Viongozi wakuu wa Makanisa wamewaandikia wananchi wa Sudan ya Kusini Ujumbe wa Matumaini kama sehemu ya kumbukizi la miaka 10 ya uhuru wa bendera. Viongozi wakuu wa Makanisa wamewaandikia wananchi wa Sudan ya Kusini Ujumbe wa Matumaini kama sehemu ya kumbukizi la miaka 10 ya uhuru wa bendera. 

Barua ya Viongozi wa Makanisa Kwa Sudan ya Kusini Julai, 2021

Tarehe 9 Julai 2011 ni tukio muhimu sana katika historia ya maisha ya wananchi wa Sudan ya Kusini wanaokumbuka yale yaliyopita, hali yao ya sasa na matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi. Viongozi wa Makanisa wanawahamasisha viongozi wa Serikali nchini Sudan ya Kusini kuhakikisha kwamba, wanawajengea wananchi wao mazingira ya kusherehekes vyema matunda ya uhuru.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameungana na Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Canterbury ambaye pia ni kiongozi mkuu wa Kanisa la Anglikani pamoja na Mchungaji Jim Wallace, Mratibu wa Kanisa la Scotland, wameandika ujumbe wa matashi mema kwa watu wa Mungu Sudan ya Kusini. Itakumbukwa kwamba, Sudan ya Kusini, tarehe 9 Julai 2021 inaadhimisha kumbukizi la miaka 10 tangu ilipojipatia uhuru wa bendera hapo tarehe 9 Julai 2011. Hili ni tukio muhimu sana katika historia ya maisha ya wananchi wa Sudan ya Kusini wanaokumbuka yale yaliyopita, hali yao ya sasa na matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi. Viongozi wa Makanisa wanawahamasisha viongozi wa Serikali nchini Sudan ya Kusini kuhakikisha kwamba, wanawajengea wananchi wao mazingira yatakayowawezesha kusherehekea na kufurahia kikamilifu matunda ya uhuru.

Katika maadhimisho ya Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2020, viongozi hawa walisali na kuwaombea, ili viongozi wa Sudan ya Kusini waweze kutambua na kunafsisha ndani mwao uaminifu na ukarimu mkubwa kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Viongozi wa Makanisa wanaendelea kusali, ili hatimaye, viongozi wa Serikali ya Sudan ya Kusini waweze kutambua amani ya Mungu, ipitayo akili zote, iwahifadhi nyoyo na nia zao kwa ajili ya taifa la Sudan ya Kusini. Wanakiri kwamba, wameona na kushuhudia maendeleo kidogo yaliyofikiwa, lakini bado wanatambua kwamba, wananchi wengi hawajaonja mafanikio katika mchakato wa utekelezaji wa Makubaliano ya Amani. Familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini katika wimbo wa Taifa lake, inamwomba, inamshukuru na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka anazowakirimia waja wake! Ni wimbo wa amani, haki, uhuru, ustawi na maendeleo ya wengi!

Bado kuna mambo mengi yanayopaswa kutekelezwa ili kweli Sudan ya Kusini, iweze kuhakisi Ufalme wa Mungu kama unavyofafanuliwa na Mtakatifu Paulo, Mtume katika Waraka wake wa Pili kwa Wakorintho Sura ya 5: yaani: Utu, heshima na haki msingi za binadamu zinalindwa na kudumishwa sanjari na kujielekeza katika mchakato wa huduma ya upatanisho wa kitaifa. Dhamana na wajibu huu unahitaji sadaka na majitoleo kutoka kwa viongozi wa Sudan ya Kusini. Kristo Yesu, awe ni mfano bora wa uongozi na wanapaswa kutambua kwamba, viongozi wa Kanisa wako upande wao, wanapoonesha matumaini yao kwa Sudan ya Kusini kwa kupyaisha mang’amuzi yao, ili kuangalia ni kwa jinsi gani wanavyoweza kuwahudumia watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini. Viongozi wakuu wa Serikali na kidini kutoka Sudan ya Kusini walifanya mafungo ya kiroho kuanzia tarehe 10-11 Aprili 2019 mjini Vatican.  Hili ni tukio ambalo lilikita mizizi yake katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene; maisha ya kiroho na kidiplomasia, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini.

Hiki kilikuwa ni kipindi muafaka cha tafakari, toba na wongofu wa ndani, tayari kuanza mchakato wa upatanisho, msamaha na ujenzi wa umoja wa kitaifa. Viongozi wa Serikali na Kidini nchini Sudan ya Kusini, walijiweka chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu wakiomba: haki, amani, msamaha, upatanisho na ujenzi wa umoja wa kitaifa! Katika ujumbe wao, viongozi wa Makanisa wanasema kwamba, wanaendelea kusali ili ahadi walizoweka viongozi wa Sudan ya Kusini ziweze kuratibu shughuli zao, ili hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko na viongozi wenzake wa Kikanisa waweze kutembelea Sudan ya Kusini na kusherehekea mchango wao kwa Taifa la Sudan ya Kusini katika kumwilisha matumaini yaliyotolewa kunako tarehe 9 Julai 2011. Kwa wakati huu, viongozi wa Makanisa wanapenda kuwapatia baraka ya Mwenyezi Mungu inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu na amani! Sudan ya Kusini ilijipatia uhuru wake wa bendera tarehe 9 Julai 2011.

Tangu wakati huo, ikajikuta inatumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo imekwisha kusababisha zaidi ya watu laki nne kupoteza maisha na wengine milioni nne kukosa makazi ya kudumu. Nusu ya idadi ya wananchi wa Sudan ya Kusini wanakabiliwa na baa la njaa. Mwaka 2018 Serikali na viongozi wa upinzani walitiliana sahihi Mkataba wa Amani “Revitalised Agreement on the Resolution of Conflict in South Sudan” (R-ARCSS). Taarifa ya Umoja wa Mataifa inaonesha kwamba, hali nchini Sudan ya Kusini bado ni tete kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara, maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 pamoja na baa la njaa.

Sudan ya Kusini
09 July 2021, 15:44