Papa Francisko tarehe 1 Julai 2021 Siku Maalum ya Kufunga, Kusali na Kutafakari Kuhusu Hatima ya Lebanon. Papa Francisko tarehe 1 Julai 2021 Siku Maalum ya Kufunga, Kusali na Kutafakari Kuhusu Hatima ya Lebanon. 

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Watu wa Mungu Nchini Lebanon

Nchi ya Lebanon ni amana na utajiri wa ustaarabu na tasaufi ambayo imekuwa ni chemchemi ya maridhiano na amani. Ni wito wa Lebanon kuwa ni nchi inayokita mizizi yake katika uzoefu wa amani, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Lebanon kuzamisha mizizi yao katika ndoto ya amani, tayari kung’arisha mwanga wa matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Usiku wa kinzani na migogoro utoweke; mapambazuko ya matumaini yaangaze, chuki na uhasama vikome, Lebanon irejee tena kuangaza nuru ya amani. Hii ndiyo sala ya Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Lebanon. Alhamisi, tarehe 1 Julai 2021 imekuwa ni Siku Maalum ya Sala, Kufunga na Kutafakari Kuhusu Hatima ya Lebanon na imenogeshwa na kauli mbiu: “Mwenyezi Mungu ana mawazo ya amani”. Sote kwa pamoja kwa ajili ya Lebanon. Yer 29: 11. Viongozi wa Makanisa ya Kikristo kutoka Lebanon asubuhi, walijiunga na Baba Mtakatifu Francisko ili kusalimiana na kutakiana heri. Baadaye walikwenda kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kusali mbele ya kaburi la Mtakatifu Petro, Mtume. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 1991, Mtakatifu Yohane Paulo II aliitisha Siku Maalum ya Sala kwa ajili ya Lebanon na baadaye mwaka 1995 yakafuatia maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki. Viongozi hawa kwa mwaka 2021 wamesali na kumwomba Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, awakirimie watoto wake wa Lebanon amani ya kudumu. Viongozi hawa wamewasha Mshumaa wa matumaini kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro, kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Lebanon.

Baadaye Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wageni wake wameshiriki kwenye vipindi vitatu vya majadiliano ya faragha. Baadaye, majira ya jioni, kwa pamoja wakaadhimisha Liturujia ya Kiekumene iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake kwa Watu wa Mungu nchini Lebanon alioutoa wakati wa Liturujia ya Kiekumene kwa ajili ya kuombea amani; ameomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu kwa niaba ya viongozi wa Makanisa walioshindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Nchi ya Lebanon ni amana na utajiri wa ustaarabu pamoja na tasaufi ambayo imekuwa ni chemchemi ya maridhiano na amani. Ni wito wa Lebanon kuwa ni nchi inayokita mizizi yake katika uzoefu wa amani, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Lebanon kuzamisha mizizi yao katika ndoto ya amani, tayari kung’arisha mwanga wa matumaini. Baba Mtakatifu ameanza ujumbe wake kwa kuwashukuru viongozi wote walioitikia wito wake wa kusali, kutafakari na kuombea amani Lebanon, sanjari na kufanya toba, ili kuomba msamaha na huruma ya Mungu pale waliposhindwa kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Injili ya Kristo. Lakini zaidi pale ambapo wameshindwa kutumia kikamilifu njia ya udugu wa kibinadamu, upatanisho na umoja kamili.

Kwa mapungufu yote haya wanamwomba Mwenyezi Mungu msamaha wa kweli. Anasema, kamwe wasichoke kumlilia Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala, ili aweze kuwakirimia waja wake amani ya kudumu. Nchi ya Lebanon ni amana na utajiri wa ustaarabu pamoja na tasaufi ambayo imekuwa ni chemchemi ya maridhiano na amani; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ujumbe unaosikika kwa wakati huu kutoka Mashariki ya Kati ni amani na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema Mwenyezi Mungu ana mawazo ya amani; anao mpango mkakati kwa ajili ya amani huko Lebanon na huu ni mradi unaopaswa kudumu katika amani, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi badala ya kumezwa na malimwengu. Wito wa Lebanon unapaswa kuwa ni nchi ya maridhiano na ya watu wengi, chemchemi ya udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Viongozi wa kisiasa waliko madarakani, wanapaswa kujizatiti zaidi kutafuta na kudumisha amani ya kweli na kamwe wasitafute masilahi yao binafsi.

