Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya : Mwanasayansi aliyepigania utu, heshima na haki msingi za binadamu ndani na nje ya DRC. Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya : Mwanasayansi aliyepigania utu, heshima na haki msingi za binadamu ndani na nje ya DRC. 

Papa Francisko: Kardinali Pasinya: Mwanasayansi, Haki, Amani na Utu!

Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya alikuwa ni mwanasayansi, kiongozi maarufu katika maisha ya kiroho na mtu aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu, mahali popote pale alipoitwa na kutumwa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa Kikuhani. Alikuwa jasiri na ameonesha moyo wa huduma, sadaka na unabii wa Kanisa! RIP.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC, amefariki dunia Jumapili tarehe 11 Julai 2021 Kwenye Hospitali ya “Clinique de l'Europe, Le Port-Marly”, mjini Versailles nchini Ufaransa akiwa na umri wa miaka 81 tangu kuzaliwa kwake! Kwa siku za hivi karibuni, hali ya afya yake ilidhohofu sana, kiasi cha kupelekwa nchini Ufaransa kwa matibabu zaidi. Baba Mtakatifu Francisko katika salam za rambirambi alizomwandikia Kardinali Fridolin Ambongo Besungu wa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC; anasema, amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kinshasa. Baba Mtakatifu Francisko anamwomba amfikishie salam zake za rambirambi kwa watu wa Mungu wa Jimbo Katoliki la Inongo, Jimbo kuu la Kisangani pamoja na Jimbo kuu la Kinshasa na mahali pote ambapo Hayati Monsengo katika maisha na utume wake kama Padre, alitoa huduma ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Anamwomba, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kumpokea Mtumishi wake mwaminifu Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya katika amani na mwanga wa uzima wa milele.

Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya alikuwa ni mwanasayansi, kiongozi maarufu katika maisha ya kiroho na mtu aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu, mahali popote pale alipoitwa na kutumwa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa Kikuhani. Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, ameonesha na kushuhudia moyo wa huduma kwa Kanisa; daima alikuwa makini kusoma alama za nyakati, kusikiliza na kujibu kilio cha mahitaji msingi ya watu wa Mungu. Ni kiongozi aliyeonesha ujasiri wa ajabu na maamuzi makini, akatumia muda wake mwingi kwa ajili ya kutamadunisha imani, huku akitoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na “akina yakhe, pangu pakavu tia mchuzi.” Alifahamu na kutambua umuhimu wa maskini kama hazina ya maisha na utume wa Kanisa katika mchakato mzima wa uinjilishaji. Ni katika muktadha huu anasema Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake za rambirambi kwamba, Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya alijitahidi kutamadunisha dhana ya unabii wa Kanisa katika maisha na utume wake.

Ni kiongozi wa Kanisa aliyejisadaka kutafuta, kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na umoja wa Kitaifa; ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini DRC. Ni kiongozi aliyesikilizwa kwa makini na watu kuthamini mchango wake katika maisha na utume wa Kanisa; katika masuala ya kijamii na kisiasa; akasimama kidete katika mchakato wa umoja wa Kitaifa nchini DRC. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Aprili 2013 akamteuwa kuwa ni kati ya Makardinali wake washauri katika mchakato wa kufanya mageuzi makubwa katika Sekretarieti kuu ya Vatican. Wakati wote amekuwa mwaminifu na tayari kutoa mchango wake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kiulimwengu. Baba Mtakatifu anapenda kutoa baraka zake za kitume kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema watakaoshiriki katika Ibada ya Mazishi ya Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC aliyefariki dunia Jumapili tarehe 11 Julai 2021 huko nchini Ufaransa.

Itakumbukwa kwamba, Hayati Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kinshasa nchini DRC alizaliwa tarehe 7 Oktoba 1939 huko Mongobelè. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi Chuo Kikuu cha Urbanian kilichoko mjini Roma, tarehe 21 Desemba 1963 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Ni kati ya wanafunzi mahiri wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu. Alibahatika kufundisha Maandiko Matakatifu na Taalimungu, Seminari kuu ya Mtakatifu Yohane XXIII pamoja na Kitivo cha Taalimungu, Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Kinshasa, DRC. Tarehe 13 Februari 1980 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Inongo nchini DRC na kuwekwa wakfu tarehe 4 Mei 1980. Tarehe 7 Aprili 1981 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo wa kuu la Kisangani. Tarehe 1 Septemba 1988 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kisangani.

Kumbukumbu za kihistoria zinaonesha kwamba, kunako mwaka 1984 alichaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zaire kama ilivyojulikana wakati ule. Akawa ni kiongozi aliyejipambanua kuongoza mageuzi makubwa yaliyokuwa yanatendeka nchini Zaire, hadi kufikia ukomo wake kwenye Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, “Democratic Republic of Congo, DRC.” Katika mchakato huu, akasimamia haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu nchini DRC. Alikosoa pale palipopinda, akapinga kwa nguvu zote kishawishi cha baadhi ya viongozi kutaka kupindisha Katiba ya nchi ili wabaki madarakani. Ni katika hali na mazingira kama haya, Hayati Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kinshasa, mara kadhaa ameponea chupu chupu kuuwawa kutokana na msimamo wake kuhusu utawala wa sheria, demokrasia, ustawi na maendeleo ya wengi. Tarehe 6 Desemba 2007, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kinshasa. Amekuwa ni mshikiri mzuri katika maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kuhusu: Uinjilishaji na urithishaji wa imani ya Mwaka 2012, Changamoto za kichungaji kwa familia katika muktadha wa Uinjilishaji ya mwaka 2014, Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia ya mwaka 2015.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Aprili 2013 akamteuwa kuwa ni kati ya Makardinali wake washauri katika mchakato wa kufanya mageuzi makubwa katika Sekretarieti kuu ya Vatican. Amefariki dunia wakati Muswada wa Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” ikiwa katika hatua zake za mwisho mwisho kabla ya kuzinduliwa rasmi. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI tarehe 20 Novemba 2010 akamteuwa na kumsimika kuwa ni Kardinali. Mwezi Oktoba 2018 akang’atuka kutoka Baraza la Makardinali Washauri. Tarehe 1 Novemba 2018, Baba Mtakatifu Francisko akaridhia kung’atuka kwake kutoka madarakani. Na Jumapili tarehe 11 Julai 2021 akaiga dunia, akiwa amewatumikia watu wa Mungu kama Padre kwa muda wa zaidi ya miaka 57. Kama Askofu mwenye dhamana ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu ametumikia kwa miaka 41 na kama Kardinali miaka 10. Amefariki dunia akiwa na umti wa miaka 81.

Papa DRC

 

13 July 2021, 15:45