Mshikamano wa Papa Francisko kwa waathirika wa majanga asilia nchini Venezuela mwezi Agosti 2021. Mshikamano wa Papa Francisko kwa waathirika wa majanga asilia nchini Venezuela mwezi Agosti 2021. 

Mshikamano wa Papa Kwa Waathirika wa Mafuriko Venezuela

Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya watu 54, 543 walikuwa wameathirika vibaya sana kiasi cha kuhitaji msaada wa kibinadamu. Maeneo yaliyoathirika vibaya zaidi ni pamoja na Merida, Tachira, Zulia Apure, Amazonas, Bolivar, Delta Amacuro, Monogas pamoja na Aragua. Papa Francisko ameguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu wa Mungu nchini Venezuela anawaombea!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Mvua kubwa iliyonyeesha hivi karibuni huku ikiambatana na maporomoko ya udongo huko Magharibi mwa Venezuela imepelekea watu zaidi ya 20 kupoteza maisha. Nyumba zaidi ya 1,200 zilibomolewa na watu zaidi 17 walikuwa hawajulikani mahali walipo! Miundombinu ya barabara iliharibiwa vibaya sana na kwamba, shughuli za kuokoa maisha ya watu zilikuwa zinakwamishwa kutokana na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na mgogoro wa kisiasa nchini Venezuela. Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya watu 54, 543 walikuwa wameathirika vibaya sana kiasi cha kuhitaji msaada wa kibinadamu. Maeneo yaliyoathirika vibaya zaidi ni pamoja na Merida, Tachira, Zulia Apure, Amazonas, Bolivar, Delta Amacuro, Monogas pamoja na Aragua.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 29 Agosti 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewakumbuka na kuwaombea wale wote waliofariki dunia kutokana na mafuriko pamoja na maporomoko ya ardhi huko nchini Venezuela. Wote hawa anawaombea huruma ya Mwenyezi Mungu ili waweze kupumzika kwa amani. Watu walioathirika waonje upendo na ukarimu kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa.

Maafa Venezuela
30 August 2021, 14:41