yenye makao yake makuu mjini Roma, iliyoanzishwa rasmi tarehe 7 Februari 1968 inaendelea kujikita katika maisha ya Sala, Huduma kwa Maskini na Amani duniani; mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha kwanza na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo.

Jumuiya hii katika kipindi cha miaka zaidi ya 50 ya uhai wake, imekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa maskini; watu wasiokuwa na makazi rasmi; watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi Barani Afrika na Amerika ya Kusini; bila kusahau huduma ya elimu kwa watoto wanaofundwa katika “Shule ya Amani”. Jumuiya imeendelea pia kuwahudumia wagonjwa na waathirika wa UKIMWI kwa njia ya utekelezaji wa Miradi ya “The Dream” pamoja na BRAVO”. Majadiliano ya kidini na kiekumene yamekuwa ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wake, mintarafu ari, moyo na changamoto zilizotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II wakati wa mkutano wa kuombea Amani Duniani, tarehe 4 Oktoba 1992. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio imechangia kwa kiasi kikubwa hata kusitishwa kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Msumbiji. Imekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji pamoja na kuhakikisha kwamba, wakimbizi na wahamiaji hawa wanashirikishwa kikamilifu katika maisha ya jamii inayowakarimu.

Professa Andrea Riccardi, Muasisi wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio anasema kwamba, upendo wenye huruma na wokovu wa Mungu uwaambate na kuwakumbatia watu wote pasi na ubaguzi. Ubaguzi ni dhambi kubwa na hatari katika mafungamano ya kijamii. Injili ya Kristo Yesu iwe ni silaha madhubuti ya kuchochea ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na hivyo kuondokana na ubaguzi unaoweza kufanywa kwa misingi ya kiitikadi, kitaifa au kikabila. Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu, kwa kuendelea kujikita katika ujenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu! Huu ni wakati wa kujenga utamaduni wa watu kukutana katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana. Nguvu ya Mama Kanisa inajikita katika sala na ushuhuda ili kuvuka kipeo cha utandawazi usiokuwa na mashiko wala mvuto! Professa Andrea Riccardi bado anakumbuka sana ile Siku ya Sala ya Kiekumene iliyoadhimishwa Jumamosi, tarehe 7 Julai 2018 huko Bari, Kusini mwa Italia kwa kuwakutanisha viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo kwa ajili ya tafakari na kuombea amani na umoja huko Mashariki ya Kati.

Siku hii ilinogeshwa na kauli mbiu “Amani ikae nawe: Umoja wa Wakristo kwa ajili ya Mashariki ya Kati”. Baba Mtakatifu alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuifanikisha Siku ya Sala ya Kiekumene, alama makini ya umoja wa Wakristo na ushiriki wa familia ya Mungu katika ujumla wake. Madonda ya vita huko Mashariki ya Kati yanaendelea kuwaathiri wananchi wa kawaida huko Siria, kiasi hata cha kuwatumbukiza katika majanga ya maisha: umaskini, magonjwa na njaa! Vita imekuwa ni sababu ya kuibuka kwa misimamo mikali ya kidini na kiimani, kiasi hata cha kufanya kufuru ya matumizi ya jina la Mungu. Lakini, vita hii, imeendelea kukuzwa kutokana na biashara haramu ya silaha, changamoto ambayo inapaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa, lakini zaidi na Nchi tajiri zaidi duniani.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 30 Agosti 2021 alikutana na kuzungumza kwa faragha na Professa Andrea Riccardi. Kati ya tema walizogusia ni janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, Machafuko ya kisiasa nchini Afghanistan na umuhimu wa ujenzi wa upendo, umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Malengo ya Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni pamoja na: kuhamasisha ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaoratibiwa na kanuni auni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni dhana inayokumbatia maisha ya kifamilia, kijamii, kitaifa na kimataifa. Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya kujenga na kudumisha tasaufi ya udugu wa kibinadamu kama chombo cha kufanyia kazi katika medani za kimataifa, ili kusaidia kupata suluhu ya matatizo yanayoikumba Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni msaada mkubwa katika kupambana na changamoto mamboleo kama vile: Vita na kinzani mbali mbali; baa la njaa na umaskini duniani pamoja na athari za uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Kipaumbele cha kwanza ni ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mshikamano wa kidugu usaidie ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya Jumuitya ya Kimataifa kama ilivyo pia miongoni mwa wananchi wenyewe. Ujasiri na ukarimu ni mambo yanayohitajika ili kufikia malengo ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Papa Nguvu ya Sala

 

31 August 2021, 15:49