Mkutano wa X wa Familia Duniani utaadhimishwa mjini Roma kuanzia 22-26 Juni 2022. Kielelezo cha Arusi ya Kanisa kimechaguliwa kunogesha maadhimisho haya! Mkutano wa X wa Familia Duniani utaadhimishwa mjini Roma kuanzia 22-26 Juni 2022. Kielelezo cha Arusi ya Kanisa kimechaguliwa kunogesha maadhimisho haya! 

Siku ya Familia Duniani 2022: Kielelezo Arusi ya Kana ya Galilaya

Maaadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani mjini Roma, kuanzia tarehe 22 hadi 26 Juni, 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”, Arusi ya Kana ya Galilaya ndicho kielelezo kilichochaguliwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha sanjari na Jimbo kuu la Roma, ambalo litakuwa ni Mwenyeji wa maadhimisho haya! Injili ya Familia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” yalizinduliwa rasmi tarehe 19 Machi 2021 na yatahitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani mjini Roma, kuanzia hapo tarehe22 hadi 26 Juni, 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”. Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” unakwenda sanjari na maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu. Itakumbukwa kwamba, Mwaka wa Mtakatifu Yosefu ulizinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2020 na unatarajiwa kufungwa hapo tarehe 8 Desemba 2021. Huu ni wakati muafaka wa kufanya tafakari ya kina kuhusu Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”. Baba Mtakatifu Francisko anasema, furaha ya upendo inayopatikana katika familia ni furaha ya Kanisa pia. Bado waamini wengi wanataka kufunga ndoa takatifu kwa sababu ni tamko la Kikristo kuhusu familia ni Habari Njema kweli! Huu ni wakati muafaka wa kutafakari tunu msingi za kifamilia katika mwanga wa Neno la Mungu.

Ni muda wa kuyaangalia matukio mbalimbali ya maisha, utume na changamoto ambazo familia zinakabiliana nazo katika ulimwengu mamboleo. Waamini wanahimizwa kumtaza Kristo Yesu ili kutambua na kuendeleza wito wa ndoa na familia kwa kujikita zaidi katika nyaraka mbalimbali ambazo zimetolewa na Mama Kanisa kwa ajili ya familia, Sakramenti ya Ndoa na Malezi kwa watoto ndani ya familia. Baba Mtakatifu anawaalika wanandoa kukuza na kudumisha upendo unaobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo zao. Wanandoa wanahimizwa kuendelea kupyaisha upendo huu, ili kuzaa matunda yanayokusudiwa. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa Kanisa kusaidia mchakato wa kutangaza na kushuhidia Injili ya familia katika ulimwengu mamboleo. Kwa kuweka sera na mikakati ya kichungaji ili kuwaandaa wanandoa wapya na kuwasindikiza wanandoa wapya katika maisha na utume wao. Familia zinahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, zinajikita kikamilifu katika malezi na makuzi ya watoto wao: kiimani, kimaadili na kiutu! Familia iwe ni shule ya malezi na makuzi ya watoto wanaochota mifano bora kutoka kwa wazazi na walezi wao! Wazazi watambue dhamana ya kuwarithisha watoto imani, maadili, mila na desturi njema.

Baba Mtakatifu anahimiza umuhimu wa Kanisa kuwasindikiza wanandoa; kutambua changamoto na fursa zilizopo na kuwasaidia wanandoa kuchukuliana katika safari yao ya maisha ya ndoa na familia. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko anakazia huruma ya kichungaji kwa wanandoa, elimu ya maisha ya kiroho kuhusu ndoa na familia kama sehemu ya malezi na katekesi endelevu kwa watu wa ndoa! Yote haya yanafafanuliwa kwa kina na mapana kwenye Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”. Ni katika muktadha wa maaadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani mjini Roma, kuanzia tarehe 22 hadi 26 Juni, 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”, Arusi ya Kana ya Galilaya ndicho kielelezo kilichochaguliwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha sanjari na Jimbo kuu la Roma, ambalo litakuwa ni Mwenyeji wa maadhimisho haya! Mtakatifu Paulo Mtume na mwalimu wa Mataifa akitafakari kuhusu upya wa kidugu nyumbani anakaza kusema, “siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari za Kristo na Kanisa”. Ef 5:32.

Akiwa kwenye arusi ya Kana, mji wa Galilaya, Kristo Yesu alifanya muujiza wake wa kwanza, kielelezo kwamba, Mwenyezi Mungu amefunga ndoa na watu wake. Hiki ni kiini cha Habari Njema, ingawa wale waliokuwepo arusini, hawakutambua kwamba, kati yao, alikuwepo Mwana wa Mungu, ambaye kimsingi ndiye Bwana arusi. Muujiza wa arusi ya Kana ya Galilaya unafumbatwa kwa uwepo wa Kristo Yesu anayejifunua kati ya watu wake kama Bwana arusi, aliyetangazwa na kushuhudiwa na Manabii na kwamba, Yeye ndiye kiini cha Agano Jipya linalojikita katika upendo. Bikira Maria alipogundua kwamba, wanaarusi wanatindikiwa na divai, mara akamwendea Yesu na kumwambia kwamba, “hawana divai” na Yesu akatenda muujiza wake wa kwanza, kwa kugeuza maji kuwa divai. Maandiko Matakatifu yanaonesha kuwa, divai ni sehemu muhimu sana kwenye karamu ya Kimasiha, kwa sababu ni chemchemi ya furaha! Yesu anageuza Sheria ya Musa katika Injili ili kuwakirimia watu furaha ya kweli!

Baba Mtakatifu akielezea nafasi ya Bikira Maria katika muujiza huu, anasema kwamba, Bikira Maria aliwaambia wale watumishi: “Lo lote atakalowaambia, fanyeni”. Maneno haya ni amana na hazina kubwa ambayo Bikira Maria amewaachia wafuasi wa Kristo Yesu. Wale watumishi wakatii na kuyajaziliza maji hata juu na baadaye Yesu akawaamuru kuyateka na kumpelekea mkuu wa meza, hii ni alama ya Agano Jipya kati ya Kristo Yesu na Kanisa lake linalopaswa kuwa ni chombo cha huduma kwa ajili ya utume wake. Kumhudumia Kristo Yesu, maana yake ni kusikiliza kwa makini maneno yake na kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha. Hili ni ombi kutoka kwa Bikira Maria ambalo linakuwa sasa ni sehemu ya programu ya maisha ya Mkristo! Katika mahangaiko ya maisha na hali ya kukata tamaa, Baba Mtakatifu anawashauri waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumkimbilia Bikira Maria na kumwambia kwamba, “hawana divai” na Bikira Maria atamwendea Kristo Yesu na kumwambia!

Kumbe, sasa utakuwa ni wajibu wa waamini kutenda kadiri watakavyokuwa wameagizwa na Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kuchota maji kutoka kwenye mabalasi maana yake ni kujiaminisha kwa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa ili kumwezesha mwamini kupata neema katika maisha yake, ili hatimaye, kufurahia upya wa maisha kama alivyosikika mkuu wa meza akiisifia ile divai mpya. Kwa hakika, Kristo Yesu anaendelea kuwashangaza wafuasi wake kila kukicha! Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa aendelee kuwasaidia waamini kutenda kadiri ya maelekezo ya Yesu, ili hatimaye, kujifunua kwake na kumtambua katika maisha ya kila siku pamoja na alama za uwepo wake hai unaojenga na kuwaimarisha watu wake!

Wakati huo huo, Padre Ivan Rupnik, SJ. Aliyepewa dhamana ya kuchora picha ya Arusi ya Kana ya Galilaya kama kielelezo cha Maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani anasema kwa Wakristo familia ni kielelezo cha Sakramenti ya Ndoa, inayowashirikisha waamini upendo wa Kristo Yesu kwa Kanisa lake. Maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani kwa Mwaka 2022 yataadhimishwa kimataifa mjini Roma. Kwanza kutafanyika kongamano la familia na hatimaye, Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Matukio ya Roma yatahudhuriwa na wawakilishi kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu mahalia pamoja na vyama vya utume wa familia kimataifa. Lakini Maaskofu mahalia katika majimbo yao, nao wataadhimisha tukio hili muhimu katika maisha na utume wa Kanisa.

Siku ya Familia 2022
02 August 2021, 15:58