Tafuta

Vatican News

Papa Francisko Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa: Upendo na Faraja

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 11 Julai 2021 akiwa kwenye dirisha la Hospitali ya Gemelli mjini Roma, amekazia kuhusu Sakramenti ya Mpako Mtakatifu na huduma makini kwa wagonjwa kama njia ya kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya Hukumu ya Mwisho. Rej. Mt. 25. Kila mtu anahitaji mafuta ya faraja, upendo na huduma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema, Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa inaweza kutolewa kwa mwamini aanzapo kuwa katika hatari ya kufa kwa sababu ya ugonjwa au uzee. Inafaa kupokea Mpako Mtakatifu wa Wagonjwa kabla ya kupata operesheni ya hatari. Ni sawa pia kwa wazee ambao udhaifu wao unazidi kujitokeza. Matunda ya adhimisho la Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa: Mosi ni kipaji cha pekee cha Roho Mtakatifu. Neema ya kwanza ya Sakramenti hii ni neema ya nguvu, amani na ujasiri ili kushinda magumu yatokanayo na ugonjwa wa hatari au udhaifu wa uzee. Neema hii ni paji la Roho Mtakatifu anayeamsha matumaini na imani kwa Mwenyezi Mungu dhidi ya jaribu la kukata tamaa na hofu ya kifo. Hii ni neema ya faraja ya roho na mwili pamoja na msamaha wa dhambi. Kwa neema ya Sakramenti hii, mgonjwa hupata nguvu na paji la kujiunga kwa ndani zaidi na mateso ya Kristo Yesu na hivyo kutakaswa na hatimaye, kushiriki katika kazi ya wokovu inayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu.

Wagonjwa wanaopokea Sakramenti hii wanajiunga kwa hiari na mateso na kifo cha Kristo Yesu na hivyo kuchangia kulifaidia Taifa la Mungu. Mama Kanisa katika ushirika wa watakatifu wake, huomba kwa manufaa ya wagonjwa na mgonjwa kwa upande wake, huchangia utakaso wa Kanisa na mema ya watu wote wa Mungu wanaoteseka ambao kwa ajili yao Mama Kanisa anateseka na kujitoa kwa Mungu Baba kwa njia ya Kristo Yesu. Mpako wa wagonjwa unakamilisha kufananishwa kwa waamini na kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu kama ilivyo pia katika Sakramenti ya Ubatizo. Kimsingi Mpako wa wagonjwa hukamilisha mipako mitakatifu iliyotia alama yote ya Kikristo yaani: muhuri wa maisha mapya; mapambano ya maisha ya Kikristo na Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa huimarisha mwisho wa maisha ya mwamini hapa duniani, kama ngome thabiti kwa ajili ya mapambano ya mwisho, kabla ya kuingia katika nyumba ya Baba wa milele! Rej. KKK 1514 – 1532.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 11 Julai 2021 akiwa kwenye dirisha la Hospitali ya Gemelli mjini Roma, ametafakari kuhusu Sakramenti ya Mpako Mtakatifu na huduma makini kwa wagonjwa kama njia ya kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya Hukumu ya Mwisho. Rej. Mt. 25 Baba Mtakatifu Francisko ameonesha furaha kubwa kutoka moyoni kwa Mwenyezi Mungu aliyemjalia nguvu na uwezo wa kuendeleza utume wake wa kutafakari na kusali Sala ya Malaika wa Bwana akiwa kwenye Hospitali ya Gemelli mjini Roma ambako amelazwa na kufanyia operesheni kubwa hapo tarehe 4 Julai 2021. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru watu wote wa Mungu kwa sala na sadaka zao, ambazo zimekuwa ni ushuhuda wa uwepo wao wa karibu katika kipindi hiki cha ugonjwa. Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XV ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa na kwa namna ya pekee, Injili inamwonesha Kristo Yesu akiwatuma Mitume thenashara, wawili wawili kwenda kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kutoa pepo wachafu na kuwapaka mafuta wagonjwa, ili kuwaganga, kuwaponya na kuwafariji. Rej. Mk 6: 13.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Mafuta” yanayozungumziwa hapa ni Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa inayotoa faraja kiroho na kimwili. Mpako Mtakatifu ni kielelezo cha sanaa ya kusikiliza kwa makini; uwepo na ukaribu kwa mgonjwa, kwa hali na mawazo; kwa huruma na upendo kwa wale wanaowahudumia wagonjwa. Mpako Mtakatifu ni kielelezo cha faraja inayomfanya mgonjwa walau kujisikia nafuu katika shida na mahangaiko yake. Baba Mtakatifu kwa kuzingatia uzoefu wake kwa sasa anasema, kila mtu anahitaji “Mafuta ya faraja” kama siyo leo, basi ni kesho. Mafuta ya faraja ni zawadi inayoweza kutolewa na kila mtu katika hija ya maisha yake hapa duniani kwa njia ya kuwatembelea wagonjwa, kuwapigia walau simu kuwajulia hali zao; kwa kuwasaidia kwa hali na mali wale wanaoteseka na kuhangaika katika maisha yao!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, katika kipindi hiki ambacho amelazwa Hospitalini Gemelli, ameshuhudia mwenyewe umuhimu wa huduma bora ya afya, inayoweza kuwafikia na wote kama ilivyo kwa Italia na nchi nyingine duniani. Huu ni mfumo wa huduma ya afya unaowahakikishia watu wote huduma bora ya afya inayotolewa kwa watu wote. Baba Mtakatifu anatoa angalisho kwa watu wa Mungu nchini Italia, kamwe wasipoteze “kito hiki cha thamani” na badala yake ni kuulinda mfumo wa huduma bora ya afya. Ni katika muktadha huu, kila mtu anapaswa kuwajibika barabara kwani ufanisi wake ni matokeo ya mchango wa kila mtu! Kwa bahati mbaya sana kwa kwa baadhi ya Taasisi za Kanisa zinazomiliki na kuendesha huduma katika sekta ya afya, zinapokabiliwa na hali ngumu ya uchumi, jambo la kwanza kufikiriwa ni kuuza hospitali hizi. Lakini ikumbukwe kwamba, utume wa Kanisa ni huduma makini kwa wagonjwa na wala si rasilimali fedha ingawa ina umuhimu wake.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwashukuru na kuwatia shime madaktari, wauguzi pamoja na wafanyakazi wote katika sekta ya afya. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwakumbuka na kuwaombea wagonjwa, lakini zaidi, wale ambao wako katika hali tete zaidi. Kuna maswali ambayo hayana majibu ya mkato hasa kuhusu mateso na mahangaiko ya watoto wadogo. Basi asiwepo mgonjwa anayebaki katika upweke hasi, kiasi cha kujikatia tamaa! Kila mgonjwa apate “Mpako Mtakatifu” wa kusikilizwa, kupendwa, ujirani mwema na huduma makini. Baba Mtakatifu anayaomba yote haya kwa njia ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa na Afya ya Wagonjwa!

Mpako wa Wagonjwa
11 July 2021, 15:04

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >