Tafuta

Huruma na Upendo wa Mungu: Mikate 5 na Samaki 2: Ukarimu!

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake amekazia kuhusu: Ukarimu wa kijana uliosadia kulisha mkutano mkuu wa watu, kielelezo cha sadaka inayofumbatwa katika mantiki ya utendaji wa Mwenyezi Mungu. Hii ni changamoto ya kujikita katika tunu msingi za Kiinjili tayari kujimega na kujitosa sadaka kwa ajili ya Injili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Ukarimu ni muhimu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya kwanza ya Wazee na Wajukuu Duniani Jumapili tarehe 25 Julai 2021, umenogeshwa na kauli mbiu: “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote” Mt 28:20. Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican imeongozwa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilishaji mpya na Baba Mtakatifu katika mahubiri yaliyosomwa kwa niaba yake pia amekazia mambo makuu matatu: kuona, kushirikishana na kuhifadhi. Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Tafakari na Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 25 Julai 2021. Katika tafakari yake amekazia kwa namna ya pekee kabisa kuhusu: Ukarimu wa kijana uliosadia kulisha mkutano mkuu wa watu, kielelezo cha sadaka inayofumbatwa katika mantiki ya utendaji wa Mwenyezi Mungu. Hii ni changamoto ya kujikita katika tunu msingi za Kiinjili tayari kujimega na kujitosa kwa ajili ya Injili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Balaa la njaa na utapiamlo wa kutisha duniani unahitaji ujasiri wa kugawana hata kile kidogo kilichopo!

Injili ya Jumapili ya kumi na saba ya Mwaka B wa Kanisa inaonesha ishara ya Kristo Yesu, kuwashibisha mkutano mkuu wa watu kwa mikate mitano na samaki wawili. Kwa Mitume wa Yesu, chakula hiki, kisingelitosha mkutano mkuu wa watu, lakini kwa Kristo Yesu, mambo yote yamekwenda vyema, kiasi hata cha kukusanya na kujaza vikapu kumi na viwili! Baba Mtakatifu anakaza kusema, si rahisi sana watu kujiweka katika mazingira ya kijana yule mkarimu, aliyediriki kutoa chakula chake kwa ajili ya kulisha mkutano mkuu. Kwa mantiki ya kibinadamu, jambo hili linaonekana kana kwamba, haliwezekani, lakini mbele ya Mungu linawezekana kabisa. Ingependeza, ikiwa kama waamini na watu wenye mapenzi mema wangethubutu kila kukicha kuchukua kitu kidogo na kumpelekea Kristo Yesu ili aweze kufanya miujiza yake! Kwa njia sala, matendo ya huruma: kiroho na kimwili na hata ule udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu, yakitolewa na kuwekwa mbele ya huruma ya Mungu, Kristo Yesu anaweza kutenda ishara kubwa kama inavyojionesha katika Injili.

Mwenyezi Mungu hupenda kutenda makuu kupitia kwa mambo madogo madogo na ya kawaida katika maisha ya mwanadamu. Huu ni ushuhuda unaobubujika kutoka katika uzoefu na mang’amuzi ya Maandiko Matakatifu, kama ilivyokuwa kwa Ibrahimu, Baba wa Imani, Bikira Maria na Kijana mkarimu anayesimuliwa kwenye Injili ya leo. Wote hawa ni mashuhuda wa ukuu, huruma na upendo wa Mungu unaoshuhudiwa katika mambo madogo madogo katika maisha, lakini ni kielelezo kikuu cha sadaka ya maisha. Kwa bahati mbaya, walimwengu wanapenda kujilimbikizia mali na utajiri wa mambo ya duniani. Leo Kristo Yesu, anatoa changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kutoa sadaka na kupunguza hayo mengi ambayo wamejikusanyia katika maisha. Watu wanapenda kung’ang’ania, lakini Kristo Yesu anataka kuwagawia wengine, changamoto na mwaliko wa kujenga utamaduni wa kushirikishana na kugawana mema ya nchi.

Katika muktadha wa ishara ya Kristo Yesu kuwalisha mkutano mkuu kwa mikate mitano na samaki wawili, lakini kitenzi kinachotumiwa ni: kumega mkate, kutoa na kuwagawia watu na wala si kuongeza mikate kwa njia ya miujiza. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, muujiza mkuu unaotendeka hapa ni upendo na mshikamano unaowawezesha watu wa Mungu kushirikiana na kushirikishana mema, neema na baraka ya Mungu. Kwa njia ya upendo na ukarimu wa binadamu, Mwenyezi Mungu anaweza kutenda miujiza. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, hata leo hii mchakato wa uzalishaji wa mali na huduma, haviwezi “kufua dafu” kutatua matatizo na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo, ikiwa kama hakuna mgawanyo wa haki wa rasilimali za dunia. Kuna baa la njaa na utapiamlo wa kutisha unaopekenya utu, maisha na haki msingi za watoto wadogo sehemu mbalimbali za dunia.

Takwimu zinazoonesha kwamba, kuna zaidi ya watoto elfu saba wanaopoteza maisha yao kila siku kutoka sehemu mbalimbali za dunia kutokana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha. Hata leo hii, Kristo Yesu anaendelea kutoa wito na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuonesha ujasiri, huruma na moyo wa upendo, kutoa na kushirikishana na wengine ili kupambana na baa la njaa duniani. Kristo Yesu, anawaalika waja wake kutoa: karama, mapaji sanjari na mali, kwa ajili ya Kristo Yesu na ukarimu wa upendo kwa jirani. Hakuna kitu kinachopotea ikiwa kama watu wengine wameshirikishwa, na badala yake, kitaongezeka maradufu! Hii ni changamoto ya kuondokana na uchoyo pamoja na ubinafsi kwa kisingizio kwamba, Mwenyezi Mungu amewajalia “kiduchu” kumbe, hawana hata kitu cha kutoa ili kuwashirikisha maskini na jirani zao! Jambo la msingi ni kujiamini na kujiaminisha katika upendo wenye huruma unaomwilishwa katika nguvu ya huduma na sadaka! Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu aliyekubali na kuitikia “Ndiyo”, awaombee ili waweze kufungua nyoyo zao kwa Mwenyezi Mungu, ili kusikiliza na kujibu kilio na mahitaji ya maskini na jirani!

Ukarimu wa Mungu

 

25 July 2021, 14:52

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >