Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Julai 2021 ni ujenzi wa urafiki wa kijamii ili kuvunjilia mbali dhana ya uadui, kinzani, mipasuko, chuki na vita. Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Julai 2021 ni ujenzi wa urafiki wa kijamii ili kuvunjilia mbali dhana ya uadui, kinzani, mipasuko, chuki na vita. 

Nia za Baba Mtakatifu Francisko Mwezi Julai 2021: Urafiki wa Kijamii

Baba Mtakatifu Francisko katika Nia zake za Jumla kwa Mwezi Julai, 2021 anawataka waamini kujikita katika mchakato wa ujenzi wa urafiki wa kijamii. Madhumuni makuu ni kuondokana na dhana ya uadui, kinzani na mipasuko, ili hatimaye kujenga urafiki unaonogesha maisha yenye tija na afya bora kwa watu wote wa Mungu. Waamini wanahimizwa kujikita katika majadiliano na udugu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume wa: "Fratelli Tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”, anatoa fursa kwa watu wa Mungu kufanya tafakari ya kina kuhusu: udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii unaowafunga na kuwaambata watu wote bila ubaguzi. Ulimwengu mamboleo unakabiliwa na changamoto kubwa ya vita, umaskini, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, athari za mabadiliko ya tabianchi, myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa pamoja na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Hapa kuna umuhimu wa kutambuana kama ndugu wamoja walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu sanjari na kuwaona wale wote wanaoteseka kuwa ni ufunuo wa Sura ya Kristo Yesu anayeteseka kati pamoja nao. Lengo ni kujizatiti kikamilifu ili kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Huu ni wakati wa kuimarisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa kutambua kwamba, watu wanategemeana na kukamilishana na wala hakuna mtu anayeweza kujiokoa peke yake kama ambavyo imeshuhudiwa katika mapambano dhidi ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika Nia zake za Jumla kwa Mwezi Julai, 2021 anawataka waamini kujikita katika mchakato wa ujenzi wa urafiki wa kijamii. Madhumuni makuu ni kuondokana na dhana ya uadui, kinzani na mipasuko, ili hatimaye kujenga urafiki unaonogesha maisha yenye tija na afya bora kwa watu wote wa Mungu. Si rahisi sana kuweza kutekeleza azma hii kutokana na ukweli kwamba, sehemu kubwa ya sera na siasa, jamii pamoja na vyombo mbalimbali vya mawasiliano ya jamii, vinaendelea kutengeneza dhana ya maadui, ili waweze kushindwa katika kinyang’anyiro cha madaraka. Baba Mtakatifu anawahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujikita zaidi katika majadiliano yanayosimikwa katika misingi ya uhuru, ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni wajibu wa waamini kujenga utamaduni wa kukutana, kushirikishana na kusaidiana na wale ambao wamesukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Huu ni wakati kwa waamini kujiondoa kabisa na mchakato wa kutafuta umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko sanjari na tabia ya watu kutaka “kujimwambafai.”

Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kubomoa kuta za utengano ili kujenga urafiki wa kijamii, utakaowawezesha kuishi kwa amani na utulivu. Kadiri ya Maandiko Matakatifu, waamini wanakumbushwa kwamba, imeandikwa, kwamba, mtu anayepata rafiki wa kweli huyo amepata hazina. Mwezi Julai ni fursa ya kusali ili katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, watu wajifunze kuondokana na chuki, hasira, uhasama, mipasuko na kinzani na hivyo kuanza kujielekeza zaidi katika mchakato wa majadiliano ya urafiki wa kijamii. Nia hizi zinasambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa. Kiini cha ujumbe kutoka katika Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko “Fratelli Tutti” ni baraka za utambulisho wa pamoja unaowafanya watu wote walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu kujisikia kuwa ni ndugu wamoja. Udugu na urafiki wa kijamii ni tema inayowaunganisha watu wote, wanaume kwa wanawake, si tu katika masuala ya udugu wa damu, bali kwa kutakiana mema ya nchi na kusaidiana wakati wa raha na uchungu. Tabia ya kujaliana inavuka mipaka ya utambulisho na mahali anapotoka mtu. Kumbe, “Fratelli Tutti” ni ujumbe unaowakumbatia na kuwaunganisha watu wote ili waweze kujisikia kuwa ni ndugu wamoja walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, licha ya tofauti zao msingi ambazo zinapaswa kuchukuliwa kuwa ni utajiri mkubwa na wala si sababu ya chokochoko za chuki, uhasama, kinzani na vita!

Nia za Papa Julai 2021
20 July 2021, 15:07