Waamini na watu wenye mapenzi mema kutoka sehemu mbalimbali za dunia wanaendelea kusali kwa ajili ya Papa Francisko ambaye tangu tarehe 4 Julai 2021 amelazwa Hospitalini. Waamini na watu wenye mapenzi mema kutoka sehemu mbalimbali za dunia wanaendelea kusali kwa ajili ya Papa Francisko ambaye tangu tarehe 4 Julai 2021 amelazwa Hospitalini. 

Papa Francisko Ni Mgonjwa: Sala na Matashi Mema Toka Kwa Waamini

Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alionesha upendo wa dhati kwa wagonjwa kiasi hata cha kuliachia Kanisa dhamana na wajibu wa kuwaganga na kuwatibu wagonjwa. Upendo huo umekuwa ni chemchemi ya juhudi zisizochoka kwa ajili ya kuwafariji wagonjwa. Rais Sergio Mattarella, Waamini wa Jimbo Kuu la Roma na watu wenye mapenzi mema wanasali kwa ajili ya Papa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Huruma ya Kristo Yesu kwa wagonjwa na kazi zake nyingi za kuponya wagonjwa wa kila aina ni ishara inayong’aa kwamba Mwenyezi Mungu amewajia watu wake na kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia. Yesu aliwaponya wagonjwa na kusamehe dhambi, kielelezo kwamba, amekuja kumkomboa mtu mzima: kiroho na kimwili. Kristo Yesu ni mganga wa kweli ambaye wagonjwa wanamhitaji. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alionesha upendo wa dhati kwa wagonjwa kiasi hata cha kuliachia Kanisa dhamana na wajibu wa kuwaganga na kuwatibu wagonjwa. Upendo huo umekuwa ni chemchemi ya juhudi zisizochoka kwa ajili ya kuwafariji wagonjwa. Jambo la msingi kwa wagonjwa wenyewe ni kuwa na imani thabiti ili kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, Kristo Yesu aendelee kuwagusa, kuwaponya na kuwatakasa. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, Kristo Yesu ameyapa mateso maana mpya: kwa kuwafananisha waamini sanjari na kuwaunganisha na Kristo Yesu katika mateso yake yanayoleta ukombozi.

Kwa hakika Yesu ni “Mungu anayeokoa”. Pozeni wagonjwa ni utume ambao Kanisa limeupokea kutoka kwa Kristo Yesu na linajibidiisha kuutekeleza: kwa kuwatunza wagonjwa na kusali kwa ajili yao. Mama Kanisa anasadiki katika uwepo unaohuisha wa Kristo mganga wa roho na miili. Huwepo huu hutenda kazi kwa namna ya pekee kwa njia ya Sakramenti na hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, mkate uletao uzima wa milele, na ambao Mtakatifu Paulo, Mtume hudokeza uhusiano wake na afya ya mwili! Rej. KKK 1503 – 1510. Ni katika muktadha huu, familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma inapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala kwa Baba Mtakatifu Francisko wakati huu, anapoendelea na matibabu yake kwenye Hospitali ya Gemelli iliyoko mjini Roma. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanaendelea kuungana kwa njia ya sala, kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kumkirimia neema, baraka na uponyaji, Baba Mtakatifu Francisko. Watu wote wa Mungu, Jimbo kuu la Roma, wanamwombea Baba Mtakatifu Francisko aweze kupona haraka na kurejea katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Wakati huo huo, Rais Sergio Mattarella wa Italia, wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi nchini Ufaransa, Jumapili tarehe 4 Julai 2021 amemtumia Baba Mtakatifu Francisko salam na matashi mema, akimwombea kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kupona haraka. Amesema, salam na matashi mema amemtumia kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Italia. Waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema, sehemu mbalimbali za dunia, baada ya taarifa ya kulazwa na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko kufanyiwa upasuaji mkubwa, wameendelea kusali na kumwombea, kwa kumweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Afya ya Wagonjwa, ili aweze kumwombea kwa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu na hatimaye, apate kupona kadiri ya mapenzi ya Mungu. Sala kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko: Ee Bwana Yesu Kristo, ulishiriki ubinadamu wetu kwa hiari yako upate kuwaponya wagonjwa na kuwaokoa wanadamu. Sikiliza kwa huruma sala zetu, umjalie afya ya mwili na roho Baba Mtakatifu Francisko. Mfariji kwa kinga yako, mpe nafuu kwa nguvu yako. Msaidie atumaini kuokoka kwa njia ya mateso, kama ulivyotufundisha kutumaini hapo ulipoteswa kwa ajili yako. Utujalie sisi sote amani na furaha zote za ufalme wako huko unakoishi daima na milele. Amina. Unaweza kuwashirikisha pia jirani zako!

Sala kwa Wagonjwa
05 July 2021, 15:00