Papa Francisko asikitishwa sana na mauaji ya kinyama nchini Haiti, awataka wadau wote kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Papa Francisko asikitishwa sana na mauaji ya kinyama nchini Haiti, awataka wadau wote kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. 

Papa Francisko Asikitishwa na Mauaji ya Kinyama Nchini Haiti

Baba Mtakatifu Francisko kwa nguvu zote ana laani ghasia na matumizi ya nguvu kama njia ya kutafuta suluhu ya migogoro na changamoto za maisha nchini Haiti. Baba Mtakatifu Francisko anaiombea Haiti pamoja na watu wake kuanza kujikita katika ujenzi wa umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Haki, Amani na Utulivu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kufuatia mauaji ya kikatili dhidi ya Rais Jovenel Moïse wa Haiti na baadaye mkewe Martine Moïse kuponea chupuchupu kufariki dunia kufuatia mauaji yaliyofanyika nyumbani kwake usiku wa kuamkia Jumatano tarehe 7 Julai 2021, anasema amesikitishwa sana na mauaji haya. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii, kutuma salam zake za rambirambi kwa watu wa Mungu nchini Haiti kufuatia msiba huu mzito wa kitaifa. Baba Mtakatifu anamwombea Hayati Jovenel Moïse na mkewe, huruma na upendo wa Mungu, ili aweze kuwapatia mwanga, faraja na maisha ya uzima wa milele. Baba Mtakatifu kwa nguvu zote ana laani ghasia na matumizi ya nguvu kama njia ya kutafuta suluhu ya migogoro na changamoto za maisha nchini Haiti. Baba Mtakatifu Francisko anaiombea Haiti pamoja na watu wake kuanza kujikita katika ujenzi wa umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mwishoni mwa salam zake za rambirambi, Baba Mtakatifu Francisko anawapatia watu wa Mungu wote nchini Haiti, baraka zake za kitume!

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Haiti lina laani sana mauaji ya kikatili dhidi ya Rais Jovenel Moïse na hatimaye mke wake Martine Moïse aliyefariki dunia baadaye baada ya kupata majeraha makubwa mwilini mwake! Baraza la Maaskofu Katoliki Haiti linapenda kuonesha uwepo wake wa karibu, umoja na mshikamano wake na watu wote wa Mungu nchini Haiti. Linawakumbuka na kuwaombea wale waliopoteza maisha na linawafariji wananchi wote wa Haiti kwa kuguswa na msiba huu mzito. Baraza la Maaskofu Katoliki Haiti linasema, ghasia haziwezi kuwa ni suluhu ya kumaliza ghasia na changamoto zinazowakabili wananchi wa Haiti. Jambo la msingi katika hali hii tete ni kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Haiti. Huu ni wakati wa kuvunjilia mbali uchu wa mali na madaraka na masilahi ya mtu binafsi na kuanza kujikita katika kutafuta suluhu ya kudumu, kwa kuzingatia upendo, amani na tunu msingi zinazowaunganisha watu wa Mungu nchini Haiti. Ni muda wa kuweka silaha chini ili kuondokana na utamaduni wa kifo na kuanza kujichimbia katika Injili ya uhai, ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote nchini Haiti. Usiue ni Amri ya Mungu!

Taarifa kutoka Haiti zinasema kwamba, watuhumiwa 4 wa mauaji haya ambao wanasadikiwa kuwa ni askari wa kukodiwa, wameuwawa na vikosi vya ulinzi na usalama nchini Haiti. Watu 3 wamepigwa pingu na wanashikiliwa na Polisi, ili kujibu mashtaka yanayowakabili. Askari 4 waliokuwa wametekwa nyara wameachiwa huru. Kwa sasa Serikali inadai kwamba, inadhibiti ulinzi wa usalama wa raia na mali zao. Inawataka wananchi wa Haiti katika kipindi hiki kigumu kuendeleza utulivu! Itakumbukwa kwamba, Haiti kunako mwaka 2010 ilikumbwa na tetemeko la ardhi lililosababisha watu 220, 000 kupoteza maisha. Watu zaidi ya milioni 1.5 wakakosa mahali pa kuishi na wengine 300, 000 wakapata majeraha na ulemavu wa kudumu. Haiti katika siku za hivi karibuni imekumbwa na machafuko ya kisiasa kutokana na uchu wa mali na madaraka.

Hayati Rais Jovenel Moïse wa Haiti amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 53. Alichaguliwa kuiongoza Haiti kunako mwaka 2017 na ukomo wa uongozi na madaraka yake ulikuwa ni mwezi Februari 2021, lakini akajiongezea muda wa kuendelea kukaa madarakani hadi mwaka 2022. Wakati huo huo, akavunja Bunge na kushindwa kutoa nafasi kwa ajili ya uchaguzi mkuu, hali iliyopelekea machafuko ya kisiasa, ghasia na vitendo vya uvunjaji wa haki msingi za binadamu. Haiti pia imekuwa ikikabiliwa na mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza na kwamba, chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 bado haijaanza kutolewa nchini Haiti hadi wakati huu.

Papa Haiti
08 July 2021, 15:23