Kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu Jimbo kuu la Roma, tarehe 5 Agosti: Tafakari kuhusu Bikira Maria Afya ya Warumi. Kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu Jimbo kuu la Roma, tarehe 5 Agosti: Tafakari kuhusu Bikira Maria Afya ya Warumi. 

Kutabarukiwa kwa Kanisa Kuu la B. Maria Mkuu Roma; Afya ya Warumi

Kanisa hili ni chimbuko la utajiri na amana ya Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipofanyika mwili na kukaa kati ya waja wake. Kanisa hili pia linatunza masalia ya Sanamu ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani”, faraja ya wale wote wanaomkimbilia kwa imani na matumaini katika shida na mahangaiko yao ya ndani! Papa anawaalika waamini kumwendea B. Maria!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 5 Agosti anaadhimisha Kumbukumbu ya Kutabarukiwa kwa Kanisa la Bikira Maria Mkuu, lililoko mjini Roma. Hili ni Kanisa lililojengwa kwa heshima ya Mama wa Mungu mara baada ya Mtaguso wa Efeso, uliofanyika kunako mwaka 431, hapo Kanisa likamtangaza Bikira Maria kuwa ni "Theotokos" yaani Mama wa Mungu. Kanisa hili ni chimbuko la utajiri na amana ya Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipofanyika mwili na kukaa kati ya waja wake. Kanisa hili pia linatunza masalia ya Sanamu ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani”, faraja ya wale wote wanaomkimbilia kwa imani na matumaini katika shida na mahangaiko yao ya ndani! Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 4 Agosti 2021 katika salam zake, amewasihi waamini, kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Afya ya Warumi na hasa kwa namna ya pekee, tarehe 5 Agosti, Kanisa linapoadhimisha Kumbukumbu ya Kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma.

Huu ni mwaliko wa kumtafakari Bikira Maria, Afya ya Warumi!  Kanisa hili ni ushuhuda wa utenzi wa Bikira Maria, “Magnificat” aliposema “Kwa maana, tazama, tokea sasa vizazi vyote wataniita mbarikiwa kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu na jina lake ni takatifu.” Lk. 1:47. Ujumbe huu wa Bikira Maria umepokelewa na waamini wa vizazi vingi, wanaofika kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, ili kuadhimisha Sakramenti mbali mbali za Kanisa. Kanisa hili limekuwa ni Madhabahu ya kwanza yaliyojengwa kwa heshima ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa kwa nchi za Magharibi.

Madhabahu haya ni mahali ambapo waamini wanapata fursa ya kusikiliza Neno la Mungu, Kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na kujipatia neema ya toba na wongofu wa ndani, tayari kuandika upya historia ya maisha yao. Kwa wale waliopondeka na kuvunjika moyo, wanaweza kupata faraja kutoka kwa Bikira Maria, Afya ya Warumi, hasa katika kipindi hiki cha janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kama ilivyokuwa kwa Mtume Yohane, hata waamini wa nyakati hizi, wanaalikwa kumkaribisha Bikira Maria katika makazi yao, lakini zaidi nyoyoni mwao. Bikira Maria ni Mama na Mwalimu. Daima yuko tayari kuwasikiliza, kuwajibu na kuwafariji wale wote wanaomkimbilia huku bondeni kwenye machozi, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao.

Maria Afya Warumi
05 August 2021, 15:05