Tafuta

Yesu Anakataliwa Kwao: Maamuzi Mbele! Kashfa ya Umwilisho!

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwa ufupi kwamba, kukataliwa kwa Kristo Yesu na watu wa nchini mwake, ni kushindwa kutambua undani wa maisha na utume wake; ni sababu ya mazoea na maamuzi mbele, lakini kubwa zaidi ni kashfa ya Fumbo la Umwilisho kwa kushindwa kumtambua Mungu katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku! Mungu ambaye amejitwalia hali ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mama Kanisa anasadiki na kufundisha: “Kwa Bwana mmoja Yesu Kristo, Mwana wa pekee wa Mungu. Aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli. Aliyezaliwa bila kuumbwa, wenye umungu mmoja na Baba; ambaye vitu vyote vimeumbwa naye. Ameshuka kutoka mbinguni kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu. Akapata mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake yeye Bikira Maria; akawa mwanadamu”. Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili ya 14 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa inasimulia jinsi Yesu alivyofika nchi ya kwao akifuatana na wanafunzi wake na siku ya sabato alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema: “Huyu ameyapata wapi haya? Na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake? Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na dada zake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake. Yesu akawaambia, Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake. Wala hakuweza kufanya mwujiza wowote huko, isipokuwa aliweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache, akawaponya. Akastaajabu kwa sababu ya kutoamini kwao.” Mk 1:1-6.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 4 Julai 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amefanya tafakari ya kina kuhusu sehemu hii ya Injili. Baba Mtakatifu anasema kwa ufupi kwamba, kukataliwa kwa Kristo Yesu na watu wa nchini mwake, ni kushindwa kutambua undani wake; ni sababu ya mazoea na maamuzi mbele, lakini kubwa zaidi ni kashfa ya Fumbo la Umwilisho kwa kushindwa kumtambua Mungu katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku! Kristo Yesu baada ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwenye vijiji vya Galilaya anakwenda mjini Nazareti, mahali alipolelewa na kukulia chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu na Bikira Maria. Alipokuwa anafundisha kwenye sinagogi, watu wengi wakajikwaa kwake kutokana na mafundisho yake. Kristo Yesu anasikitika kutokana na kutoamini kwao kiasi cha kusema; “Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake.”

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwa kusema kwamba, watu wa Nazareti walidhani kwamba, wanamfahamu fika Kristo Yesu, lakini kwa bahati mbaya sana, ufahamu wao ulikuwa ni wajuu juu tu bila kuzama katika undani wa maisha na utume wa Kristo Yesu. Matokeo yake, wakajikuta wanakosa imani kwake, kwa kuelemewa na tabia ya mazoea na maamuzi mbele kwa sababu ya miaka thelathini waliyomwona Yesu akiwa kati yao, kiasi cha kutupilia mbali upya wa maisha uliokuwa unabubujika kutoka kwa Kristo Yesu! Kukosa, imani, mazoea na maamuzi mbele ni hatari sana kwa maisha ya mwamini kwani hiki ni kikwazo kikubwa cha mabadiliko na ukomavu wa ndani. Hata waamini katika ulimwengu mamboleo wanaweza kukumbwa na mkasa huu kwa kudhani kwamba, wanamfahamu Kristo Yesu na hivyo hawana sababu ya kujibidiisha zaidi ili waweze kumfahamu na matokeo yake ni kuendelea kurudia yale mambo “kiduchu” wanayofahamu kumhusu Kristo Yesu. Changamoto kwa waamini ni kujiweka tayari kupokea upya na mshangao wa maisha unaoletwa na Mwenyezi Mungu. Bila ya mwelekeo huu, imani inakuwa ni “litania ya wachovu” kiasi kwamba, taratibu itazimika na kutoweka kama umande wa alfajiri.

Watu nchini mwake walishindwa kumtambua na kumwamini Kristo Yesu, kwa sababu hawakukubali kupokea Kashfa ya Fumbo la Umwilisho, kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, kujifunua katika udogo wa mwili wa mwanadamu. Katika udogo na unyenyekevu huu, Kristo Yesu akawa ni Seremala na Mwana wa Seremala; Umungu wake ukafichwa katika Ubinadamu. Kristo Yesu akawa ni ufunuo wa Sura na sauti ya Mungu; na kutenda yote kama binadamu wengine isipokuwa hakuwa na dhambi. Kashfa ya Fumbo la Umwilisho ikajionesha katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Kwa maneno mengine, huu ni ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya kila siku na hivyo kuwaachia watu wakiwa wameshikwa na bumbuwazi! Watu wanashangaa kwa kukutana na Kristo Yesu katika maisha na vipaumbele vyao na wala si jambo la mazoea! Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu ni Mungu ambaye amejifunua katika hali ya upole, unyenyekevu pamoja na kujificha na anaendelea kuwa ni jirani mwema katika uhalisia wa maisha ya kila siku.

Waamini wanapewa angalisho kuwa makini sana, vinginevyo wanaweza kujikuta wakiwa wanashindwa kumtambua Kristo Yesu anapowapitia katika uhalisia wa maisha yao, kiasi cha kuzama na kutopea katika kashfa ya Fumbo la Umwilisho! Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa alipenda kusema kwamba, anamwogopa Mwenyezi Mungu na Bwana anapopita, kwa sababu alichelea kwamba, atashindwa kumtambua anapopita! “Timeo Dominum transeuntem” kwa sababu anapopita, pengine watu wakaona kuwa ni kashfa. Hili ni jambo ambalo waamini wanapaswa kulitafakari katika undani wa maisha yao! Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Bikira Maria ambaye alikubali na kupokea ufunuo wa Mungu katika uhalisia wa maisha ya kila siku, ili hata wao waweze kuwa na macho na nyoyo huru ambazo hazina maamuzi mbele kutokana na mshangao wa Mungu, kwa uwepo wake mwanana katika hali ya unyenyekevu sanjari na kujificha katika uhalisia wa maisha ya kila siku!

Kashfa ya Umwilisho

 

04 July 2021, 15:08

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >