Papa Francisko atoa wito kwa wadau mbalimbali nchini Eswatini kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya amani na utulivu. Papa Francisko atoa wito kwa wadau mbalimbali nchini Eswatini kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya amani na utulivu. 

Mshikamano wa Papa Francisko na Wananchi wa Eswatini! Machafuko!

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 4 Julai 2021 ametoa wito kwa viongozi wenye dhamana, mamlaka na wananchi wanaoandamana wakitaka maboresho katika maisha yao, kuunganisha nguvu zao kwa pamoja na kuanza kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli, uwazi, ustawi na mafao ya wengi. Watu zaidi ya 40 wamekwisha fariki dunia na wengine 150 kujeruhiwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kwenda kulazwa na hatimaye kufanyiwa upasuaji mkubwa, Jumapili tarehe 4 Julai 2021, aliwaongoza watu wa Mungu kutafakari kuhusu kashfa ya Fumbo la Umwilisho. Baada ya sala ya Malaika wa Bwana, aliyageuzia mawazo yake hadi nchini Eswatini, ambako katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na machafuko ya kisiasa ambayo yamepelekea hadi wakati huu watu zaidi ya 40 kupoteza maisha na wengine 150 kujeruhiwa vibaya. Baba Mtakatifu ametoa wito kwa viongozi wenye dhamana, mamlaka na wananchi wanaoandamana wakitaka maboresho katika maisha yao, kuunganisha nguvu zao kwa pamoja na kuanza kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli, uwazi, ustawi na mafao ya wengi.

Iwe ni fursa ya kujikita katika mchakato wa upatanisho wa kitaifa, ili kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika haki na amani licha ya tofauti zao msingi. Katika siku za hivi karibuni, kumekuwepo na maandamano makubwa nchini Eswatini kudai demokrasia zaidi lakini kwa mshangao mkubwa, waandamanaji wamekuwa wakikumbana na “mkono wa chuma”. Watetezi wa haki msingi za binadamu wanautaka utawala wa nchi ya Eswatini kujielekeza katika kujenga na kudumisha demokrasia na utawala bora unazozingatia sheria. Umefika wakati kwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini Eswatini kutotumia nguvu kupita kiasi kupambana na waandamanaji.

Papa Eswatini

 

05 July 2021, 16:26