Papa Francisko Chanjo dhidi ya UVIKo-19 ni wajibu wa kimaadili kwa kila mtu ili kuhakikisha usalama, ustawi na maendeleo ya wengi. Papa Francisko Chanjo dhidi ya UVIKo-19 ni wajibu wa kimaadili kwa kila mtu ili kuhakikisha usalama, ustawi na maendeleo ya wengi. 

Papa Francisko: Chanjo Dhidi ya UVIKO-19 Ni Wajibu wa Kimaadili!

Chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ni wajibu wa kimaadili kwa kila mtu, ili kuhakikisha usalama, ustawi na maendeleo ya wengi. Hakuna mtu anayeweza kujidai kuwa ni salama dhidi ya UVIKO-19, huu ni ugonjwa hatari ambao haubagui wala kuchagua. Kwa bahati mbaya sana, chanjo hii imepokelewa kwa hisia tofauti sana na malengo yanayokusudiwa kisayansi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, chanjo ni sehemu ya utekelezaji wa mchakato wa ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu. Kwa njia hii, watu wanajenga udugu na ujirani mwema kwa njia ya chanjo, ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza kutokana na athari za Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ili hatimaye, kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Huu ni utamaduni unaosababisha maafa na utengano! Ujirani mwema ni dhana inayopaswa kufanyiwa kazi, ili kujenga umoja na mafungamano ya kijamii, kitaifa na ndani ya Kanisa katika ujumla wake. Chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ni wajibu wa kimaadili kwa kila mtu, ili kuhakikisha usalama, ustawi na maendeleo ya wengi. Hakuna mtu anayeweza kujidai kuwa ni salama dhidi ya UVIKO-19, kwani huu ni ugonjwa hatari ambao haubagui wala kuchagua. Kwa bahati mbaya sana, chanjo hii imepokelewa kwa hisia tofauti sana na malengo yanayokusudiwa kisayansi!

Ufanisi na usalama wa chanjo dhidi ya UVIKO-19 ni kati ya vipaumbele vinavyotolewa na Shirika la Afya Duniani, WHO kwa wakati huu. Chanjo dhidi UVIKO-19 lazima ipatikane kwa kila mtu mahali alipo! Huu ndio mkakati wa Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa mapambano dhidi ya UVIKO-19. Hivi karibuni, Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu kwa kushirikiana na Taasisi ya Kipapa ya Maisha (Pontificia Academia Pro Vita), wamechapisha Waraka unaoonesha umuhimu wa chanjo; na chanjo Kama Sehemu ya mafao ya wengi. Waraka huu ulitoa angalisho dhidi ya chanjo zinazokumbatia utaifa, kwa baadhi ya Mataifa kutaka kuwa na chanjo zake binafsi, kwa kuhakikisha kwamba, zinapata kiasi kikubwa cha dawa ya chanjo kwa ajili ya wananchi wake. Hii ni hatari sana, kwani uzalishaji na usambazaji wa chanjo hii unaweza kujikuta unawanufaisha watu wachache peke yao na hivyo, kutawala soko la chanjo kwa kupanga bei wanayoitaka wao wenyewe hata kama ni kwa hasara ya watu wengi duniani.

Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, “Urbi et Orbi” wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Noeli tarehe 25 Desemba 2020 aliwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumtafakari Mtoto Yesu aliyewawezesha kuwa ndugu wamoja. Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika kipindi hiki cha historia ya mwanadamu, kimeguswa na kutikiswa kwa namna ya pekee kabisa na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Hali hii imechangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa uchumi na hivyo kusababisha mwelekeo tenge katika jamii, hali inayodai ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu. Mwenyezi Mungu amewapatia Mwanaye wa pekee, Kristo Yesu, ili aweze kuwa ndugu yao. Huu ni undugu unaofumbatwa katika upendo unaomwezesha mtu kukutana na jirani zake, licha ya tofauti zao msingi. Kwa njia hii, ataweza kuguswa na mateso na mahangaiko yake, tayari kumkaribia, ili kuweza kumhudumia kama alivyofanya yule Msamaria mwema.

