Kumbukumbu ya Mtakatifu Yohane Maria Vianney Msimamizi wa Maparoko duniani: Wito kuwaombea Maparoko na Mapadre wote ili wawe ni mashuhuda wa upendo, huruma na mshikamano. Kumbukumbu ya Mtakatifu Yohane Maria Vianney Msimamizi wa Maparoko duniani: Wito kuwaombea Maparoko na Mapadre wote ili wawe ni mashuhuda wa upendo, huruma na mshikamano. 

Mtakatifu Yohane Maria Vianney: Upendo, Huruma na Mshikamano

Papa anawaalika waamini kuwaombea Maparoko wao pamoja na Mapadre wao wote, ili waweze kuchota amana na utajiri kutoka katika maisha na utume wa Mtakatifu Yohane maria Vianney. Wajizatiti zaidi katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Mapadre wawe ni mashuhuda na vyombo vya: huruma, upendo, faraja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. SALA!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Mama Kanisa, tarehe 4 Agosti 2021 ameadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 162 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney, mfano bora wa kuigwa na mapadre wote duniani katika wema, upendo, ukarimu, sadaka na majitoleo yake kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 4 Agosti 2021 amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwakumbuka na kuwaombea Maparoko wao pamoja na Mapadre wao wote, ili waweze kuchota amana na utajiri kutoka katika maisha na utume wa Mtakatifu Yohane maria Vianney. Wajizatiti zaidi katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Mapadre wawe ni mashuhuda na vyombo vya: huruma, upendo, faraja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya Miaka 160 tangu Mtakatifu Yohane Maria Vianney alipofariki dunia, aliwaandikia Mapadre wote barua maalum ambamo alikazia mambo makuu yafuatayo: Kwanza kabisa aliwataka mapadre wanaendelee kuandika kurasa za maisha na utume wa Kipadre sehemu mbali mbali za dunia. Anapenda kuwashukuru na kuwatia moyo Mapadre wote wakitambua kwamba, wao kwa hakika ni marafiki wa Kristo Yesu katika maisha na utume wao. Baba Mtakatifu anasema, kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale, ameyaona mateso na mahangaiko ya watu wake, anasema haachi kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Mapadre, akiwakumbuka katika sala zake; anataka kuwafariji wote katika nyoyo zao, ili hatimaye, waweze kuimba ukuu na utukufu wa Mungu katika maisha yao.

Ushuhuda wa maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Maria Vianney uwe ni mfano bora wa sadaka na majitoleo ya maisha na utume wa Kipadre katika ulimwengu mamboleo. Mtakatifu Yohane Maria Vianney alizaliwa kunako tarehe 8 Mei 1786. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi kwa shida kubwa, alipewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 12 Agosti 1815. Akafariki dunia tarehe 4 agosti 1859 akiwa na umri wa miaka 73. Tarehe 8 Januari 1905 akatangazwa kuwa Mwenyeheri na Papa Pio X. Ilikuwa ni tarehe 31 Mei 1925 Papa Pio wa XI akamtangaza kuwa Mtakatifu na kunako mwaka 1929 akamtangaza kuwa ni Msimamizi wa Maparoko duniani. Ni Padre ambaye kwa muda wa miaka 40 alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia watu wake kwa Neno na Sakramenti za Kanisa; akajitakatifuza kwa: Neno la Mungu,  Sala, Toba na Wongofu wa ndani, uliofumbatwa katika maisha adili na unyenyekevu mkuu. Akajitahidi kuwaongoza watu wa Mungu katika hija ya maisha, kuelekea kwenye utakatifu na furaha ya maisha na uzima wa milele.

Mt. Vianney

 

04 August 2021, 14:47