Baba Mtakatifu Francisko amemaliza likizo ya kipindi cha kiangazi, Julai 2021 na tayari Jumatano tarehe 4 Agosti 2021 anaendelea na Katekesi kuhusu Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia. Baba Mtakatifu Francisko amemaliza likizo ya kipindi cha kiangazi, Julai 2021 na tayari Jumatano tarehe 4 Agosti 2021 anaendelea na Katekesi kuhusu Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia. 

Papa Francisko Amaliza Likizo: Tarehe 4 Agosti 2021 Katekesi!

Baba Mtakatifu tarehe 4 Agosti 2021 anaendelea na Katekesi kuhusu Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia. Katekesi hii inafanyika kwenye Ukumbi wa Paulo VI kuanzia majira ya saa 3:15 kwa saa za Ulaya. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu baada ya kumaliza Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala, ameanza Katekesi Kuhusu Waraka Wa Mtume Paulo kwa Wagalatia. Biblia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko baada ya mapumziko ya Kipindi cha Kiangazi, Julai 2021 sanjari na mapumziko baada ya kufanyiwa operesheni ya utumbo mpana hapo tarehe 4 Julai 2021 anarejea tena uringoni kuendelea na utume wake. Baba Mtakatifu tarehe 4 Agosti 2021 anaendelea na Katekesi kuhusu Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia. Katekesi hii inafanyika kwenye Ukumbi wa Paulo VI ulioko mjini Vatican kuanzia majira ya saa 3:15 kwa saa za Ulaya. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu baada ya kumaliza Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala, ameanza Katekesi Kuhusu Waraka Wa Mtume Paulo kwa Wagalatia. Ni Waraka unaowawezesha waamini kumfahamu zaidi Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa na tema msingi katika maisha na utume wake, zinazonogesha uzuri wa Injili. Anakazia toba na wongofu wa ndani na jinsi alivyoyasadaka maisha yake kwa ajili ya huduma ya Injili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Anazungumzia mambo msingi katika imani kwa kujikita zaidi kuhusu: uhuru, neema ya kuishi kikamilifu kama Mkristo. Waraka huu unagusa mambo nyeti hata katika nyakati hizi, kana kwamba, ni Waraka ulioandikwa kwa ajili ya waamini katika mapambazuko ya Millenia na Tatu ya Ukristo.

Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa anatoa kipaumbele cha kwanza katika mchakato wa utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema, uliomwezesha kutembelea Jumuiya ya Wagalatia walau mara mbili, wakati wa safari zake za kimisionari. Kuna mambo mengi ambayo hayana majibu ya moja kwa moja. Paulo alikuwa ni Mtume kweli kweli! Anuani, msingi na muhtasari wa Injili ya Paulo unabubujika kutoka katika sehemu hii ya Maandiko Matakatifu: “Paulo, mtume, (si mtume wa wanadamu, wala kutumwa na mwanadamu, bali na Yesu Kristo, na Mungu Baba aliyemfufua kutoka kwa wafu), na ndugu wote walio pamoja nami, kwa makanisa ya Galatia; Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba, na kwa Bwana wetu Yesu Kristo; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu, ili atuokoe na dunia hii mbovu iliyopo sasa, kama alivyopenda Mungu, Baba yetu… Maana mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba nililitesa Kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu… Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake, alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake…” Gal 1:1.13.15-16.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Mtume Paulo alikuwa na ufahamu mkubwa wa Fumbo la Maisha ya Kristo Yesu. Katika mawazo yake, anapaa zaidi na kuwaonesha waamini jinsi ya kufikiri na kutenda, wanapokabiliana na matatizo na changamoto za mipasuko ya kiimani ndani ya jumuiya. Mwishoni mwa Waraka huu, anazungumzia kuhusu Sheria na Msalaba wa Kristo na wale wote ambao wamekuwa ni viumbe wapya kwani wanachukua mwilini mwao chapa ya Kristo Yesu! Kutahiriwa kadiri ya mila na desturi za Kiyahudi lilikuwa ni jambo muhimu na utambulisho wao. Ni katika muktadha huu, Paulo Mtume aliamua kuzama zaidi ili kuubainisha ukweli wa Injili na uhuru wa Wakristo kama sehemu muhimu sana ya utambulisho wao. Mtume Paulo katika ufafanuzi wake, hakubaki juu juu tu, bali aliamua kuzama ndani zaidi ili hatimaye, kupata suluhisho la kudumu. Mtume Paulo anasema: “Maana, sasa Je! Ni wanadamu ninaowashawishi, au Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza wanadamu, nisingekuwa mtumwa wa Kristo.” Gal 1:10.

Mtume Paulo anasikia ndani mwake umuhimu wa kuwakumbusha Wagalatia kwamba, kuhusu wito wake kwamba, unapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, ni mtume kweli kweli. Anawasilimua jinsi alivyotubu na kumwongokea Mungu baada ya kukutana mubashara na Kristo Yesu Mfufuka alipokuwa njiani kuelekea Dameski. Rej. Mdo 9:1-9. Mtume Paulo anawadadavulia kuhusu historia ya maisha yake ya hapo awali akisema: “Maana mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba naliliudhi kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu. Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu. Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake, alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake”. Gal 1: 13-14. Anakazia kuhusu kufuata mapokeo ya baba zake na kwamba, alisimamia sheria kwa nguvu zote. Anatambua kwamba, aliliudhi na kuliharibu Kanisa, lakini neema na huruma ya Mungu imemletea wongofu ambao sasa unafahamika na wengi.

Mtume Paulo anasema, “Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo; ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.” Gal 1:22-23. Hiki ni kielelezo cha toba na wongofu wa ndani, kiini na ukweli wa historia ya wito wake, sasa anatangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, huku akiwa ni mtu huru kabisa! Anakiri dhambi zake kutoka katika sakafu ya moyo wake na hivyo kujaliwa uhuru wa ndani kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Historia hii inaonesha mshangao mkubwa wa Paulo ambaye sasa ni Mtume wa Kristo Yesu! Lakini Mwenyezi Mungu, alimtenga tangu tumboni mwa mama yake, akamwita kwa neema yake, alipoona vema akamdhihirisha Mwanawe mpendwa Kristo Yesu ndani yake, ili awatangazie na kuwashuhudia Mataifa Habari Njema ya Wokovu. Mwenyezi Mungu anasema Baba Mtakatifu Francisko anamwita mtu kadiri ya hali na mazingira yake ambayo wakati mwingine, huwashangaza wanadamu. Hakuna jambo linalotendeka kwa bahati mbaya, bali kila kitu ni sehemu ya mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu, changamoto kwa waamini ni kutekeleza mapenzi ya Mungu na kutekeleza utume ambao Mwenyezi Mungu amemwandalia kila mtu.

Kwa njia ya neema na baraka zake, Mwenyezi Mungu anawaita waja wake, kumbe, ni vyema ikiwa kama watatambua neema ya Mungu inayotenda kazi ndani mwao, kiasi cha kuwaletea mabadiliko makubwa katika maisha, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kikristo kwa watu wa Mataifa. Neema ya Mungu ilete toba na wongofu wa ndani kwa wadhambi; ili waweze kutubu na kumwongokea Mungu, ili hatimaye, waweze kuona njia mpya ambao Mwenyezi Mungu amewaandalia waja wake!

Papa Katekesi

 

 

 

03 August 2021, 14:59