Katekesi Waraka wa Mtume Paulo Kwa Wagalatia: Torati na Sheria

Papa Francisko: Kiini cha historia ya Wokovu ni Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Huyu ndiye ambaye Mtume Paulo amemtangaza na kumshuhudia, ili kuamsha imani kwa Mwana wa Mungu, kiini cha wokovu. Ni katika Kristo Yesu, waamini wanaweza kuwa na historia ya kabla na baada ya Yesu kama ilivyo hata katika Torati ambayo inapaswa kuheshimiwa kikamilifu

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Mzunguko wa Katekesi ya Waraka wa Mtume Paulo Kwa Wagalatia amekwisha kukazia kuhusu: Ushuhuda wa Mtume Paulo, Fumbo la Maisha ya Kristo Yesu, Wito wa Mtume Paulo kutoka kwa Mungu, jinsi alivyolitesa Kanisa na jinsi ambavyo neema ya Mungu ilivyomwezesha kuwa ni Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia ni katekesi ya jinsi ambavyo Wakristo wanavyopaswa kuishi kikamilifu imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Utume wa Kanisa ni kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu yaani “Kerygma”. Maadui wa Mtume Paulo walijikita zaidi katika mapokeo na Torati na kusahau upya ulioletwa na Injili ya Kristo Yesu! Hakuna Injili mpya isipokuwa ile iliyotangazwa na kushuhudiwa na Mitume wa Yesu! Mtume Paulo anapozungumzia kuhusu Sheria anagusia: Sheria ya Musa pamoja na Amri Kumi za Mungu, msingi wa Agano kati ya Mwenyezi Mungu na Waisraeli. Sehemu ifuatayo ya Maandiko Matakatifu inaelezea kwa muhtasari kuhusu Torati! “Na BWANA, Mungu wako, atakufanya uwe na wingi wa uheri katika kazi yote ya mkono wako, katika uzao wa tumbo lako, na katika uzao wa ng’ombe wako, na katika uzao wa nchi yako; kwa kuwa BWANA atafurahi tena juu yako kwa wema, kama alivyofurahi juu ya baba zako; ukiwa utaifuata sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa kuyashika maagizo yake, na amri zake zilizoandikwa katika chuo hiki cha torati; ukimwelekea BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote.” Kum 30. 9-10.

Umuhimu wa utangulizi wa Torati ndiyo kiini cha Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 18 Agosti 2021 aliyoitoa kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Paulo VI mjini Vatican. Katekesi hii, imenogeshwa na sehemu ya Maandiko Matakatifu isemayo: Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa. Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani. Lakini, iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi. Gal 3:23-25. Baba Mtakatifu katika katekesi yake, amegusia kuhusu historia ya wokovu inayopaswa kugawanywa katika sehemu kuu mbili, Sheria na Dhambi na hatimaye, Torati ipewe uzito wa pekee, kama watoto wa Mungu wanavyopswa kuishi kwa upendo katika Kristo Yesu Mfufuka! Mtume Paulo anaonesha fadhaa kwani Wagalatia wanakabiliwa na utumwa mpya kutokana na Torati na kwamba, neema inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu imewaletea uungwana na kwamba, Wakristo ni “watoto wa ahadi” wanaopaswa kuishi kadiri ya uhuru wa Kiinjili. Lakini, Torati kama utangulizi, ilikuwa na umuhimu wa pekee ambao unapaswa kulindwa na kuheshimiwa. Historia ya Wokovu pamoja na Historia ya Mtakatifu Paulo inapaswa kugawanywa katika sehemu kuu mbili. Kabla ya kumwamini Kristo Yesu na baada ya kupokea Neema.

Kiini cha historia hii ni Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Huyu ndiye ambaye Mtume Paulo amemtangaza na kumshuhudia, ili kuamsha imani kwa Mwana wa Mungu, kiini cha wokovu. Ni katika Kristo Yesu, waamini wanaweza kuwa na historia ya kabla na baada ya Yesu kama ilivyo hata katika Torati. Historia iliyotangulia iliwaweka watu chini ya Torati na ile iliyofuatia ilikuwa chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Kabla ya imani kwa Kristo Yesu, watu walikuwa ni watumwa wa Sheria na wamekuwa katika kipindi hiki chote kwa muda mrefu kwa sababu watu walikuwa wanaishi katika utumwa wa dhambi! Mtume Paulo katika Waraka wake kwa Warumi anafafanua kwa utaratibu mzuri kuhusu Sheria na Dhambi. Huu ni Waraka ulioandikwa miaka michache baada ya kuchapishwa Waraka kwa Wagalatia. Sheria ilimwezesha mwamini kutambua dhambi zake. Mkristo ni mtu huru aliyefunguliwa katika Torati. “Kwa maana tulipokuwa katika hali ya mwili, tamaa za dhambi, zilizokuwako kwa sababu ya torati, zilitenda kazi katika viungo vyetu hata mkaizalia mauti mazao. Bali sasa tumefunguliwa katika torati, tumeifia hali ile iliyotupinga, ili sisi tupate kutumika katika hali mpya ya roho, si katika hali ya zamani, ya andiko” Rum 7:5-6.

Mtume Paulo anaendelea kuandika akisema, uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati. Rej. 1Kor 15:56. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, sehemu hii inaonesha umuhimu wa utangulizi wa Torati kama sehemu ya katekesi makini katika ulimwengu mamboleo. Lakini katika Agano la Kale Torati ilichukuliwa kama kipimo cha nidhamu. Umuhimu wake ulitoweka pale ambapo kijana alifikia umri wa ukomavu! Torati ilikuwa na nafasi ya pekee katika Historia ya Waisraeli. Torati ni ushuhuda wa ukuu wa Mungu kwa watu wake. Torati iliwalinda, ikawafunda na kuwapatia nidhamu. Ikawasaidia kunyanyuka tena katika udhaifu wao. Ilitumika katika Kipindi cha mpito kutoka katika utumishi wa Torati na hatimaye, kuingia katika uhuru wa wana wa Mungu. Paulo Mtume anakaza kwa kusema, “Lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote; bali yu chini ya mawakili na watunzaji, hata wakati uliokwisha kuamriwa na baba. Kadhalika na sisi, tulipokuwa watoto, tulikuwa tukitumikishwa na kawaida za kwanza za dunia.” Gal 4:1-3. Hata baada ya kuamini katika Kristo Yesu, Amri Kumi za Mungu bado zinaendelea kuwa ni muhimu katika maisha ya waamini. Waamini wajitahidi kumfungulia Kristo Yesu nyoyo zao, ili aweze kukutana nao katika historia ya maisha yao!

Kwa ufupi kabisa, Torati ilikuwa na umuhimu wake kadiri ya ukomo, ili kutoa nafasi kwa mtu kukua na kukomaa, ili hatimaye, aweze kufanya maamuzi yanayozingatia uhuru wake. Mwamini anapofanikiwa kupata imani, Sheria inakoma na hivyo kutoa nafasi kwa mamlaka kuu zaidi. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha Katekesi yake kuhusu umuhimu wa utangulizi wa Torati kwa kuwataka waamini kutoa nafasi ya pekee, ili iweze kupata haki yake stahiki. Hii ni fursa kwa waamini kujiuliza ikiwa kama bado wanahitaji kuwa na Sheria au wanafahamu fika kwamba, wamepokea neema na sasa wamefanyika kuwa ni watoto wapendwa wa Mungu, hivyo wanapaswa kuishi katika upendo. Waamini wawe ni mashuhuda na vyombo vya imani, matumaini na furaha inayobubujika kutoka nyoyoni mwao baada ya kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao na kuwakirimia wokovu. Ni vyema Amri za Mungu zikawa ni dira na mwongozo katika maisha na kwamba wanahesabiwa haki kwa njia ya Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu!

Papa Francisko Torati
18 August 2021, 15:00

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >