Papa Francisko: Waamini Jengeni Utamaduni wa kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika vipaumbele vya maisha yenu! Papa Francisko: Waamini Jengeni Utamaduni wa kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika vipaumbele vya maisha yenu! 

Papa Francisko: Jengeni Utamaduni wa Kusoma na Kutafakari Neno la Mungu

Injili ya Kristo ni Habari Njema ya Wokovu na nguvu inayoleta mabadiliko katika maisha ya waamini pamoja na vipaumbele vyao! Papa Francisko anawaalika waamini kujenga utamaduni wa kujisomea sehemu ya Maandiko Matakatifu kila siku, ili kuendelea kujichotea nguvu na neema kutoka katika Kisima cha Wokovu! Muhimu: Neno la Mungu dira na mwongozo wa maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Likizo ya Kipindi cha Kiangazi kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia kwa mwaka 2021 ni muda muafaka wa kujipatia nafasi ya kupumzika: kimwili na kisaikolojia, ili kujipatia tena nguvu za kuweza kusonga mbele kwa ari na mwamko mpya katika mapambano ya maisha ya kila siku. Ni nafasi muafaka ya kujenga, kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya dhati na Mwenyezi Mungu, kwa kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu, lakini zaidi kwa kuongozwa na Amri Kumi za Mungu bila shuruti! Injili ya Kristo ni Habari Njema ya Wokovu na nguvu inayoleta mabadiliko katika maisha ya waamini. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujenga utamaduni wa kujisomea na kutafakari sehemu ya Maandiko Matakatifu kila siku, ili kuendelea kujichotea nguvu na neema kutoka katika Kisima cha Wokovu! Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 4 Agosti 2021 mara baada ya Katekesi yake kuhusu Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia, kwamba, kuna Injili moja tu inayosimikwa katika: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu na wala hakuna Injili nyingine!

Likizo ni nafasi ya kutafakari kuhusu maisha, ili kubainisha ikiwa kama maisha yao yana alama ya uwepo angavu wa Mungu, ambaye kamwe hachoki kuwaongoza katika mapito ya maisha. Ni wakati muafaka wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa, shukrani, ukuu na uweza kutokana na kazi kubwa ya uumbaji. Mwanadamu katika ulimwengu mamboleo anayo kila sababu ya kulinda, kutunza na kuendeleza utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kwani mazingira bora na safi ni ufunuo wa: nguvu, wema, ukuu na utakatifu wa Mungu. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani: “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” ni dira na mwongozo makini katika mchakato wa wongofu wa kiikolojia. Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayokita mizizi yake katika misingi ya haki, amani, utu na heshima ya binadamu kwa sababu mazingira bora ni sehemu muhimu sana ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu ana matumaini makubwa kwamba, wanasiasa, wachumi na watunga sera, wataweza kujizatiti vyema zaidi, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa kazi kama utimilifu wa mtu binafsi, kijamii na kiikolojia.

Katika ulimwengu mamboleo kuna haja ya kutengeneza na kulinda fursa za ajira kwa kuzingatia matumizi bora ya ardhi mintarafu mapokeo, rasilimali muda na teknolojia rafiki. Bila fursa za ajira, familia na jamii katika ujumla wake, haitaweza kusonga mbele hata kidogo. Baba Mtakatifu pamoja na mambo mengine watakayotekeleza wakati huu wa likizo anawataka zaidi kuendeleza utamaduni, ari na moyo wa sala katika maisha yao. Wawe tayari kumwiga Kristo Yesu katika ujana wake, ulioshuhudia mwanga angavu, amani na maridhiano kati ya watu. Likizo kiwe ni kipindi cha kupyaisha na kunogesha maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili! Ni kipindi cha kukuza, kujenga na kudumisha urafiki; umoja na mafungamano ya kifamilia, ili kutangaza na kushuhudia kwamba, kwa hakika familia ni Kanisa dogo la nyumbani, linalojengwa na kuimarishwa na wanandoa wenyewe, katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku kwa kutambua kwamba, Kristo Bwana, yuko daima pamoja nao! Huu ni muda muafaka wa kufanya mazoezi na kumwilisha Injili ya huruma, upendo na msamaha katika maisha na vipaumbele vyao, tayari kumfuasa Kristo Yesu bila woga!

Likizo ni muda muafaka wa kukaa pamoja na wanafamilia wote pale inapowezekana, ili kukazia malezi bora na utu wema. Ni wakati wa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kusikilizana, kuheshimiana na kuthaminiana. Likizo ni muda wa kuratibu vyema rasilimali muda kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia nzima. Umefika wakati kwa wanandoa kuangaliana usoni bila kupepesa pepesa macho ili kujenga na kuimarisha upendo na urafiki wao wa dhati, daima wakimwachia nafasi Kristo Yesu ili aweze kuwafunda na kuwapyaisha katika maisha yao ya ndoa na familia. Mazoezi haya yasaidie kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu. Ni muda wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Likizo si wakati wa kumweka Mwenyezi Mungu pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya mwanadamu kwani hii, ni hatari kubwa sana! Waamini wajifunze kutoka kwa Bikira Maria, kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya huduma kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia.

Likizo
04 August 2021, 15:06