Afrika ya Kusini kunawaka moto! Afrika ya Kusini kunawaka moto! 

Papa Francisko: Acheni Vurugu Afrika Ya Kusini, Jengeni Umoja!

Papa anaungana na Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini kutoa wito kwa wahusika wote kufanya kazi kwa umoja na mshikamano ili kwa pamoja waweze kujikita katika mchakato wa amani na huduma. Kamwe, Afrika ya Kusini isisahau matamanio halali yaliyowaongoza wananchi katika mapambano yao, ili hatimaye, kujenga na kudumisha amani, utulivu na umoja wa Kitaifa. Amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 52 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2019 ulinogeshwa na kauli mbiu “Siasa safi ni huduma ya amani.” Siasa safi inafumbatwa katika unyenyekevu, kielelezo makini cha huduma katika ngazi mbali mbali za maisha ya binadamu. Lengo ni kukuza na kudumisha dhamana, utu, heshima na tunu msingi za maisha zinazoiwezesha jamii kutekeleza mafao ya wengi. Kumbe, utekelezaji makini wa siasa safi ni changamoto endelevu kwa viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza, kwani wanapaswa kuwalinda raia wao; kwa kushirikiana kikamilifu ili kuboresha maisha ya wananchi wao katika misingi ya haki, uhuru, utu na heshima ya binadamu na kwa njia hii, siasa safi inakuwa ni chombo cha upendo! Baba Mtakatifu anasema, upendo na fadhila za kiutu ziwe ni kwa ajili ya siasa safi inayohudumia haki msingi na amani, kila mtu akijitahidi kujikita katika mafao ya wengi, kama sehemu ya ujenzi wa mji wa Mungu hapa duniani, ili kuendeleza historia ya maisha ya familia ya binadamu.

Haki na usawa; tabia ya kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu. Ukweli, uwazi na uaminifu ni tunu msingi zinazoboresha siasa safi na kwamba, mwanasiasa bora ni yule anayetambua dhamana na wajibu wake kwa jamii; anayeaminika na kuthaminiwa na jamii. Huyu ni kiongozi anayejitaabisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mwaminifu katika ahadi zake kwa wananchi waliomchagua, daima akijitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, tayari kuchochea mageuzi katika maisha ya watu; kwa kuwasikiliza na kutenda kwa ujasiri! Siasa safi ni msingi wa maendeleo fungamani ya binadamu; demokrasia shirikishi na uongozi bora unaojikita katika hoja zenye mashiko na huduma kwa wananchi. Siasa safi inafumbatwa katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi yanayowashirikisha wadau mbalimbali katika jamii; marika pamoja na tamaduni, daima wakijitahidi kujenga imani kati yao kama sehemu ya kukuza na kudumisha amani.  Siasa ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu na kwamba, siasa safi hutekelezwa kwa kufuata katiba, sheria na kanuni maadili; mambo msingi katika kukuza na kudumisha misingi ya amani, haki, ustawi na maendeleo ya wengi.

Siasa safi ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo katika jamii; ni matunda ya ukomavu yanayojikita katika uongozi bora, maridhiano, utawala wa sheria, uvumilivu, uaminifu na bidii. Kamwe tofauti za kiitikadi kisiwe ni chanzo cha vita, kinzani, vurugu na mipasuko ya kijamii inayowatumbukiza watu kwenye majanga na maafa makubwa! Machafuko ya kisiasa na kijamii yanayoendelea ni hatari sana kwa maisha, ustawi, maendeleo, mshikamano wa kitaifa na mafungamano ya kijamii kwa wananchi wengi wa Afrika ya Kusini. Bado janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 linaendelea kupukutisha maisha ya wananchi wengi, hali ambayo inatishia maisha, fursa za ajira na ukuaji wa uchumi fungamani wa binadamu. Wananchi wengi wa Afrika ya Kusini wametumbukia katika dimbwi kubwa la umaskini unaopekenya utu, heshima na haki zao msingi.

Ili kujenga na kuimarisha demokrasia, kuna haja kwa wananchi wa Afrika ya Kusini kujikita katika utawala wa sheria, majadiliano katika ukweli na uwazi. Ukosefu wa haki na usawa, kiwango kikubwa cha umaskini na madhara ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ni kati ya mambo yanayoendelea kuchochea vurugu Afrika ya Kusini. Wananchi wanahitaji huduma na wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa uchumi nchini Afrika ya Kusini. Afrika ya Kusini imekumbwa na machafuko makubwa ya kisiasa na kijamii na hadi kufikia tarehe 16 Julai 2021, watu zaidi ya 212 wamekwisha kupoteza maisha na wengine 2,554 wametiwa mbaroni kwa makosa ya: mauaji, vurugu na uporaji wa mali. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 18 Julai 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amesikitika kusema kuhusu machafuko ya kisiasa na kijamii yaliyojitokeza nchini Afrika ya Kusini kwa siku za hivi karibuni. Afrika ya Kusini bado inakabiliwa na changamoto ya kuyumba kwa uchumi kitaifa pamoja maambukizi makubwa ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Baba Mtakatifu anaungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini kutoa wito kwa wahusika wote kufanya kazi kwa umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili kwa pamoja waweze kujikita katika mchakato wa amani na huduma kwa maskini. Kamwe, Afrika ya Kusini isisahau matamanio halali yaliyowaongoza watu wa Mungu Afrika ya Kusini katika mapambano yao, ili hatimaye, kujenga na kudumisha amani, utulivu na umoja wa Kitaifa. Maandamano makubwa yalianza siku kadhaa zilizopita baada ya Rais wa zamani Jacob Zuma mwenye umri wa miaka 79 kuanza kutumikia kifungo chake cha miezi 15 jela. Zuma alihukumiwa kwa kukaidi agizo la Mahakama, la kumtaka afike mahakamani hapo kujibu shutuma za kesi ya rushwa dhidi yake. Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini, “Southern African Bishops’ Conference, SABC” katika tamko lake mintarafu machafuko ya kisiasa nchini Afrika ya Kusini lina laani vitendo vyote vya vurugu na uvunjifu wa amani ambao umepelekea watu kadhaa kupoteza maisha yao. Huu ni wakati wa kuanza kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi ili kujenga na kuimarisha umoja wa Kitaifa. Chama cha Wamiliki Afrika ya Kusini “South African Property Owners Association” (SAPOA) kinakadiria kwamba, machafuko ya kisiasa na kijamii nchini Afrika ya Kusini yamesababisha hasara ya zaidi ya Fedha ya Afrika ya Kusini Rand bilion 20.

Papa Afrika ya Kusini
19 July 2021, 14:57