Papa Francisko asema Michezo ya Olimpiki ya Tokyo Japani 2020-2021 ni kielelezo cha matumaini, alama ya udugu wa kibinadamu na afya bora! Papa Francisko asema Michezo ya Olimpiki ya Tokyo Japani 2020-2021 ni kielelezo cha matumaini, alama ya udugu wa kibinadamu na afya bora! 

Papa: Michezo ya Olimpiki Tokyo 2020: Matumaini, Udugu na Afya!

Baba Mtakatifu anasema, mashindano ya Michezo ya Olimpiki ya Tokyo, Japan 2020-2021 ni kielelezo cha matumaini, alama ya udugu wa kibinadamu na kielelezo makini cha afya bora! Amewaombea wadau wote baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa mapendo, ili aweze kuwabariki wote wanaoshiriki katika Sherehe hii kubwa ya michezo. Michezo kwa Afya! Yaani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mashindano ya Michezo ya Olimpiki ya Tokyo, Japan 2020-2021. Michezo ni kiungo maalum cha majiundo na tunu msingi za maisha ya kiutu. Hapa ni mahali pa kukuza na kudumisha: ukarimu, unyenyekevu, sadaka, udumifu na furaha, kila mtu akijitahidi kuchangia kadiri ya uwezo na karama zake, kielelezo makini cha ujenzi wa umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaobomolea mbali tabia ya ubinafsi na uchoyo. Baba Mtakatifu Francisko anasema Michezo Katika Mtazamo wa Kikristo ni njia ya utume na mchakato wa utakatifu wa maisha. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, ni Sakramenti ya wokovu; ni mtangazaji wa Habari Njema ya Wokovu na shuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Michezo katika nafasi mbalimbali ni jukwaa la kutangaza na kumshuhudia Kristo kwa walimwengu. Michezo ni wakati muafaka wa kuwashirikisha wengine, ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Michezo inatoa fursa ya kuonja: uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji kwa kukutana na watu mbalimbali walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Wanamichezo wa kweli ni wajumbe na mashuhuda wa Kristo Mfufuka wanapokuwa uwanjani. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hata wanamichezo wanaweza kuwa ni watakatifu, kwani daima wanaitwa na kuhamasishwa kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao kila kukicha! Michezo inapania kujenga na kuimarisha urafiki na udugu wa kibinadamu kati ya watu; maelewano na amani; kuheshimiana, maridhiano na utulivu kwa kuthamini tofauti zinazojitokeza kati ya watu. Mashindano ya Michezo ya Olimpiki ya Tokyo, Japan 2020 yalizinduliwa mjini Tokyo nchini Japan tarehe 23 Julai 2021baada ya kuahirishwa kwa muda wa mwaka mmoja kutokana na tishio la janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020 ni kati ya michezo ambayo imekumbana na mazingira magumu na hatarishi, kiasi kwamba, mashabiki na watazamaji hawakuruhusiwa kuhudhuria. Ugonjwa wa UVIKO-19 umekuwa na athari kubwa hata katika masuala ya kiuchumi nchini Japan kutokana na ukweli kwamba, Japan haikuweza kupata watalii waliokuwa wanakusudiwa kutembelea Japan wakati wa mashindano ya Olympiki kwa Mwaka 2020.

Ni katika muktadha wa mashindano haya, Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Tafakari na Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 25 Julai 2021 aliyaelekeza macho yake Jijini Tokyo nchini Japan ambako wanamichezo wanaendelea kupimana nguvu na uzoefu wao katika michezo mbalimbali. Hii ni michezo ambayo inafanyika wakati Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kupambana na janga kubwa la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Tayari kuna baadhi ya wachezaji na maofisa wa Michezo ya Olimpiki Tokyo, Japan 2020 wamekwisha ambukizwa na kuwekwa karantini. Baba Mtakatifu anasema, michezo hii ni kielelezo cha matumaini, alama ya udugu wa kibinadamu na kielelezo makini cha afya bora! Amewaombea wadau wote baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, ili aweze kuwabariki wote wanaoshiriki katika Sherehe hii kubwa ya michezo.

Wakati huo huo, Bwana Antonio Guterres, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, katika ujumbe kwenye ufunguzi wa michuano ya Olimpiki mjini Tokyo, Japan amesikika akisema kwamba, mashindano haya yanasaidia kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu; kwa kuwaunganisha watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia pamoja na kutoa fursa kwa wanamichezo kuonesha karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu sanjari na uvumilivu wa kutosha. Itakumbukwa kwamba, Michezo ya Olimpiki kwa Mwaka 2024 inatarajiwa kuadhimishwa Jijini Paris, nchini Ufaransa.Baba Mtakatifu Francisko kuhusu michezo anakaza kusema, tunu msingi za michezo zinapaswa kusisitizwa miongoni mwa vijana na watoto, ili kuwasaidia kutambua kwamba, kila fursa iliyopo inaweza kutumika kwa ajili ya mchakato wa maboresho ya maisha ya mtu: kiroho na kimwili. Kufaulu na kushindwa katika masuala ya michezo ni ukweli usioweza kupingika. Hii iwe ni fursa ya kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha kwa ujasiri na moyo mkuu; kwa kuzingatia na kuheshimu sheria, kanuni, maadili na utu wema; mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya michezo.

Papa Olimpiki 2020
26 July 2021, 15:03