Kumbukumbu ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola: Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola 20 Mei 2021 hadi 31 Julai 2022: Vipaumbele: Kupyaisha yote katika Kristo Yesu! Kumbukumbu ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola: Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola 20 Mei 2021 hadi 31 Julai 2022: Vipaumbele: Kupyaisha yote katika Kristo Yesu! 

Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola: Vipaumbele Vya Wayesuit!

Mtakatifu Inyasi wa Loyola alizaliwa mwaka 1491, nchini Hispania. Akafariki tarehe 31 Julai 1556 mjini Roma. Ni Askari aliyetubu na kumwongokea Yesu. Mwaka 1537 akapewa daraja takatifu ya Upadre. Akashirikiana na wenzake, akafaulu kuanzisha Shirika la Wayesuit. Alitangazwa kuwa ni Mwenyeri mwaka 1609. Papa Gregory wa XV akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe 12 Machi 1622.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mtakatifu Inyasi wa Loyola (Iñigo López de Oñaz y Loyola) alizaliwa tarehe 23 Oktoba 1491 huko Azpeitia nchini Hispania. Akafariki dunia tarehe 31 Julai 1556 mjini Roma. Ni Askari aliyetubu na kumwongokea Kristo Yesu na Kanisa lake. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 24 Juni 1537 akapewa daraja takatifu ya Upadre. Mtakatifu Inyas wa Loyola pamoja na mapadre wenzake wapya walitumia muda huu kufanya mazoezi ya shughuli za kuchungaji pamoja na kutumia muda mrefu kwa sala na tafakari ya Neno la Mungu. Kwa kushirikiana na wenzake, akafaulu kuanzisha Shirika la Wayesuit (Jesuits). Alitangazwa kuwa ni Mwenyeheri na Papa Paulo V kunako tarehe 27 Julai 1609. Papa Gregory wa XV akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe 12 Machi 1622. Mama Kanisa anafanya kumbukumbu yake kila mwaka ifikapo tarehe 31 Julai. Yote haya ni kwa ajili ya Sifa na Utukufu wa Mungu Baba Mwenyezi “Ad maiorem Dei gloriam au Ad majórem Dei glóriam.”

Shirika ya Wayesuit kuanzia tarehe 20 Mei 2021 hadi tarehe 31 Julai 2022, Kumbukumbu ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola, wanaadhimisha Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Tarehe 20 Mei wamekumbuka siku ile ambayo Mtakatifu Inyasi alijeruhiwa vitani huko Pamplona, nchini Hispania, kunako mwaka 1521. Huo ukawa ni mwanzo wa mchakato wa toba na wongofu wake wa ndani sanjari na mageuzi makubwa katika maisha, historia na utume wa Kanisa Katoliki na sasa imegota miaka 500. Padre Arturo Marcelino Sosa Abascal, Mkuu wa Shirika ya Wayesuit anabainisha kwamba, maadhimisho haya yatadumu kwa kipindi cha miezi kumi na nne, kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, ili kupyaisha maisha na utume wao mbele ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu “Angalieni mambo yote mapya katika Kristo”. Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola unaongozwa na Mpango Mkakati wa Maisha na Utume wao katika kipindi cha miaka kumi yaani: 2019-2029. Wayesuit wanamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia neema ya toba na wongofu wa ndani katika maisha na utume wao kila kukicha!

Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola ni fursa ya kushirikiana na wadau mbali mbali katika maisha na utume wa Wayesuit, ili kuweza kuyapatanisha yote na Kristo Yesu, anayepaswa kupewa kipaumbele cha kwanza! Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 23 Mei 2021 katika ujumbe wake kwa njia ya video, aliungana na mahujaji wa Kiyesuiti kwa ajili ya kusali katika maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Jeraha la Mtakatifu Inyasi wa Loyola limekuwa ni chanzo cha mageuzi makubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Ndoto ya awali ya Mtakatifu Inyasi “ikatoweka kama umande wa asubuhi”. Mwenyezi Mungu akamkirimia ndoto kubwa zaidi kwa ajili ya wokovu wa roho za watu. Toba na wongofu wa ndani ni mchakato wa maisha ya kila siku, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Toba, wongofu wa ndani na mang’amuzi ya maisha ni mambo ambayo yamekuwa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola, chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu anayewawezesha waamini kukutana na Kristo Yesu katika maisha yao. Kama mahujaji “huku bondeni kwenye machozi”, Wayesuit wanakutana pia na watu wa Mungu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Inyasi wa Loyola.