Haijalishi kama mtu huyu anatoka katika familia, kabila au dini yake, lakini ni ndugu yake. Mwelekeo huu ndio unaopaswa kuzingatiwa hata katika mahusiano na mafungamano kati ya watu na Mataifa. Nyota angavu ya Bethlehemu iwe ni chanzo cha matumaini mapya na ushirikiano wa Kimataifa, ili watu wengi zaidi waweze kupata chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 kwa kuondokana na uchoyo na utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko. Haki ya huduma bora ya afya, iwe ni kipimo cha upendo unaopaswa kushuhudiwa na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Huu ni wakati wa kushirikiana na kushikamana na wala si wa kufanya mashindano. Ni muda wa kutafuta suluhu ya kudumu, itakayowawezesha watu wengi zaidi kupata chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Koroma, UVIKO-19. Maskini na wahitaji zaidi wapewe kipaumbele cha kwanza.  Mtoto Yesu aliyezaliwa mjini Bethlehemu awasaidie watu kuwajibika barabara, kwa kuonesha ukarimu na mshikamano hasa kwa maskini na wanyonge zaidi katika jamii; maskini, watu wasiokuwa na ajira na wale wote wanaoteseka kutokana na athari za ugonjwa wa UVIKO-19, bila kuwasahau wanawake na wasichana ambao katika kipindi hiki wamekumbana na nyanyaso za kijinsia katika maisha yao.

Kristo Yesu, Mwana wa Mungu awawezeshe viongozi wa kisiasa na wale wote wenye dhamana ya kuongoza jamii, kuona umuhimu wa kugundua tena upyaisho wa ushirikiano kimataifa, huku wakianzia kwenye sekta ya afya, ili watu wote waweze kupata fursa ya chanjo na huduma msingi za afya. Katika changamoto hii ambayo haitambui mipaka, hakuna sababu msingi ya kuweka vizuizi, kwa sababu binadamu wote wamejikuta wakiwa wamepanda “boti moja” ambayo kwa sasa imekumbwa na dhoruba ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Watu wote wajisikie kuwa ni ndugu wamoja; watu wanaoakisi Sura ya Mungu hasa wale wanaoteseka na kwamba, Mwenyezi Mungu anaomba msaada kwa ajili yao. Watu wajitahidi kumwona Mwenyezi Mungu kati ya wagonjwa, maskini, wasiokuwa na ajira, wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; wamwone Mungu kati ya wakimbizi na wahamiaji.

Wakati huo huo, Kardinali Raymond Leo Burke, Mwenyekiti mstaafu wa Mahakama Kuu ya Kanisa Katoliki na Mlezi wa Kikosi cha Kijeshi cha Kitume cha Malta, kuanzia tarehe 11 Agosti 2021 amelazwa hospitalini huko Winsconsin nchini Marekani baada ya kugunduliwa kwamba, alikuwa anashambuliwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Kardinali Raymond Leo Burke anasema amegunduliwa kuwa anashambuliwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Anamshukuru Mwenyezi Mungu baada ya kupitia changamoto kubwa za kupumua, kwa sasa anaendelea kupata nafuu. Kardinali Raymond Leo Burke, anawashukuru Madaktari na wafanyakazi wote wa sekta ya afya kwa huduma nzuri wanayoendelea kumpatia. Kwa namna ya pekee, anawaomba waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumkumbuka na kumwombea ili aweze kupona haraka na kurejea katika maisha yake ya kawaida.

Kardinali Raymond Leo Burke anaendelea kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo. Timu ya madaktari inayomuuguza Kardinali Burke inasema kwamba, Kardinali Burke anaendelea vizuri. Wanatoa mwaliko kwa kusali pamoja naye Rozari Takatifu. Kardinali Raymond Leo Burke mwenye umri wa miaka 74 aliteuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Mwenyekiti wa Mahakama Kuu ya Kanisa Katoliki kunako mwaka 2008 na kung’atuka madarakani tarehe 8 Novemba 2014. Kabla ya kuteuliwa katika nafasi hii, Kardinali Raymond Leo Burke, alikuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo la Saint Louis, nchini Marekani. Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 umepulitisha sana maisha ya Wakleri na Watawa sehemu mbalimballi za dunia. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna Makardinali kadhaa, wamekwisha kuambukizwa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kati yao ni Makardinali wafuatao: Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma. Kardinali Philippe Nakellentuba Ouédraogo wa Jimbo Kuu Katoliki la Ouagadougou. Kardinali Daniel Fernando Sturla Berhouet, S.D.B. wa Jimbo kuu la Montevideo, Uruguay. Wengine ni Kardinali Celestino Aós Braco, O.F.M. Cap. Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Santiago de Chile pamoja na Kardinal Matteo Maria Zuppi, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bologna, nchini Italia.

Papa UVIKo 19

 

 

17 August 2021, 15:21