Tafuta

Vatican News

Katekesi Kuhusu Waraka wa Mtume Paulo Kwa Wagalatia: Injili Ni Moja!

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake amejikita zaidi kuhusu Injili na utume wa Kanisa wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu yaani “Kerygma”. Maadui wa Mtume Paulo walijikita zaidi katika mapokeo na Torati na kusahau upya ulioletwa na Injili ya Kristo Yesu! Hakuna Injili mpya isipokuwa ile iliyotangazwa na Mitume wa Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko Kuhusu Waraka Wa Mtume Paulo kwa Wagalatia inakita mizizi yake katika tema msingi za maisha na utume wake kama Mwalimu wa mataifa. Hizi ni tema ambazo zinapamba uzuri wa Injili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anakazia toba na wongofu wa ndani; uhuru na neema ya kuishi kikamilifu kama mfuasi wa Kristo Yesu. Paulo Mtume, anakazia kuhusu mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, chemchemi ya maisha mapya yanayokita mizizi yake katika uhuru wa kweli, licha ya historia na matukio ya maisha yao ya kale. Waraka kwa Wagalatia ni mwangozo thabiti wa Habari Njema ya Wokovu pamoja na imani inayosimikwa kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu unatekelezwa katika fadhila ya unyenyekevu, umoja na udugu wa kibinadamu. Hiki ni kielelezo cha imani na utii, matunda ya kazi ya Roho Mtakatifu, anayeendelea kutenda kazi katika Kanisa la Kristo Yesu. Imani kutoka kwa Roho Mtakatifu ndani ya Kanisa inaganga, kuponya na kuokoa!

Mtakatifu Paulo anakazia kuhusu kufuata mapokeo ya baba zake na kwamba, alisimamia sheria kwa nguvu zake zote. Anatambua kwamba, aliliudhi na kuliharibu Kanisa, lakini neema na huruma ya Mungu imemletea wongofu ambao sasa unafahamika na wengi.  Mtume Paulo anasikia ndani mwake umuhimu wa kuwakumbusha Wagalatia kwamba, wito wake unapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, ni mtume kweli kweli. Mtume Paulo anawasimulia jinsi alivyotubu na kumwongokea Mungu baada ya kukutana mubashara na Kristo Yesu Mfufuka alipokuwa njiani kuelekea Dameski. Rej. Mdo 9:1-9. Mtume Paulo anasema, “Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo; ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.” Gal 1:22-23. Hiki ni kielelezo cha toba na wongofu wa ndani, kiini na ukweli wa historia ya wito wake, sasa anatangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, huku akiwa ni mtu huru kabisa! Hali ilivyo: Wagalatia wanashawishiwa kuiharibu Injili iliyo moja!

Mtakatifu Paulo Mtume anaandika akisema, “Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo. Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe.” Gal 1:6-8. Hii ni sehemu ya Maandiko Matakatifu iliyonegesha Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 4 Agosti 2021 kwenye Ukumbi wa Paulo VI ulioko mjini Vatican. Wazo kuu: Hakuna Injili nyingine isipokuwa iliyotangazwa na kushuhudiwa na Mitume wa Yesu. Baba Mtakatifu katika tafakari yake amejikita zaidi kuhusu Injili na utume wa Kanisa wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu yaani “Kerygma”. Maadui wa Mtume Paulo walijikita zaidi katika mapokeo na Torati na kusahau upya ulioletwa na Injili ya Kristo Yesu! Dhamana, wito na utume wa Mama Kanisa ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Hiki ni kipaumbele cha kwanza anachokitoa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Anadiriki kusema, ameitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu na wala si kubatiza!

