Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Agosti 2021: Kanisa linapyaishwa kwa maisha ya sala, upendo na huduma makini kwa watu wa Mungu Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Agosti 2021: Kanisa linapyaishwa kwa maisha ya sala, upendo na huduma makini kwa watu wa Mungu 

Nia za Papa Francisko Mwezi Agosti 2021: Kanisa Linasafiri!

Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa mwezi Agosti 2021 ni Kanisa liko safarini kuinjilisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu kama sehemu ya maisha, wito na utambulisho wake. Kanisa linapania kuinjilisha na wala si wongofu wa shuruti. Kanisa linaweza kupyaishwa kutoka katika undani wake, kwa kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha ya kila siku kwa sala, upendo na huduma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Lengo la utume wa Kanisa ni wokovu wa wanadamu unaopatikana kwa imani kwa Kristo na neema yake. Kwa hiyo, utume wa Kanisa, na wa kila mwanakanisa, unaelekea kabla ya yote kudhihirisha kwa maneno na matendo mbele ya ulimwengu ujumbe wa Kristo na kushirikisha neema yake. Utume huo hutekelezwa hasa kwa huduma ya Neno la Mungu na ya maadhimisho ya Sakramenti, huduma iliyowekwa kwa namna mahsusi kwa wakleri, na ambayo pia walei wanayo sehemu yao muhimu sana ya kutekeleza, ili wapate kuwa “watenda kazi pamoja na kweli” (3Yoh 8). Hasa katika hayo utume wa waamini walei na huduma ya kichungaji zinatimilizana. Walei Wanapata fursa nyingi sana za kuweza kuutimiza utume wa uinjilishaji na wa utakatifuzaji. Ushuhuda wenyewe wa maisha ya kikristo na ya matendo mema yaliyotimizwa kwa roho ya kimungu vina nguvu ya kuwavutia watu kwenye imani na kwa Mungu, kama anavyosema Bwana: “Hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni” (Mt 5:16). Rej. Utume wa Walei, 6. Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa mwezi Agosti 2021 ni Kanisa liko safarini kuinjilisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu kama sehemu ya maisha, wito na utambulisho wake. Kanisa linapania kuinjilisha na wala si wongofu wa shuruti. Kanisa linaweza kupyaishwa kutoka katika undani wake, kwa kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha ya kila siku.

Haya ni mageuzi yanayopaswa kuongozwa na Roho Mtakatifu, Zawadi ya Baba wa milele katika nyoyo za waamini. Roho Mtakatifu anawakumbusha waamini kile ambacho Kristo Yesu aliwafundisha waja wake, ili kuweza kukimwilisha katika uhalisia wa maisha. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuanza mchakato wa kulipyaisha Kanisa kwa kujitakatifuza kwanza wao wenyewe. Zoezi hili linafumbatwa katika mang’amuzi ya maisha ya sala, upendo na huduma makini kwa watu wa Mungu. Hii ni ndoto ya kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari, kwa kuwaendea jirani bila wongofu wa shuruti na kwamba, hii sehemu ya miundombinu ya uinjilishaji katika ulimwengu mamboleo! Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, Kanisa daima lina matatizo, changamoto na fursa mbalimbali kwa sababu, Kanisa ni hai na linaishi. Viumbe hai, katika safari yake hapa duniani, vinakumbana na changamoto nyingi. Ni wafu peke yao, ambao hawana tena changamoto za maisha! Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali na kuliombea Kanisa, ili liweze kupokea neema ya Roho Mtakatifu na nguvu ya kuweza kufanya mageuzi ndani mwake kwa mwanga wa Injili ya Kristo Yesu.

Padre Frederic Fornos, Mkurugenzi wa Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa anasema, hivi karibuni Kardinali Reinhard Marx, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Munich na Freising nchini Ujerumani alimwandikia Baba Mtakatifu Francisko barua na kutia nia ya kutaka kung’atuka kutoka madarakani iliyoandikwa tarehe 21 Mei 2021 na Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake ya tarehe 10 Juni 2021 akamjibu na kumtaka aendelee na utume wake wa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo kuu la Munich na Freising. Baba Mtakatifu anasema hiki ni kipindi muafaka kwa watu wa Mungu Jimbo kuu la Munich na Freising, kukaa chini na kuanza kutafakari na kupembua makosa yaliyojitokeza katika historia na maisha ya Kanisa; kutubu na kuongoka na hivyo kuanza utekelezaji wa sera na mikakati mipya kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa zima. Lengo ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu kwa ari na moyo mkuu, tayari kuchangia mchakato wa kuendelea kulipyaisha Kanisa la Kristo katika ujumla wake. Mama Kanisa anatambua na kukiri udhaifu wa watoto wake, uliopelekea kutumbukia katika kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo na kwamba, kila mwamini ajifunge kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, anapambana kufa na kupona ili kamwe nyanyaso za kijinsia zisirejee tena katika maisha na utume wa Kanisa.

Mama Kanisa anatambua udhaifu na mapungufu ya watoto wake. Katika maisha na utume wake, Kanisa limewahi kuomba msamaha kutokana na dhambi za watoto wake. Kanisa ni takatifu kwa sababu limeanzishwa na Kristo Yesu mwenyewe, lakini lina wadhambi ambao wanaelemewa na udhaifu wao. Katika nafasi zote hizi, Kanisa linatakiwa kufanya mageuzi makubwa! Lakini ikumbukwe kwamba, mageuzi yanaanza kutoka katika ngazi ya mtu mmoja mmoja na baadaye jamii nzima ya waamini kwa kumwachia Kristo Yesu kutenda kazi ndani mwao. Hapa kila mwamini anapaswa kuwajibika. Kristo Yesu alifanya mageuzi makubwa katika maisha na histroria ya binadamu kwa: Maisha na mafundisho yake lakini zaidi kwa njia ya Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko uletao uzima wa milele. Kardinali Reinhard Marx kwa upande wake, ilikuwa ni kung’atuka kutoka madarakani. Watu wa Mungu hawana budi kukiri kwamba, wamekosa na wametenda dhambi. Ni wakati wa kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kupokea na kuambata neema na baraka zake zinazoganga, kuponya na kuokoa.

Papa Nia Agosti
03 August 2021, 16:00