Papa Francisko Barua Binafsi Kuhusu Liturujia "Tradionis custodes" Walinzi wa Mapokeo" Papa Francisko Barua Binafsi Kuhusu Liturujia "Tradionis custodes" Walinzi wa Mapokeo" 

Papa: Barua Binafsi: Traditionis Custodes: Walinzi wa Mapokeo!

Barua Binafsi: Kuhusu Liturujia: “Traditionis custodes” yaani Walinzi wa Mapokeo ya Kanisa: Juu ya Matumizi ya Liturujia ya Kirumi Kabla ya Mageuzi ya Mwaka 1970. Sheria Mpya Kuhusu Ibada ya Misa Takatifu, Maaskofu mahalia wanawajibika zaidi. Makundi ya waamini yanayotumia Misale ya Kirumi ya Mwaka 1962 iliyorekebishwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Umoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Ibada ya Misa Takatifu ni kumbukumbu ya sadaka ambamo hudumisha sadaka ya Msalaba, na karamu takatifu ya ushirika katika Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu. Lakini adhimisho la sadaka ya Ekaristi huelekezwa kwenye umoja wa ndani wa waamini na Kristo Yesu kwa njia ya komunyo. Kukomunika ni kumpokea Kristo Yesu mwenyewe aliyejitoa sadaka kwa ajili ya waja wake. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni moyo na kilele cha uzima wa Kanisa, kwani ndani yake Kristo Yesu hulishirikisha Kanisa lake na viungo vyake vyote na sadaka yake ya sifa na shukrani inayotolewa Msalabani kwa Baba yake mara moja na kwa daima. Kwa njia ya sadaka hii anamimina neema za wokovu juu ya Fumbo la Mwili wake, ndiko Kanisa. Adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu daima lina: Liturujia ya Neno la Mungu, shukrani kwa Mungu Baba kwa ajili ya fadhili zake zote, juu ya yote, paji la Mwanawe, mageuzo ya mkate na ya divai na ushirika katika karamu ya kiliturujia kwa kupokea Mwili na Damu Azizi; mambo yote haya huunda tendo moja na lile lile la Ibada.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 16 Julai 2021 amechapisha Barua Binafsi: Kuhusu Liturujia “Motu Proprio “Traditionis custodes” yaani Walinzi wa Mapokeo ya Kanisa: Juu ya Matumizi ya Liturujia ya Kirumi Kabla ya Mageuzi ya Mwaka 1970. “Sheria Mpya Kuhusu Ibada ya Misa Takatifu, Maaskofu mahalia wanawajibika zaidi.” Makundi ya waamini yanayotumia “Missale Romanarum” yaani Misale ya Kirumi ya Mwaka 1962 iliyorekebishwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI miaka 14 iliyopita imefanyiwa marekebisho na Baba Mtakatifu Francisko na anatoa sababu msingi zilizompelekea kuandika Barua Binafsi “Motu Proprio “Traditionis custodes” yaani Walinzi wa Mapokeo ya Kanisa: Juu ya Matumizi ya Liturujia ya Kirumi Kabla ya Mageuzi ya Mwaka 1970. Papa Francisko anasema, ni wajibu wa Askofu mahalia kuhakikisha kwamba hata makundi ya waamni yanayotumia misale hii kuyatambua na kuheshimu mabadiliko ya Kiliturujia yanayofanywa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na kadiri ya mwanga angavu wa Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji katika Kanisa, yaani “Magisterium”.

Tangu sasa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa kufuata Misale ya Kirumi ya zamani, hayataruhusiwa tena kuadhimisha kwenye Parokia. Utakuwa ni wajibu wa Askofu mahalia kupanga Kanisa na siku ambamo Ibada hii ya Misa Takatifu itaadhimishwa. Masomo ya Ibada ya Misa Takatifu yanapaswa kuwa ni katika lugha ya watu mahalia iliyopitishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki husika. Kiongozi mkuu wa Ibada atakuwa ni yule aliyeteuliwa na kutumwa na Askofu mahalia. Maadhimisho haya yawe ni kwa ajili ya ukuaji na ustawi wa maisha ya kiroho. Padre kiongozi wa Ibada lazima awe siyo tu na moyo na ari ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa bali pia awe ni kiongozi wa shughuli za kichungaji na maisha ya kiroho ya waamini hawa. Askofu mahalia “ana wajibu wa kutoruhusu katiba ya makundi mapya”. Kwa Mapadre wote watakaopewa daraja Takatifu ya Upadre baada ya kuchapishwa kwa Barua Binafsi “Motu Proprio “Traditionis custodes” yaani “Sheria Mpya Kuhusu Ibada ya Misa Takatifu, Maaskofu mahalia wanawajibika zaidi” watapaswa kutoa maombi maalum kwa Askofu mahalia. Na kabla ya kutoa ruhusa, Askofu mahalia itabidi apate ushauri kutoka Vatican.

Kwa wale waliokuwa wanaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa kutumia Misale ya Kirumi ya zamani, inawapasa sasa kuomba kibali upya kutoka kwa Askofu mahalia, ili kuendelea kuitumia Misale hii. Kwa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume yaliyoanzishwa chini ya Tume ya Kipapa ya Ecclesia Dei, tangu sasa yatakuwa chini ya usimamizi wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume. Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa sanjari na Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, yanao wajibu wa kuhakikisha kwamba, Kanuni, Sheria na Taratibu hizi mpya zinafuatwa na kutekelezwa kikamkilifu. Baba Mtakatifu Francisko katika barua inayofafanua msingi wa maamuzi yake anasema kwamba, watangulizi wake walikuwa wametoa uamuzi wa kutumia Misale ya Kirumi ya zamani kama njia ya kuganga na kuponya utengano uliokuwa umejitokeza ndani ya Kanisa kwa Jumuiya ya Udugu wa Mtakatifu Pio X iliyoanzishwa na Askofu mkuu mstaafu Marcel François Marie Joseph Lefebvre kujitenga na Kanisa Katoliki.

Viongozi wa Kanisa wakapokea kwa mikono miwili ombi la waamini kuendelea kutumia Misale ile ya Kirumi. Lengo kuu lilikuwa ni kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa Kanisa katika Liturujia na Tasaufi. Bahati mbaya, matumizi ya Misale hii yalitafsiriwa vibaya kiasi kwamba, Misale ile ilianza kutumika sanjari na Misale ya Kirumi iliyochapishwa na kuidhinishwa na Mtakatifu Paulo VI. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI tarehe 7 Julai 2007 alichapisha Barua Binafsi, Motu Proprio “Summorum Pontificum” alikaza kusema, alitegemea kwamba, Mafundisho na Maamuzi yaliyotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yangefuatwa na kuheshimiwa, lakini mambo yalikwenda kinyume kabisa! Uchunguzi uliofanywa na Maaskofu baada ya miaka kumi na nne, unaonesha masikitiko makubwa kwa sababu anasema Baba Mtakatifu Francisko badala ya kujenga na kuimarisha umoja wa Kanisa, matokeo yake yakawa ni waamini hawa kuendelea kujitenga zaidi, kwa kupingana na Kanisa, hali ambayo inachangia kuzorota kwa maisha na utume wa Kanisa, kiasi cha kuhatarisha umoja na mshikamano wa Kanisa.

Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa kutumia Misale ya Kirumi ya Mwaka 1962 yalikataliwa na wala hawakuwa tayari kukubali na kupokea mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusiana na Liturujia ya Kanisa. Waamini hawa waliendelea “kujimwambafai” kwa kusema kwamba, wao ndilo “Kanisa la kweli.” Kutilia shaka maamuzi na mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ulioadhimishwa chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro “Cum Petro et sub Petro” ni sawa na kumtilia shaka Roho Mtakatifu anayeliongoza na kulitakatifuza Kanisa. Inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya waamini wameendelea kutumia Vitabu vilivyochapishwa kabla ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kiasi cha kushindwa kufuata Sheria, Taratibu na Kanuni za Kanisa kwa kudhani kwamba, wao ndio “Kanisa la kweli”. Hii ni tabia inayokwenda kinyume kabisa cha umoja na mshikamano wa Kanisa na matokeo yake ni kuendelea “kuwasha moto wa utengano ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ili kulinda umoja na mshikamano wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa, analazimika kufuta vibali vilivyokuwa vimetolewa na watangulizi wake.

Walinzi wa Mapokeo
17 July 2021, 09:29