“Paulo, mtumwa wa Kristo Yesu, aliyeitwa kuwa mtume, na kutengwa aihubiri Injili ya Mungu; ambayo Mungu amekwisha kuiahidi kwa kinywa cha manabii wake katika maandiko matakatifu; yaani, habari za Mwanawe, aliyezaliwa katika ukoo wa Daudi kwa jinsi ya mwili, na kudhihirishwa kwa uweza kuwa Mwana wa Mungu, kwa jinsi ya roho ya utakatifu, kwa ufufuo wa wafu, Yesu Kristo Bwana wetu; ambaye katika yeye tulipokea neema na utume ili mataifa yote wapate kujitiisha kwa imani, kwa ajili ya jina lake; ambao katika hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu Kristo; kwa wote walioko Rumi, wapendwao na Mungu, walioitwa kuwa watakatifu” Rum 1:1-7. Huu ndio utume wake. Mtakatifu Paulo, Mtume anatambua kwamba, ametengwa ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa moyo, akili na nguvu zake zote! Ndiyo maana anasikitishwa sana na tabia pamoja na mwelekeo ulioneshwa na Wagalatia, ambao kwa macho yake, inaonekana kana kwamba, wanaanza kufuata njia mbaya itakayowapoteza kabisa! Kipaumbele cha kwanza ni Injili ya Kristo! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, wakati Mtakatifu Paulo alipokuwa anaandika Waraka huu kwa Wagalatia Injili nne kama zinavyofahamika wakati huu, zilikuwa bado hazijaandikwa.

Mtume Paulo anatangaza, “Kerygma” kuhusu: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chemchemi ya wokovu. Hii ni Injili inayosimikwa katika ujumbe ufuatao: “Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale Thenashara…” 1 Kor 15:3-5. Injili ni utimilifu wa ahadi ya Mungu na chemchemi ya wokovu unaotolewa kwa watu wote bila ubaguzi. Anayepokea Injili ya Kristo anapatanishwa na Mungu na hivyo kuwa ni mwana mrithi wa maisha ya uzima wa milele! Mtume Paulo anashindwa kuwaelewa Wagalatia, kwa nini wanataka kukengeuka na hatimaye kupoteza njia ya Injili. Hao waamini wanaojidai kuinjilisha, hakuna upya wowote, kwa sababu maneno yao ni kikwazo cha kufikia uhuru wa kweli ambao wamejitwalia kwa njia ya imani. Hawa ni watu ambao bado walikuwa hawafahamu sana Torati ya Musa na ule mwamko wa kutaka kukumbatia Injili ya Kristo Yesu na Kanisa lake!

Mtume Paulo anawahakikishia Wagalatia kwamba, kuna Injili moja tu aliyoitangaza na kuishuhudia kama walivyokuwa wakifanya Mitume wengine, sehemu mbalimbali za dunia. Paulo Mtume anathibitisha wito wake kwa kusema, “Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo” Gal 1:11-12. Kumbe, Injili ya Kristo Yesu ilipaswa kupokelewa jinsi ilivyo bila ya kuchakachuliwa, kwa sababu ni chemchemi ya wokovu na wala si bidhaa inayouzwa dukani! Wamisionari wapya walikazia umuhimu wa kufuata kikamilifu mapokeo kutoka kwa mababa zao. Kwa upande wao, imani ya kweli ilisimikwa kwa waamini kufuata mapokeo! Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anakazia upya unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuipokea na kuimwilisha katika uhalisia wa maisha na vipaumbele vyao. Waamini wajibidishe kumpenda Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hata leo hii, kuna baadhi ya watu wanahubiri Injili kadiri wanavyojisikia, kiasi cha kuigeuza Injili kuwa kama chombo cha wanaharakati! Injili kama hii, kamwe haiwezi kuzaa matunda yanayokusudiwa na wala kuzamisha mizizi yake katika akili, nyoyo na maisha ya watu. Ikumbukwe kwamba, Injili ya Kristo Yesu na Kanisa ni zawadi kwa waamini wake na ufunuo uliotolewa na Kristo Yesu mwenyewe. Injili ni chemchemi ya maisha na uzima wa milele!

Papa Injili ya Kristo

 

04 August 2021, 15:53

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >