Kiini cha Katekesi za Baba Mtakatifu Francisko ni Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kiini cha Katekesi za Baba Mtakatifu Francisko ni Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! 

Kiini cha Katekesi za Papa Francisko: Kristo Yesu Mfufuka!

Hizi ni Katekesi ambazo zimetolewa na Baba Mtakatifu hata wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Kiini cha Katekesi hizi ni Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kuhubiri upya kunaweza kuwapa hamasa waamini, pamoja na wale waliolegea na wasioiishi imani yao, furaha mpya katika imani na uaminifu katika kazi ya uinjilishaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” uliochapishwa tarehe 24 Novemba 2013, anatoa kipaumbele cha kwanza kwa furaha ya Injili, kwa kuwaalika waamini kushirikisha furaha yao inayopata chimbuko kutoka katika huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu. Katika mwono huu, Kristo Yesu ni kiini cha Injili na kwamba, Kanisa linaalikwa kufanya mageuzi makubwa kama sehemu ya Uinjilishaji Mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Wosia huu ni ramani inayotoa dira na mwongozo thabiti wa shughuli za kichungaji zinazopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa siku za mbeleni kwa kuwa na mwono wa kinabii na mwelekeo chanya, licha ya vikwazo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa, ili Kristo Mfufuka aendelee kupeperusha bendera ya ushindi. Wosia huu wa kitume unachota utajiri wake kutoka katika mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu!

Baba Mtakatifu Francisko, akayasoma na kuyafanyia tafakari ya kina mapendekezo ya Mababa wa Sinodi na hatimaye kuyaweka kuwa ni sehemu ya ujumbe wake kwa Familia ya Mungu wakati huu inapojielekeza katika hija ya Uinjilishaji Mpya, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ndiye kiini cha Uinjilishaji na ndiye Mwinjilishaji Mkuu. Wakristo wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi, iliyoanzishwa na Kristo Yesu mwenyewe katika mazingira na tamaduni mpya za uinjilishaji. Mwono huu wa kimisionari ni mwaliko kwa Makanisa mahalia kuangalia changamoto na fursa zilizopo mintarafu tamaduni na hali halisi ya nchi husika. Baba Mtakatifu anatoa kigezo kwa ajili ya Kanisa la Kiulimwengu na kwa kila mdau wa uinjilishaji, ili kwa pamoja kuwa na mbinu mkakati shirikishi katika mchakato mzima wa uinjilishaji pasi na kujitenga kama kisiwa!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Yesu. Wale wanaoikubali zawadi yake ya ukombozi wanawekwa huru kuondokana na dhambi, uchungu, utupu wa ndani na upweke. Pamoja na Kristo, daima furaha inazaliwa upya.” EG 1. Baba Mtakatifu kama sehemu ya utekelezaji wa Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji katika Kanisa, yaani “Magisterium” amekwisha fanya katekesi 366 kama inavyojionesha kwenye Tovuti ya Vatican.va. Hizi ni Katekesi ambazo zimetolewa na Baba Mtakatifu hata wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Kiini cha Katekesi hizi ni Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kuhubiri upya kunaweza kuwapa hamasa waamini, pamoja na wale waliolegea na wasioiishi imani yao, furaha mpya katika imani na uaminifu katika kazi ya uinjilishaji.

Kiini cha ujumbe wa Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Mwenyezi Mungu anawapyaisha daima waja wake! Kristo Yesu ndiye Injili ya milele, Yeye ni yule yule, Mwanzo na Mwisho, nyakati zote ni zake na kwamba, Yeye ndiye chemchemi ya ujana wa Kanisa! Re. EG 11. Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi zake, amejikita zaidi katika tema zifuatazo: Kanuni ya Imani kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliotangazwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Sakramenti za Kanisa ambazo zinagusa nyakati muhimu za maisha ya mwamini na kwamba, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Sakramenti za Kanisa. Karama za Roho Mtakatifu na Kanisa kama Sakramenti ya Wokovu! Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Wakati wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, dhana ya huruma ya Mungu ilipewa msukumo wa pekee kabisa.

Baba Mtakatifu amekwisha kudadavua kuhusu Matumaini ya Kikristo, Ibada ya Misa Takatifu na Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara. Amechambua kwa kina na mapana kuhusu Amri Kumi za Mungu dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu. Alizungumzia sana kuhusu Sala ya Baba Yetu, kiini cha Mafundisho makuu ya Kristo Yesu kama zilivyo pia Heri za Mlimani. Aligusia umuhimu na udumifu wa sala katika maisha ya wamini. Wakati wa mlipuko wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, Baba Mtakatifu alianzisha Mzunguko mpya wa katekesi uliongozwa na kauli mbiu “Uponyaji wa Ulimwengu."Magonjwa yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Yaani: mwono tenge wa mwanadamu, uharibifu wa mazingira nyumba ya wote; Ubinafsi na uchoyo. Alikazia umuhimu wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu kama changamoto pevu, endelevu na fungamani ya kiimani.

Mzunguko wa Katekesi ya Waraka wa Mtume Paulo Kwa Wagalatia; Baba Mtakatifu Francisko amekazia kuhusu: Ushuhuda wa Mtume Paulo, Fumbo la Maisha ya Kristo Yesu, Wito wake kutoka kwa Mungu, Jinsi alivyolitesa Kanisa na jinsi ambavyo neema ya Mungu ilivyomwezesha kuwa ni Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Kwa muhtasari, Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia ni katekesi ya jinsi ambavyo Wakristo wanavyopaswa kuishi kikamilifu imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kwa nyakati mbalimbali, Baba Mtakatifu Francisko ametoa Katekesi maalum baada ya hija zake za kitume au nyakati za vipindi maalum vya Liturujia ya Kanisa. Baba Mtakatifu kuhusu Kanuni ya Imani anakazia umuhimu wa kutangaza na kushuhudia imani katika uhalisia wa maisha ya waamini. Sakramenti ni chemchemi za neema na baraka katika maisha ya waamini, kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa. Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu: kiroho na kimwili. Huruma ya Mungu iwe ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo kwa watu wa Mungu popote pale waliopo! Waamini wajifunze kusali na kujenga utamaduni wa udumifu katika sala, huku wakimwomba Mwenyezi Mungu aweze kutenda kadiri inavyompendeza!

Katekesi
17 August 2021, 15:02