Papa Francisko asikitishwa na kifo cha Mzee Dino Impagliazzo, Mpishi mkuu wa maskini wa mji wa Roma. Papa Francisko asikitishwa na kifo cha Mzee Dino Impagliazzo, Mpishi mkuu wa maskini wa mji wa Roma. 

Dino Impagliazzo Mpishi Mkuu wa Maskini wa Roma Amefariki Dunia!

Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake anasema, kamwe kifo hakiwezi kuzoeleka na daima kitakuwa ni sababu ya majonzi na machungu ya moyo, hata kama ni sehemu ya Fumbo la Mungu katika maisha ya mwanadamu. Papa anapenda kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwa mapaji ambayo alimkirimia Mzee Dino Impagliazzo katika safari ya maisha yake ya miaka 91.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mzee Dino Impagliazzo, aliyekuwa na umri wa miaka 91 alifahamika na watu wengi na hasa maskini wa mji wa Roma kwa sadaka na majitoleo yake kwa maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum. Kila siku ajitahidi kuhakikisha kwamba, walau anapika kila siku chakula cha kuwatosheleza watu zaidi ya 300. Hiki ni chakula ambacho walikuwa wanagawiwa maskini wa Roma wanaoishi kwenye vituo vya treni. Alikuwa ni mwanachama hai wa watu wa kujitolea, yaani RomAmor, Chama cha Kitume cha Wafokolari pamoja na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ambayo mtoto wake Marco Impagliazzo ni Rais wake. Mzee Dino Impagliazzo amefariki dunia wakati Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya kwanza ya Wazee na Wajukuu Duniani, hapo tarehe 25 Julai 2021 na mazishi yake kufanyika tarehe 27 Julai 2021 kwa kuwashirikisha viongozi wakuu wa Kanisa na kwa namna ya pekee kabisa Kardinali Konrad Krajewski, Mtunza Sadaka Mkuu wa Kipapa. Kanisa linawategemea sana maskini katika maisha na utume wake, kwani maskini ni amana na utajiri wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kimsingi, maskini ndio walengwa wakuu wa Injili.

Dhana ya umaskini inajikita katika umaskini wa hali na mali; maadili na utu wema; kwani wote hawa, Kristo Yesu amejisadaka kwa ajili ya kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu. Wakristo wanapaswa kuwajali, kuwathamini na kuwapenda maskini na watu wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama alivyojitahidi kutenda Mzee Dino Impagliazzo. Kanisa linatoa huduma ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa maskini, kwa kujali na kuthamini utu, heshima na haki zao msingi, kwani hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake za rambirambi kwa Professa Marco Impagliazzo anasema, kamwe kifo hakiwezi kuzoeleka na daima kitakuwa ni sababu ya majonzi na machungu ya moyo, hata kama ni sehemu ya Fumbo la Mungu katika maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii, kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwa karama na mapaji ambayo alimkirimia Mzee Dino Impagliazzo katika safari ya maisha yake ya miaka 91.

Ni Baba ambaye amemfundisha na kumrithisha kijana wake Marco Impagliazzo tunu msingi za Kiinjili hata naye leo hii, anaendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma ya Injili kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mzee Dino Impagliazzo alikuwa na upendo mkuu kwa maskini, kiasi cha kutambulikana nao kama “Lo Chef dei poveri” yaani “Mpishi mkuu wa maskini”. Ni mzee tangu ujana wake, alijitahidi kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini, ushuhuda makini na wenye mvuto unaoacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za watu. Amekuwa ni shuhuda wa Injili ya upendo kwa vijana wengi kwa hakika wengi wanasikitika kutokana na kifo chake! Kwa upande wake, Askofu Ambrogio Spreafico anayetekeleza utume wake miongoni mwa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, ndiye aliyeongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mazishi ya Mzee Dino Impagliazzo. Amemtaja Mzee Dino Impagliazzo kuwa ni mtu wa haki, aliyekita maisha yake katika sala, tafakari ya Neno la Mungu na kulimwilisha katika matendo ya huruma.

Mzee Dino alishiriki kikamilifu katika Ibada ya Ekaristi Takatifu, ikampatia nguvu ya kujisadaka kwa ajili ya maskini wa Roma. Huduma hii, iliwasaidia wengi kuboresha maisha, mahusiano na mafungamano yao ya kijamii pamoja na Mwenyezi Mungu. Imani kwake, ikawa ni chemchemi na kikolezo cha ujenzi wa urafiki wa kibinadamu unaosimikwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu. Alipenda kusimika maisha na utume wake kwa upendo kwa Mungu na jirani kama sehemu ya utekelezaji wa Amri kuu ya upendo. Ni Mzee aliyesadiki umuhimu wa ujenzi wa umoja, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu.

Fumbo la Kifo

 

29 July 2021, 15:19