Baba Mtakatifu Francisko ameandika barua ya shukrani kwa Jumuiya ya Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, IRCCS kwa ukarimu wao wakati alipokuwa amelazwa hospitalini hapo. Baba Mtakatifu Francisko ameandika barua ya shukrani kwa Jumuiya ya Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, IRCCS kwa ukarimu wao wakati alipokuwa amelazwa hospitalini hapo. 

Papa Francisko: Barua ya Shukrani Kwa Hospitali ya Gemelli, Roma!

Baba Mtakatifu anawapongeza kwa kazi nyeti na ngumu wanayoitekeleza Hospitalini hapo! Hii ni huduma ya huruma ambayo kwa njia ya wagonjwa, wahudumu hao wanaweza kukutana na Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anakiri na kutambua kwamba, ameona kwa macho yake mwenyewe na akatunza hicho alichokiona na atakiwakilisha mbele ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Waswahili husema, “Moyo usio na shukrani hukausha mema yote.” Baba Mtakatifu Francisko baada ya kulazwa tarehe 4 Julai 2021 na kufanyiwa operesheni kubwa kwenye utumbo mpana; aliendelea kupata matibabu hadi aliporuhusiwa tarehe 14 Julai 2021, akawashukuru wale wote waliomsindikiza kwa sala na sadaka zao. Siku hiyo hiyo alikwenda moja kwa moja kumshukuru Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Popoli Romani” kwa sala, maombezi na tunza yake ya kimama wakati wote alipokuwa amelazwa Hospitali ya Gemelli. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 19 Julai 2021 amemwandikia Wakili Carlo Fratta Pasini, Rais wa Mfuko wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli IRCCS “Fondazione Policlinico Universitario Agostino Gemelli IRCCS” kumshukuru kwa niaba ya Familia kubwa ya watu wa Mungu Hospitali ya Gemelli, Roma, kwa ukarimu na udugu wao wa kibinadamu, ambao ameuonja wakati wote alipokuwa amelazwa hospitalini hapo, kiasi cha kumfanya ajisikie kuwa yuko nyumbani!

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa huduma ya afya, daima utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza. Huduma hii imenogeshwa kwa weledi wa kisayansi. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, ndani ya moyo wake, anabeba nyuso, historia na mahangaiko ya watu mbalimbali. Hospitali ya Gemelli ni sawa na mji mdogo ndani ya Jiji kuu la Roma. Hapa ni mahali ambapo kila siku kuna maelfu ya watu wanaofika wakiwa na matumaini pamoja na wasiwasi mbalimbali kutokana na mahangaiko yao. Hospitalini hapo, licha ya kutoa huduma ya tiba, wagonjwa wanapata pia huduma ya kiroho na hivyo Hospitali inamhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili; daima utu na heshima yake vikipewa msukumo wa pekee.

Huduma hii anasema Baba Mtakatifu inakuwa ni chemchemi ya faraja na matumaini wakati wa mateso na majaribu katika maisha. Baba Mtakatifu anawapongeza kwa kazi nyeti na ngumu wanayoitekeleza Hospitalini hapo! Hii ni huduma ya huruma ambayo kwa njia ya wagonjwa, wahudumu hao wanaweza kukutana na Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anakiri na kutambua kwamba, ameona kwa macho yake mwenyewe na akatunza hicho alichokiona na atakiwakilisha mbele ya Mwenyezi Mungu kama ushuhuda wa matendo ya huruma mbele ya Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kumshukuru tena Wakili Carlo Fratta Pasini, Rais wa Mfuko wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli IRCCS, wafanyakazi na wale wote wanaounda familia kubwa ya Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli. Wote hawa amewapatia baraka zake za kitume na kuwaomba kuendelea kumsindikiza kwa sala katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Papa Shukrani

 

19 July 2021, 15:22