Ujumbe wa Papa kwa Caritas Argentina ni kupenda na huduma kwa ishara za nyakati!

Katika ujumbe wa Papa kwa njia ya video,anaungana kiroho na mchakato wa Jumuiya katika safari 2021 iliyoanzishwa na Caritas nchini Argentina katika muktadha wa mchakato wa kitaasisi ambao unafanyika kwa miaka mitatu.”Ni uzoefu wa kujiweka tayari katika safari ya kusikilizana na kufanya mang’amuzi kama ilivyo kupenda kwa dhati katika ulimwengu wa leo hii”anasema Papa kwa washiriki hao.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Safari ya 2021 ni kipindi cha kufanya mang’amuzi ya kijumuiya katika hatua tofauti ambazo zitakuwa kwa kipindi cha miaka mitatu kichachowahusu wakala wote wa kichungaji wa Caritas nchini Argentina, ambao ni wahudumu wa kila ngazi (kiparokia, kijimbo na kitaifa), na hawa ni wakuu wa mipango, washirika wa kitume kwa ajili ya kutafakari na kusikilizana kwa pamoja katika mwanga wa roho mtakatifu ili kutathimini changamoto zilizopo na zile zijazo. Katika kufanya  hija hiyo ya safari ya kijumuiya na kisinodi katikati ya maisha na katika matumaini ya jumuiya ya Nchi, anaunganika hata Papa Francisko kwa kuwatumia ujumbe salamu, ukaribu, matashi mema na kuwatia moyo kwa njia ya video.

Papa anasema: “Kwa mara nyingine tena ninajiruhusu kuwasalimia katika safari hiyo. Safari ya 2021 ni mchakato wa kisinodi ambao unafanyika kwa miaka mitatu. Ni uzoefu wa kutufanya kujiweka tayari katika hatua ya kutoka nje, kujisikiliza na kufanya mang’amuzi ya  jinsi gani ya kupenda na kuhudumia kwa dhati katika misingi ya kipindi na wakati. Na hasa kwa kutazama ishara za nyakati na mahalia. Ninawatakia mema ya kwamba Bwana awasindikiza katika safari na tafadhali msisahau kusali kwa ajili yangu”.

PAPA FRANCISKO NA UJUMBE WAKE  KWA CARITAS ARGENTINA
PAPA FRANCISKO NA UJUMBE WAKE KWA CARITAS ARGENTINA

Kwa mujibu wa waandaaji wa tukio hili wanaandika kuwa “leo hii, katika kipindi cha janga, safari hii inakuwa kama fursa ya kushirikishana yale mafunzo yaliyopatikana, ili kutiana moyo na kuwasha tena huduma ya kiroho kwa kuweka mikono, macho na moyo ili kupata majibu ya kina na yanayostahili katika mahitaji ya ubinadamu wa leo hii. Kwa maana hiyo, ni katika kuota ndoto pamoja, kushinda tofauti na kung’amua njia mpya. Safari ya 2021 inawaalika katika mchakato wa safari ya ndani ya kila mmoja wao kwa ajili ya  usali, kushukuru, kuomba, ili kupata amani na faraja kutoka kwa Yule ambaye anafanya mambo yote kuwa  mapya na ambaye anaeleza kuwa “ lolote lile mfanyalo kwa aliye mdogo ambao ni kaka na dada , mnafanyia na mimi”. Wanaongeza kuandika “ Yeye anatualika kutembea pamoja kama mitume wa kimisionari, na kuwa namna hii kama Kanisa ambalo linatafakari kauli mbiu “Sisi Caritas: uwepo unaotunza, vizingiti vinavyokutana na shauku inayobadirisha".

Kwa upande wa Caritas Argentina inaeleza kuwa safari ya 2021 ina michakato miwili, kwa upande mmoja, ni hija ya Picha ya Bikira Maria na Yosefu na Mtoto kupitia kila mkoa na kila jimbo, kuzungukia kila mji na jumumiya ili kuamsha tena furaha na tumaini ambalo linazailiwa na imani ya watu wa Mungu. Na kwa upande wa pili, ni kufanya mang’amuzi ya kichungaji kwa kila jimbo ambayo yanapekelea mapendekezo na wakati huo huo, ambayo yanasaidia kujua ishara ambazo Mungu anaibua tena kila sehemu na kuendelea kutafakari kwa kina daima katika maelekezo ya kichungaji kwa ajili ya upendo mkuu kwa Kanisa.

26 August 2021, 10:00