Papa Francisko aguswa sana na salam kutoka kwa watoto wagonjwa wa Saratani pamoja na Maskini wa mji wa Roma. Kielelezo cha mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Papa Francisko aguswa sana na salam kutoka kwa watoto wagonjwa wa Saratani pamoja na Maskini wa mji wa Roma. Kielelezo cha mshikamano wa udugu wa kibinadamu. 

Afya ya Papa Francisko: Aguswa na Ujumbe wa Watoto na Maskini!

Watoto wagonjwa wa Saratani wanasema katika shida na mahangaiko yao, wamekuwa wakifarijika kwa sala kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Huu ni wakati wao, kusali na kumwombea apone haraka, ingawa kwa sasa mazingira hayawaruhusu kumtembelea mubashara, lakini wanamwombea apone haraka. Maskini wa Roma wanamwombea pia! Udugu wa kibinadamu katika utu

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, anawaalika Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujifunza kutoka kwenye shule ya maskini, kwani kati ya maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum, humu humu kuna watakatifu na watu ambao wanaweza kuwafundisha wengine tunu msingi za maisha ya kijamii, kiutu na kiroho. Maskini si mzigo bali ni shule makini kwa watu wa Mungu. Maskini ni kielelezo cha Kristo Yesu kati ya watu wake. Katika shule ya upendo, watu wanatafuta faraja, mahusiano na mafungamano; utu na heshima ya binadamu na kwa njia hii, waamini wanaweza kujifunza kutoka kwa maskini kwa kuwakaribisha, kuwasikiliza, kuwakirimia na kuwahudumia kwa upendo na nidhamu ya hali ya juu. Maskini ni: rasilimali, amana na utajiri wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kimsingi, maskini ndio walengwa wakuu wa Injili. Dhana ya umaskini inajikita katika umaskini wa hali na mali; maadili na utu wema; kwani wote hawa, Kristo Yesu amejisadaka kwa ajili ya kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu.

Wakristo wanapaswa kuwajali, kuwathamini na kuwapenda maskini na watu wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama afanyavyo mama mzazi kwa watoto wake. Kanisa linatoa huduma ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa maskini, kwa kujali na kuthamini utu, heshima na haki zao msingi, kwani hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, maskini wa hali na mali amewapatia kipaumbele cha kwanza. Dr.  Matteo Bruni, Msemaji mkuu wa Vatican katika taarifa yake kuhusu hali ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 10 Julai 2021 anasema kwamba, Baba Mtakatifu anaendelea vyema na matibabu yake. Ameanza taratibu kufanya kazi, kusali pamoja na kushiriki chakula cha pamoja na wasaidizi wake wa karibu kwa wakati huu. Anasali Ibada ya Misa Takatifu na kufanya mazoezi ya kutembea kidogo kidogo. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anawasifu na kuwapongeza wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo kwa wagonjwa.

Hawa ni wale ambao wameamua kuchagua “Uso wa wale wanaoteseka” kwa kufungamana nao katika shida na mahangaiko yao; lakini, kubwa zaidi ni huduma kwa maskini na wale wasiokuwa na uwezo zaidi. Katika kipindi hiki cha ugonjwa na kulazwa hospitalini Gemelli mjini Roma, Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kupata ujumbe wa faraja, matashi mema pamoja na sala kutoka kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa, Viongozi wa kidini, waamini na watu wenye mapenzi mema.Kati ya makundi maalum ambayo yametuma ujumbe wa matashi mema ni watoto wagonjwa ambao wamelazwa kwenye Wodi ya Watoto Wagonjwa wenye saratani.

Wodi hii iko karibu sana na chumba ambacho Baba Mtakatifu Francisko amelazwa huko kwenye Hospitali ya Gemelli mjini Roma kuanzia Jumapili tarehe 4 Julai 2021. Watoto hawa wanasema, wanasali kwa ajili ya Baba Mtakatifu Francisko ili aweze kupona haraka na kurejea katika utume wake. Watoto wagonjwa wa Saratani wanasema katika shida na mahangaiko yao, wamekuwa wakifarijika kwa sala kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Huu ni wakati wao wa kusali na kumwombea apone haraka, ingawa kwa sasa mazingira hayawaruhusu kumtembelea na kumsalimia mubashara, lakini wanamwombea apone haraka. Hii ni kati ya barua ambazo zimegusa Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee. Watoto pia wamechora michoro inayoonesha nia yao ya kutaka kumfariji wakati huu ambapo amelazwa hospitalini hapo kama wao. Kwa namna ya pekee, mchoro wa Mtoto Giulia umewagusa wengi kwenye mitandao ya kijamii.

Ni katika muktadha huu, maskini wa jiji la Roma, wakiwa wamesindikizana na wafanyakazi wa kujitolea wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio mjini Roma, Ijumaa tarehe 9 Julai 2021 walikwenda kusali kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko na kumpelekea shada la maua ambalo limewekwa kwenye Kikanisa cha chumba chake, kama kielelezo chao cha upendo na mshikamano wa udugu wa binadamu. Walibeba mabango yanayosema, “Baba Mtakatifu Francisko tuko pamoja katika kipindi hiki kigumu”. Wanamwombea ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, apende kumkirimia afya njema na maisha tele. Maskini hawa hata katika umaskini wao wanatambua mchango wa Kanisa katika maisha, ustawi na haki zao binafsi. Baba Mtakatifu ameonesha ukaribu kwa maskini. Leo hii, wengi wao wamepata chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Afya ya Papa
10 July 2021, 14:48