Baba Mtakatifu Francisko kuhusu chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 anasema, kuchanjwa ni kitendo cha upendo kwa kwako mwenyewe, familia na jamii katika ujumla wake. Baba Mtakatifu Francisko kuhusu chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 anasema, kuchanjwa ni kitendo cha upendo kwa kwako mwenyewe, familia na jamii katika ujumla wake. 

Papa Francisko Kuchanjwa Dhidi UVIKO-19 Ni Kitendo Cha UPENDO

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuchanjwa chanjo iliyoidhinishwa na Serikali na Mamlaka husika ni kitendo cha upendo. Na ikiwa kama watu wengi zaidi watapata chanjo dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO-19 ni kitendo cha upendo wa hali ya juu kabisa. Huu ni upendo wa mtu binafsi; upendo kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na hatimaye ni upendo kwa watu wote. Watu wakachanje!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Kimaadili na kiutu inakubalika kutumia chanjo iliyotengenezwa kutokana na chembe chembe za mimba zilizoharibiwa. Mtu anaweza kuamua kutokutumia chanjo hii, lakini kutokana na madhara na hatari kubwa ya ugonjwa huu unaoendelea kusababisha vifo vya watu wengi duniani, kumbe, inaruhusiwa kutumia chanjo zote zinazopatikana, ikiwa kama zimeidhinishwa kuwa ni salama na zina ufanisi mkubwa katika kuzuia Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa linakaza kusema ni wajibu wa kimaadili kwa makampuni ya dawa, mawakala na watengenezaji wa dawa za Serikali kuhakikisha kwamba, wanazalisha, wanaidhinisha, kugawa na kutoa chanjo ambazo zinakubalika kimaadili na kiutu, ambazo kimsingi hazisababishi matatizo kwenye dhamiri za watu. Ikumbukwe kwamba, kimsingi chanjo si kanuni wala jambo la lazima kimaadili, bali linapaswa kuwa ni hiyari ya mtu mwenyewe na inapaswa kuzingatia mafao na ustawi wa wengi katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Chanjo itoe kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wanyonge ndani ya jamii.

Kwa wale wanaokataa kutumia chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 kwa sababu mchakato wa chanjo hii umetumia pia chembe chembe za mimba zilizoharibiwa wakumbuke kwamba, wanao wajibu wa kimaadili kuhakikisha kwamba, wanajilinda wao wenyewe na wala wasiwe ni sababu ya maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 kwa watu wengine. Hapa kuna haja ya kuhakikisha kwamba, usalama na afya za watu wengine unalindwa kikamilifu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 18 Agosti 2021, ameungana na viongozi mbalimbali wa Kanisa kuhamasisha ushiriki wa waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema katika chanjo inayoendelea kutolewa sehemu mbalimbali za dunia kama njia ya kudhibiti maambukizi na maafa makubwa yanayosababishwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Jambo la muhimu kuzingatia ni kuhakikisha kwamba, chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ni salama, ina ufanisi na kwamba, inaokoa maisha ya watu.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuchukua fursa hii, kumshukuru Mwenyezi Mungu na hivyo kujiunga katika kampeni ya chanjo dhidi ya UVIKO-19, kwa kutoa ujumbe wa matumaini ya kesho inayong’ara zaidi. Kazi hii ni matunda ya ushirikiano wa watu wengi walioiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kupata chanjo inayoweza walau kuwalinda watu wa Mungu dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Chanjo inatoa matumaini ya kuweza kudhibiti janga hili, lakini ikiwa kama chanjo hii itapatikana kwa wote na ikiwa kama wote watashirikiana kikamilifu! Baba Mtakatifu anasema, kuchanjwa chanjo iliyoidhinishwa na Serikali na Mamlaka husika ni kitendo cha upendo. Na ikiwa kama watu wengi zaidi watapata chanjo dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO-19 ni kitendo cha upendo wa hali ya juu kabisa. Huu ni upendo wa mtu binafsi; upendo kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na hatimaye ni upendo kwa watu wote. Baba Mtakatifu anakaza kusema, upendo pia unafumbatwa katika masuala ya kijamii na kisiasa kwa sababu kuna upendo jamii na upendo wa kisiasa. Huu ni upendo kwa watu wote unaoshuhudiwa katika matendo madogo madogo yanayoweza kusaidia mchakato wa maboresho ya kijamii.

Chanjo ni jambo la kawaida, lakini linapata uzito wake kwa kusaidia kuragibisha maendeleo, ustawi na mafao ya wengi; kwa watu kulindana na hasa zaidi kwa wale wanaoishi katika mazingira hatarishi zaidi. Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa njia ya video kwa kuonesha matumaini kwamba, watu wengi watajitokeza kuchanjwa kama kielelezo cha upendo. Na kwa njia ya matendo haya madogo madogo wanaweza kusaidia mchakato wa maboresho ya maisha ya watu kwa sasa na kwa siku za usoni! Viongozi mbalimbali wa Kanisa na jamii katika ujumla wake, wanahimizwa kuunga mkono kampeni ya chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona inayoongozwa na kauli mbiu “It’s Up to You” kwa Kiswahili chepesi, tunaweza kusema, “Ni Shauri Yako”. Hii ni kampeni inayowaunganisha hata viongozi mashuhuri wa kisiasa pamoja na wasanii maarufu duniani! Lengo ni kuokoa maisha ya watu na wala si vinginevyo!

Papa Chanjo Korona

 

 

18 August 2021, 15:41