Huu ni mwaliko wa kuendelea kutubu na kumwongekea Mungu, ili kuweza kuisikiliza sauti ya Mungu anayezungumza nao kwa njia yao. Wayesuit wajifunze kusoma alama za nyakati na kuendeleza mchakato wa majadiliano na jirani pamoja na ulimwengu katika ujumla wake. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, wale wote wanaokumbatia tasaufi ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola, wataweza kusafiri pamoja kama wanafamilia moja ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Mwaka huu iwe ni fursa ya kuuendea ulimwengu, kusaidia roho za watu na kuyaangalia mambo yote mapya katika jicho la Kristo Yesu. Wayesuit wajinyenyekeshe na kuwaachia wengine nafasi ili waweze kuwasaidia. Hii inatokana na ukweli kwamba, hakuna mtu anayeweza kujiokoa mwenyewe. Wote wanaweza kuokolewa kama jumuiya au kuangamia na wala hakuna njia ya mkato. Ni Yesu peke yake ambaye amewaonesha njia, hivyo ni wajibu wao kusaidiana kutafuta na hatimaye kuambata njia inayokwenda kwa Kristo Yesu.

Tarehe 12 Machi 2022 Wayesuit wataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu mjini Roma kama sehemu ya kumbukumbu ya Miaka 400 tangu Mtakatifu Inyasi wa Loyola, Mtakatifu Francisko Xavier, Mtakatifu Theresa wa Yesu, Mtakatifu Isidore Labrador pamoja na Mtakatifu Philipo Neri walipotangazwa na Kanisa kuwa ni Watakatifu. Karama ni chemchemi ya maisha na utume wa Shirika, mwaliko na changamoto ya kujenga ukaribu zaidi katika utume ambao Shirika limekabidhiwa na Roho Mtakatifu, ili mwaliko huu uweze kuingia na kugusa undani wa maisha ya watu zaidi. Wayesuit wanataka kujifunza kutoka kwa vijana, ili waweze kuwasindikiza, ili kugundua maana ya maisha kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Lengo ni kuwajengea vijana uwezo wa kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi; mahali ambapo utu, heshima na haki msingi za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa, sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Wayesuit wanataka kushirikiana na vijana wa kizazi kipya: Muda, ndoto na matumaini waliyo nayo! Kwa Wayesuit waliotawanyika sehemu mbali mbali za dunia, huu ni muda wa kufuata nyayo za Mtakatifu Inyasi wa Loyola, hujaji maarufu, kwa njia ya mapambano ya maisha ya kiroho, toba na wongofu wa ndani, ili kujenga mahusiano ya karibu na Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Ukaribu na upendo kwa Mwenyezi Mungu, uwasaidie Wayesuit kujenga na kudumisha umoja katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Maisha na Utume wao katika kipindi cha Miaka 10. Wao ni warithi wa karama ambayo imesheheni tunu msingi za maisha ya kimisionari. Ufukara pamoja na kutekeleza mapenzi ya Mungu ni kati ya mambo ambayo Mtakatifu Inyasi wa Loyola aliyapokea kama zawadi kutoka juu. Mfano wa maisha ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola na wale wenzake, uwawezeshe Wayesuit kujenga mahusiano ya pekee na Kristo Yesu, ili aweze kuwakirimia amani na utulivu wa ndani. Wawe mstari wa mbele katika kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Hii ni sehemu ya urithi na amana inayobubujika kutoka katika Karama ya Wayesuit. Huu ni wakati wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote ambao utu, heshima na haki zao msingi zinasiginwa kila kukicha! Lengo ni kushikamana na maskini, ili kuleta mageuzi katika miundo mbinu inayokandamiza utu na heshima ya binadamu. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limesababisha madhara makubwa katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu. Mpasuko mkubwa kati ya maskini na matajiri umeonekana wazi wazi. Kumekuwepo na kinzani katika Jumuiya ya Kimataifa pamoja na uwiano tenge katika masuala ya kiikolojia. Wayesuit waungane na Kristo Yesu pamoja na maskini, kwa kuishi na kuukumbatia ufukara wao, kama ushuhuda wa upendo wao kwa Kristo Yesu. Wayesuit watambue na kukiri dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu, daima wakijitahidi kujitambulisha na Kristo Yesu, ili aweze kuwasaidia kutubu na kumwongokea. Wawe tayari kuleta mabadiliko katika maisha ya maskini, kwa kusoma alama za nyakati, kwa toba na wongofu wa ndani ili kupyaisha karama ya Shirika.

Wayesuit wajenge umoja na mshikamano na Kristo Yesu, ndugu na rafiki yao mpendwa, ili aweze kuwakirimia imani, matumaini na mapendo kwa kuendelea kukaaa pamoja nao, chini maongozi ya Roho Mtakatifu. Shirika la Wayesuit lililoanzishwa na Mtakatifu Inyasi wa Loyola katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa, linapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mambo makuu yafuatayo. Kwanza: Kuendeleza mchakato wa mang’amuzi na mafungo ya maisha ya kiroho; Kushikamana na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; Kuwasindikiza vijana katika safari ya maisha yao; Mwishoni, ni utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Haya ni mambo ambayo yanabainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika barua aliyomwandikia hivi karibuni Padre Arturo Sosa Abascal, Mkuu wa Shirika ya Wayesuit kama sehemu ya Mpango Mkakati wa Maisha na Utume wao katika kipindi cha miaka kumi yaani kuanzia mwaka 2019-2029. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hivi pia ndivyo vipaumbele vya Kanisa la Kiulimwengu kwa wakati huu! Mambo ambayo yanapaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya Sinodi za Maaskofu na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia. Vipaumbele hivi vinachota utajiri wake kutoka katika Wosia wa Kitume, “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili.”

Vipaumbele vya Wayesuit katika kipindi cha miaka kumi ni msingi wa mahusiano na mafungamano kati ya Wayesuit na Kristo Yesu; mambo yanayomwilishwa katika maisha binafsi na katika Jumuiya inayosali na kufanya mang’amuzi ya pamoja. Vipaumbele hivi ni sehemu ya mchakato wa maisha na utume wa Wayesuit ambao umefanyiwa kazi katika kipindi cha miaka miwili, ili kuhakikisha kwamba, Wayesuit wanatumia kikamilifu rasilimali watu, vitu na fedha, ili kufikia lengo hili muhimu, daima wakiendelea kusoma alama za nyakati. Hapa kinachohitajika ni kukuza na kudumisha kipaji cha ubunifu, kwa kuwashirikisha watu kutoka katika makundi na medani mbali mbali za maisha, ili kugundua amana na utajiri unaofumbatwa katika mafungo ya kiroho yanayotolewa na Wayesuit. Lengo ni kuhakikisha kwamba, haki jamii inapewa msukumo wa pekee, ili kweli mabadiliko makubwa yanayojitokeza katika masuala ya: kiuchumi, kijamii na kisiasa, yanazingatia haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Kuwasindikiza vijana katika safari ya maisha yao ni pamoja na kuyaangalia yale mema, mazuri na matakatifu yanayowazunguka vijana katika “vijiwe vyao”, kwa kusikiliza na kujibu kiu na matamanio yao halali kadiri ya mabadiliko ya jamii; kwa kuendelea kusoma alama za nyakati.

Hii ni changamoto ya kuwapatia vijana fursa ya kuonesha vipaji na ubunifu wao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Umefika wakati kwa viongozi wa Kanisa kujifunza kutoka kwa vijana wa kizazi kipya! Mwishoni, ni utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Huu ni mwaliko wa kushiriki katika sera, mbinu na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira, pamoja na kuangalia sera mbadala, ili kuweza kudhibiti uharibifu wa mazingira unaoendelea kusababisha majanga makubwa katika maisha ya watu wengi duniani. Hii ni changamoto ya kushirikiana na wadau mbali mbali kama sehemu ya mbinu mkakati wa utekelezaji wa malengo haya katika maisha na utume wa Wayesuit.

Mtakatifu Inyasi
31 July 2021, 07:47