Papa Francisko: Wazee na vijana kwa pamoja ni ufunuo wa sura pendevu ya Mama Kanisa katika ulimwengu mamboleo! Papa Francisko: Wazee na vijana kwa pamoja ni ufunuo wa sura pendevu ya Mama Kanisa katika ulimwengu mamboleo! 

Papa: Vijana na Wazee Ni Ufunuo wa Sura Pendevu ya Mama Kanisa!

Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza wazee pamoja na wajukuu wao, ambao kwa pamoja wameshuhudia ile sura pendelevu ya Kanisa, inayoonesha agano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu aliwaalika vijana kuadhimisha siku hii kwa kuwatembelea na kuwasalimia wazee, lakini zaidi wale ambao wako pweke. Wote kwa pamoja wadumishe majadiliano na umoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Siku ya Wazee na Wajukuu Duniani iliyoadhimishwa kwa mara ya kwanza katika historia, maisha na utume wa Kanisa, Jumapili tarehe 25 Julai 2021 imekuwa ni fursa kwa wazee na wajukuu kudemka, ili kumshukuru Mungu kwani maisha yataka matao! Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya umenogeshwa na kauli mbiu: “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote” Mt 28:20. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake amegusia kuhusu: Upweke hasi, janga la UVIKO-19; faraja kutoka kwa vijana na kwamba, Mwenyezi Mungu daima yuko pamoja na waja wake. Waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema. Wito wa wazee duniani ni kulinda mapokeo, amana na utajiri wa jamii husika! Baba Mtakatifu mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aliwapongeza wazee pamoja na wajukuu wao, ambao kwa pamoja wameshuhudia ile sura pendelevu ya Kanisa, inayoonesha agano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu aliwaalika vijana kuadhimisha siku hii kwa kuwatembelea na kuwasalimia wazee, lakini zaidi wale ambao wako pweke, ili kuwashirikisha ujumbe wa Baba Mtakatifu maalum kwa maadhimisho haya unaoongozwa na kauli mbiu “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote” Mt 28:20.

Baba Mtakatifu amewaombea wazee wote, ili jamii iweze kutambua umuhimu wa watu hawa hasa katika ulimwengu wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Vijana na wazee wanahitajiana na kukamilishana katika hija ya maisha yao hapa duniani. Kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni unaowakutanisha vijana na wazee, ili kukoleza moyo wa majadiliano. Bila mchakato wa majadiliano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya, maisha na historia ya mwanadamu vitagota mwamba na maisha hayataweza kusonga mbele hata kidogo! Majadiliano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya ni changamoto katika ulimwengu mamboleo. Wazee wanayo haki ya kuota ndoto, huku wakiwaangalia vijana. Na vijana kwa upande wao, wanayo haki na ujasiri wa kinabii, huku wakichota hekima na busara kutoka kwa wazee. Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee kabisa, anawaalika wazee na vijana wa kizazi kipya kujenga utamaduni wa kukutana na kuzungumza kwa pamoja, mwelekeo huu utakuwa ni wa manufaa kwa makundi yote mawili!

Itakumbukwa kwamba, Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, imeongozwa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilishaji mpya. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yaliyosomwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, amekazia mambo makuu matatu: kuona, kushirikishana na kuhifadhi. Mbele ya Mwenyezi Mungu, kila mtu anayo nafasi na thamani ya pekee na wala hakuna mkutano mkuu. Kristo Yesu analo jicho la tafakuri linaloweza kuzama katika undani wa maisha ya mwanadamu. Leo hii kuna haja ya kujenga mahusiano na mafungamano mapya kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee, ili kushirikishana amana na utajiri wa maisha, ili waweze kuota ndoto ya pamoja, kwa kuvuka kinzani na mipasuko kati ya kizazi na kizazi, tayari kujiandaa kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Bila ya mwelekeo huu mpya wa maisha, matamanio hayo halali yatakufa kwa baa la njaa kutokana na kuongezeka kwa upweke hasi; uchoyo na ubinafsi sanjari na nguvu za ubaguzi na utengano. Katika ulimwengu mamboleo asiwepo mtu awaye yote anayetelekezwa au kutwezwa. Ni wakati wa kusimama kidete kukusanya, kutunza na kuhudumia kwa upendo. Wazee ni watu wanaopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na jamii kwani ni hazina, amana na utajiri mkubwa, kwa sababu ndani mwao wanatunza kumbukumbu! Bila mizizi ya kumbukumbu hii, mwanadamu si mali kitu! Ni wajibu wa jamii kulinda maisha ya wazee, kwa kuwarahisishia matatizo na changamoto za maisha. Ni wakati wa kusikiliza, kujibu na kuwatekelezea mahitaji yao msingi, ili kamwe wasielemewe na upweke hasi.

Papa Wazee Na Vijana

 

26 July 2021, 14:37