Na kamwe watu wachache wasiendelee kufaidika kwa mateso na mahangaiko ya wananchi wa Lebanon na kwamba, watu wanataka kusikia ukweli wote kuhusu hatima ya maisha yao. Lebanon na Mashariki ya Kati katika ujumla wake, “lisiwe ni pango la wevi” kwa ajili ya msilahi ya watu wachache, wanaotaka faida na utajiri wa haraka haraka. Baba Mtakatifu anawakumbusha watu wa Mungu nchini Lebanon kwamba, Mwenyezi Mungu ana mawazo ya amani; anao mpango mkakati kwa ajili ya amani huko Lebanon. Umoja na tofauti zao msingi ziliwawezesha wahenga wa Lebanon kuishi kwa pamoja. Huu ni wakati wa kuzamisha mizizi kwa ajili ya ndoto ya amani, kwa kushirikiana na wengine. Wananchi wasikate tamaa bali waendelee kuwa na matumaini. Viongozi wa kisiasa kadiri ya wajibu wao watafute majibu ya matatizo na changamoto za kiuchumi kwa kujikita katika haki kama msingi wa amani. Wananchi wa diaspora kutoka Lebanon, wajifunge kibwewe kwa ajili ya kuwasaidia ndugu zao huko Lebanon. Jumuiya ya Kimataifa isaidie juhudi za kufufua uchumi nchini Lebanon; yote haya ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu anasema, ikiwa kama Lebanon inataka kujenga na kudumisha amani; wote wanapaswa kuungana na kushikamana ili kutenda katika umoja, upendo na huruma. Wakristo wanaitwa na kuchangamotishwa kuwa ni wapanzi wa amani na wajenzi wa udugu wa kibinadamu, kwa kuwajibika kikamilifu sanjari na kuendelea kuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi inayosimikwa katika njia ya amani. Majadiliano ya kidini na kiekumene yaimarishe mchakato wa umoja na mshikamano, tayari kufanya kazi kwa pamoja kama ndugu! Katika amani hakuna mshindi wala anayeshindwa. Ni wakati wa kunogesha majadiliano, kukuza na kudumisha elimu na mshikamano wa kweli. Katika pazia la usiku wa giza nene, kuna mapambazuko ya matumaini kama walivyoonesha vijana waliowakabidhi viongozi wa kidini mishumaa inayowaka, kielelezo cha matumaini kwa sasa na kwa siku zijazo. Katika mchakato wa kufanya maamuzi, viongozi watambue na kukumbuka kwamba, watu wanataka kuona mwanga wa matumaini ukiwashwa katika safari ya maisha yao. Viongozi waongozwe na mang’amuzi yanayobubujika kutoka katika dhamiri nyofu, ili kuwashirikisha watu wa Mungu matumaini mapya.

Wanawake wathaminiwe na kushirikishwa katika vikao vyote vinavyotoa maamuzi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Lebanon. Katika kipindi hiki cha kinzani, migogoro na mipasuko ya kijamii, changamoto kubwa ni wote kushikamana na kuungana ili kuwa ni kitu kimoja. Kwa njia hii wataweza kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi; ili kuendeleza nia njema, ili hatimaye, kuwasha mwanga wa matumaini pale penye giza. Mwisho mwa ujumbe wake kwa watu wa Mungu nchini Lebanon, Baba Mtakatifu amewaaminisha wote chini ya ulinzi na tunza ya Kristo Yesu, Mfalme wa amani, ili awakirimie huruma na matumaini! Usiku wa kinzani na migogoro utoweke; mapambazuko ya matumaini yaangaze, chuki na uhasama vikome, Lebanon irejee tena kuangaza nuru ya amani.

Amani Lebanon

 

 

 

02 July 2021, 15:19